WATER AID NA HABITAT FOR HUMANITY WAJENGA VYOO ARUSHA DC

Na Mwandishi wetu, Arusha

Mashirika ya Water Aid na Habitat for Humanity Tanzania wamefanikiwa miradi ya ujenzi wa vyoo kwenye masoko ya Kata za Olmotonyi na Olturumet Mkoani Arusha.

Watumiaji na wafanyabiashara 5,000 wa masoko hayo, waliokosa huduma ya vyoo kwa muda mrefu wameondokana na tatizo hilo baada ya vyoo bora kuzinduliwa.

Mkurugenzi wa Taifa wa shirika la Habitat for Humanity Tanzania, Magdalena George amesema gharama za mradi huo ni Sh220 milioni kwenye masoko yote mawili.

Amesema wanatarajia miradi hiyo itakuwa endelevu kwani wamekabidhi ikiwa kwenye ubora na inapaswa kutunzwa.

Mkurugenzi mkazi wa shirika la WaterAid, Anna Mzinga amesema pamoja na vyoo hivyo, pia wamefunga miundombinu ya maji na eneo la wanawake kunyonyesha watoto.

“Karibuni katika hafla ya makabidhiano ya mradi wa vyoo rafiki kwa makundi ya jinsia zote kwa masoko mawili ya Olmotonyi na Olturumet ili kuboresha afya na ustawi wa wafanyabishara na wateja hususani wanawake na watoto,” amesema

Mkuu wa wilaya ya Arumeru, Amiry Mohamed Mkalipa amewaagiza vikundi vya wanawake ambao ndiyo wasimamizi wa masoko hayo kuhakikisha kuwa wanavitunza vyoo hivyo bora.

Mkalipa amezishukuru Water Aid na Habitat for Humanity Tanzania kwa kufanikisha miradi hiyo ya vyoo rafiki ya makundi ya jinsia zote.

“Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri hawa watu hawatakiwi kuondoka kaa nao mpange namna ya kufanya kwenye masoko mengine, hayo ni maelekezo yangu pia masoko yote yawe yanaendeshwa na vikundi vya wanawake,” amesema Mkalipa.

Mkurugenzi mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Arusha, Seleman Msumi amesema wataanda vyeti vya kuzishukuru asasi hizo kwa kuwajengea miradi hiyo katika masoko hayo na kuwakabidhi kwenye kikao cha baraza la madiwani..

“Pia tutarodhesha masoko yote ili tukae nao watuambie tufanye nini ili tujenge masoko yetu yote ya halmashauri ya wilaya ya Arusha ambayo hayana vyoo bora,” amesema Msumi.

Awali, wafanyabiashara wa masoko hayo na madereva wa kituo kidogo cha magari ya abiria wa maeneo hayo walikuwa wanakwenda korongoni au vichochoroni kujisaidia kutokana na ukosefu wa vyoo.

Mmoja kati ya wafanyabiashara wa masoko hayo, Neo Mollel amesema kwa miradi hiyo kuzinduliwa wanashukuru kwani watapata huduma kwenye vyoo bora.

Mollel amesema wanawashukuru Water Aid na Habitat for Humanity kwa kufanikisha miradi hiyo ambayo itasaidia kuondokana na uchafu kwema masoko hayo kutokana na awali watu kujisaidia ovyo.

“Watu walikuwa wanajisaidia haja kubwa na haja ndogo ovyo na kusababisha uchafu, hivyo kutupa hofu ya kupata maambukizi ya magonjwa ya milipuko ila sasa tunaondokana na hali hiyo,” amesema.

 

Related Posts