Ufahamu ugonjwa uliomlaza Papa Francis siku nane hospitalini

Roma. Kiongozi wa Kanisa Katoliki duniani, Papa Francis (88) amelazwa hospitalini kwa wiki moja kutokana na kuugua ‘nimonia’ katika mapafu yote mawili, pamoja na maambukizi kwenye njia ya hewa, hali ambayo madaktari wanasema inaweza kutibiwa huku wakidokeza, magonjwa hayo ni hatari hasa kwa wazee.

Papa Francis alilazwa Februari 14, 2025, katika Hospitali ya Gemelli mjini Roma baada ya kugundulika kuwa na maambukizi kwenye mapafu, hali inayosababisha kuvimba kwa mirija maarufu kama ‘bronchi’ kwenye mapafu.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani aligunduliwa kuugua nimonia kwenye mapafu yote na maambukizi ya njia ya upumuaji yaliyochangiwa na vimelea mchanganyiko.

Jarida la ‘Everyday Health’ limechapisha kuhusiana na maambukizi yanayomtesa kiongozi huyo kuwa huweza kusababishwa na aina tofauti za bakteria, virusi au vimelea  vingine ndani ya mapafu.

Aimarika lakini yuko hatarini

Kwa mujibu wa ukurasa rasmi wa Vatican News, timu ya madaktari wa Papa walisema kuwa ingawa hali yake imeimarika lakini bado afya yake iko hatarini kutokana na maambukizi hayo.

Mkuu wa Timu ya Madaktari wanaomtibu Papa Francis, Dk Sergio Alfieri na Dk Luigi Carbone ambaye ni Naibu Mkurugenzi wa huduma za afya za Vatican, amesema Papa ataendelea kulazwa kwa angalau wiki nyingine moja.

Dk Alfieri amesisitiza kuwa Papa Francis hajawekewa mashine ya kupumulia ingawa bado anapata changamoto ya kupumua, huku madaktari wakimshauri kupunguza shughuli za kimwili.

Daktari huyo amesema Papa amekuwa akikaa kwenye kiti, akifanya kazi na hata akitaniana na watu wanaofika kumjulia hali hospitalini kama kawaida.

Mmoja wa madaktari wanaomtibu, alipomsalimia kwa kusema: “Hello, Baba Mtakatifu,” Papa alijibu kwa utani: “Hello, Mwana Mtakatifu,” amesema Dk Alfieri.

Madaktari walieleza kuwa hofu yao kubwa ni kwamba bakteria kwenye njia ya upumuaji ya Papa huenda wakaingia kwenye damu, hali ambayo inaweza kusababisha ugonjwa hatari wa maambukizi ya damu wa ‘sepsis.”

Lakini Dk Alfieri alisema ana imani kwamba Papa Francis ataondoka hospitalini na kurudi kwenye makazi yake huko Vatican.

Hata hivyo, aliongeza kuwa changamoto za kiafya za upumuaji zitabaki kuwa hali ya kudumu.

Kwa mujibu wa Vatican, Papa ameonyesha maendeleo mazuri katika siku za karibuni, anaamka kupata kifungua kinywa, anaendelea kupumua bila msaada wa mashine na moyo wake uko imara.

Miongoni mwa waliofika kumjulia hali hospitalini ni Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni aliyemtembelea Februari 19, 2025, kisha kuchapisha kwenye akaunti yake ya X kuwa hali ya kiafya ya Papa Francis inatia matumaini.

“Nilimkuta Papa Francis akiwa macho na mwenye kutia matumaini na alianza kujitania,” alisema Meloni.

‘Double Pneumonia’ ni nini?

Jarida la ‘Everyday Health’ limeandika kuwa ‘nimonia’ hutokea pale ambapo maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi yanaposababisha kuvimba na kujazana kwa majimaji kwenye mapafu.

Maambukizi haya yanaweza kuathiri pafu moja au yote mawili kwa wakati mmoja, hali hiyo kitaalamu ndiyo inaitwa ‘bilateral pneumonia’.

Kwa mujibu wa jarida hilo, visababishi vya kawaida vya nimonia ni pamoja na mafua ya msimu, Uviko-19 na ugonjwa wa pneumococcal unaosababishwa na maambukizi ya bakteria aina ya “streptococcus pneumoniae.”

“Dalili za nimonia ni pamoja na upumuaji wa shida, homa, kikohozi kinachotoa makohozi ya manjano, kijani au yenye damu. Kwa watu wazee dalili zinaweza pia kujumuisha mabadiliko ya ghafla ya hali ya akili, kukosa hamu ya kula na uchovu,” limeandika jarida hilo.

Kwa upande wake, Profesa mshiriki na Mkurugenzi wa Tiba ya Upumuaji katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Dk Meredith McCormack, anasema: “Nimonia ni maambukizi mazito yanayoweza kuhatarisha maisha.”

Dk McCormack amesema watu walio na zaidi ya miaka 65 huwa hatarini zaidi na kila mwaka wa ziada wa umri huongeza hatari ya kupata maambukizi mabaya zaidi kwenye mapafu.

“Kwa mgonjwa wa miaka 88 kama Papa, kiwango cha vifo kinaweza kufikia hadi asilimia 30,” anasema Dk Peter Chin-Hong ambaye ni mtaalamu wa Magonjwa ya Kuambukiza katika Chuo Kikuu cha California, San Francisco.

Hata hivyo, Vatican pia haijaeleza mchanganyiko wa vimelea vilivyogunduliwa kwenye maambukizi ya Papa Francis.

Dk McCormack anasema: “Antibiotiki au dawa za kuua bacteria ndio matibabu makuu. Wakati mwingine tunatumia dawa ya kuvuta inhalers au steroids hasa kwa wagonjwa wenye historia ya pumu au magonjwa sugu ya mapafu.”

Kulingana na Chama cha Mapafu cha Marekani, watu wengi wenye nimonia wanaweza kudhibiti dalili kwa kunywa maji mengi, kupumzika vya kutosha na kutumia dawa za kushusha homa na kikohozi.

“Matibabu saidizi ni muhimu,” anasema Dk McCormack huku akiongeza; “Hii inaweza kujumuisha kuwapa wagonjwa oksijeni au hata msaada wa mashine za kupumulia kwa wale walioko kwenye hali mbaya.”

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa Mashirika.

Related Posts