Andambwile aamua kikubwa, atangulia TFF

KIUNGO wa Singida Black Stars, Aziz Andambwile anayeitumika Yanga kwa mkopo ameshtukia jambo na fasta akaamua kufanya kitu ili kutaka kujiweka pazuri kabla mambo hayajamchachia zaidi.

Andambwile mwenye mkataba wa miaka mitatu na Singida iliyopo nafasi ya nne katika msimamo wa Ligi Kuu Bara ikiwa na pointi 38 kutokana na mechi 21, bado hajaonyesha makeke akiwa na kikosi cha Yanga kwa vile alikuwa majeruhi kwa muda mrefu na sasa amepona akimsikilizia kocha Miloud Hamdi.

Kiungo mkabaji huyo imedaiwa amewasilisha barua rasmi Shirikisho la Soka Tanzania (TFF), akiomba kuvunja mkataba wa miaka mitatu alionao na Wauza Alizeti hao.

Andambwile amechukua uamuzi huo ikiwa ni miezi minane tu tangu aliposaini mkataba na Singida BS, kabla ya kuhamia Yanga kwa mkopo, jambo lililozua maswali mengi kuhusu hatma yake.

Kiungo mkabaji huyo anayemudu pia kucheza kama beki wa kati, amekosa namba Yanga kutokana na kukumbwa na majeraha yaliyomweka nje ya uwanja tangu timu hiyo ikiwa chini ya Miguel Gamondi aliyeondolewa kumpisha Sead Ramovic ambaye naye ametimka CR Belouizdad ya Algeria.

Andambwile amethibitisha juu ya taarifa hiyo na kufafanua amefanya uamuzi huo kutokana na baadhi ya vipengele muhimu vya mkataba kutotekelezwa na Singida inayoshika nafasi ya nne katika Ligi Kuu.

Kiungo huyo alisema; “Ni kweli tumeenda TFF kuwasilisha maombi ya kuvunja mkataba wangu na Singida BS. Hivyo tusubiri kuona nini kitatokea, lakini ukweli ni kwamba kuna vitu ambavyo havipo sawa na siwezi kwa sasa kuviongelea kwa uwazi,” alisema Andambwile alipotafutwa na Mwananchi.

Kwa mujibu wa taarifa kutoka Kamati ya Sheria na Hadhi za Wachezaji ya TFF, ambayo inasimamiwa na Mwenyekiti Said Soud, malalamiko ya Andambwile ni kati ya mengi ambayo wamepokea na wataendelea kuyapitia ili kuyashughulikia.

Hii inakuja ikiwa ni muda mfupi tu baada ya mchezaji mwingine wa Singida BS, Benson Mangolo, kuachana na klabu hiyo. Mangolo ambaye ni beki wa kushoto kutoka Botswana, alivunja mkataba wake na kurejea nyumbani kwao.

Tofauti na Andambwile, Mangolo aliketi na viongozi wa klabu hiyo na kufikia makubaliano ya kumaliza mkataba wao kwa njia ya amani. Kwa sasa, Singida Black Stars bado haijapokea barua rasmi kutoka TFF kuhusu maombi ya Andambwile.

Kwa upande wa Andambwile, kumekuwa na matumaini ya kurejea uwanjani, huku akiwa na imani ya kupata nafasi baada ya kupona majeraha chini ya kocha Miloud Hamdi, hata hivyo nyota huyo wa zamani wa Mbeya City ana kibarua cha kupigania ili kupata namba kikosi cha kwanza cha timu hiyo.

Mwanzoni mwa msimu, Gamondi alijaribu kumtumia Andambwile kwenye eneo la beki wa kati lakini kiuhalisia, ni kiungo mkabaji nafasi ambayo kwa Yanga imekuwa ikichezwa na Khalid Aucho.

Kabla ya kutua Yanga, Andambwile alijitengeneze jina akiwa na Mbeya City na kuivutia Singida Big Stars kumsajili na kuitumikia misimu miwili iliyopita kabla ya timu hiyo kubadilishwa jina msimu uliopita ikifahamika kama Singida Fountain Gate na Julai 9 mwaka huu, ndipo alipojiunga na Yanga kwa mkopo.

Mbali na kucheza nchini, rekodi zinaonyesha Andambwile amewahi kukipiga Malawi katika timu mbili tofauti za Kalonga Utd na Nyasa Big Bullets kabla ya kusajiliwa na Mbeya City msimu wa 2020-2021.

Hakuna kiongozi wa Singida BS aliyepatikana kufafanua juu ya madai hayo ya Andambwile, lakini kesi hiyo tayari ipo Kamati ya Sheria na Hadhi ya Wachezaji ili kuanza kusikilizwa na kutolewa uamuzi.

Related Posts