Serikali ya Rwanda imelaani vikali hatua ya Wizara ya Fedha ya Marekani ya kumwekea vikwazo Waziri wa Utangamano wa Kieneo wa Rwanda, Jenerali Mstaafu James Kabarebe, kwa tuhuma za kuhusika na mzozo na machafuko yanayoendelea mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo.
Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda imesema katika taarifa kuwa: “Hatua ya kuwekewa vikwazo Waziri wa Serikali, Jenerali Mstaafu James Kabarebe ai halali na wala haina msingi wowote.”
Taarifa ya wizara hiyo imeeleza bayana kuwa, “Iwapo vikwazo vingeweza kutatua mgogoro mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, tungelikuwa na amani katika eneo miongo kadhaa iliyopita.”
Aidha taarifa ya Wizara ya Mambo ya Nje na Ushirikiano wa Kimataifa ya Rwanda imeikosoa jamii ya kimataifa kwa kutochukua hatua za kivitendo za kujaribu kuzima mgogoro wa ukosefu wa usalama na ghasia mashariki mwa Kongo, unaochochewa na serikali ya DRC.
Mbali na Jenerali Kabarebe, Marekani imemuwekea vikwazo pia msemaji wa kundi la waasi wa M23, Lawrence Kanyuka, pamoja na kampuni nyingine mbili zinazodaiwa kufadhili na kuchochea mapigano mashariki ya DRC.