Zijue dalili zisizojulikana za mshtuko wa moyo

Dar es Salaam. Maumivu ya kifua na kupumua kwa shida ni dalili zinazojulikana za mshtuko wa moyo, lakini ni muhimu pia kuwa makini na dalili zisizojulikana kama mabadiliko ya rangi ya macho na miguu kuvimba, ameonya Daktari Bhavini Shah.

Moja ya dalili za ajabu ni hali inayojulikana kama digital clubbing, ambayo ni unene na upanukaji wa kucha.

Hii hutokea kwa sababu damu yenye oksijeni haifikii vidoleni ipasavyo na hivyo kusababisha mwili kutoa kwa wingi dutu inayochochea ukuaji wa tishu za kucha.

Dalili nyingine isiyojulikana sana ni mduara wa kijivu unaozunguka sehemu ya nje ya macho yenye rangi.

Takribani asilimia 45 ya watu wenye umri wa zaidi ya miaka 40 wana mduara huu wa mafuta kwenye iris yao, na idadi hii huongezeka hadi asilimia 70 kwa wale wenye zaidi ya miaka 60, kwa mujibu wa utafiti.

Uwepo wa mduara huu umehusishwa na ugonjwa wa moyo wa mishipa (coronary heart disease), kwani unaweza kuashiria kuwa kiwango cha cholesterol mwilini ni cha juu hali inayoweza kuziba mishipa ya damu.

Daktari Shah, ambaye ni daktari wa taasisi ya LloydsPharmacy ya nchini Uingereza, ameonya kuwa watu wanapaswa kuwa makini na miguu kuvimba, hali inayojulikana kitaalamu kama oedema.

Hii hutokea pale ambapo maji yanajikusanya kwenye tishu, kutokana na moyo kuwa dhaifu kushindwa kusukuma damu ipasavyo mwilini, na hivyo kusababisha kujikusanya kwa maji kwenye mishipa ya damu na tishu za miguu na nyayo.

Ugonjwa wa moyo, mara nyingi husababishwa na kujikusanya kwa mafuta kwenye mishipa ya damu, hali inayofanya iwe vigumu kwa damu na oksijeni kutiririka ipasavyo kupitia mishipa kuelekea na kutoka kwenye moyo.

Hii huongeza hatari ya mishipa kuziba na hivyo kusababisha kiharusi au mshtuko wa moyo.

Maumivu ya kifua yanayohisiwa kama shinikizo, kubana, kukandamiza au uzito kwenye kifua yanaweza kuwa dalili ya mshtuko wa moyo hivyo ni muhimu kuona wataalamu wa afya haraka.

Hii ni dalili inayotambulika zaidi, ambapo asilimia 80 ya watu waliohojiwa walitambua kuwa ni ishara kuu. Kupumua kwa shida ni dalili nyingine, ambayo asilimia 77 ya watu wanajua kuhusu.

Daktari Shah ameeleza kuwa kama moyo hauwezi kusukuma damu ipasavyo mwilini, maji yanaweza kujikusanya kwenye mapafu, na hivyo kufanya iwe vigumu kupumua.

Mapigo ya moyo yasiyo ya kawaida pia yanaweza kuwa ishara ya ugonjwa wa moyo, jambo ambalo asilimia 70 ya watu wanatambua.

Ingawa hali hii huenda isiwe na uhusiano wa moja kwa moja na tatizo kubwa, ni muhimu kufanyiwa uchunguzi ili kuelewa chanzo chake.

Uchovu wa kupindukia unaofanya kazi za kila siku au mazoezi mepesi kuwa magumu pia ni dalili ya hatari.

Lakini ni asilimia 66 pekee ya watu waliohojiwa waliokuwa wakifahamu kuhusu dalili hii.

Jinsi ya kuzuia ugonjwa wa moyo

Daktari Shah amesisitiza kuwa kuna mambo ya mtindo wa maisha ambayo tunapaswa kuzingatia ili kuzuia ugonjwa huu, moja wapo ni kupunguza ulaji wa vyakula vyenye mafuta.

“Kupunguza ulaji wa mafuta ni njia bora ya si tu kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo wa mishipa, bali pia kusaidia kupunguza shinikizo la damu na kiwango cha cholesterol,” amesema.

Kwa mujibu wa NHS, lishe yenye nyuzinyuzi nyingi na mafuta kidogo inapendekezwa, na inapaswa kujumuisha angalau viwango vitano vya matunda na mboga kwa siku, pamoja na nafaka kamili kama shayiri, rye na mchele wa kahawia.

NHS pia inapendekeza kupunguza ulaji wa chumvi hadi gramu sita kwa siku na kuepuka mafuta yaliyojaa (saturated fats), kwani yanaweza kuongeza kiwango cha cholesterol mwilini.

Kufanya mazoezi mara kwa mara kunaweza kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo kwa hadi asilimia 35, kulingana na British Heart Foundation.

Daktari Shah amesema mazoezi kama kutembea, kuendesha baiskeli, kuogelea au kuhudhuria darasa la mazoezi yanaweza kusaidia kudhibiti shinikizo la damu na kupunguza cholesterol.

Kuacha kuvuta sigara pia kunaweza kupunguza hatari ya ugonjwa wa moyo. Hii ni kwa sababu sigara huharibu ukuta wa mishipa ya damu, ikiwemo mishipa ya moyo.

Pia, kemikali inayoitwa acrolein huvuruga uwezo wa mwili wa kushughulikia cholesterol, na hivyo kusababisha kuongezeka kwa kiwango chake kwenye damu, Daktari Shah ameonya.

Kunywa pombe kupita kiasi pia ni hatari ya ugonjwa wa moyo, na Daktari Shah amesema kunywa zaidi ya kikomo cha uniti 14 kwa wiki kwa muda wa miaka 10 kunaweza kuongeza hatari ya kupata ugonjwa wa moyo au kiharusi.

Related Posts