NA BALTAZAR MASHAKA, MWANZA
MKURUGENZI wa Kivulini,Yasin Ally, amesema ili vijana wa Kiislamu wapate maendeleo na kushindana kimataifa,ni muhimu BAKWATA na Jumuiya ya Kuendeleza Qu’ran na Sunna Tanzania (JUQUSUTA), kubadili mifumo ya elimu ya madrasa, ikiwemo kuingiza lugha ya Kiingereza katika ufundishaji wa Qur’an.
Yasin amesema leo,katika Kongamano la Vijana wa Kiislamu mkoani Mwanza,lililoandaliwa na JUQUSUTA kwa ajili ya kupokea mwezi Ramadhani kuwa viongozi wa BAKWATA na jumuiya za Kiislamu wanatakiwa kuongeza juhudi za kiuchumi na kiufundi kwa walimu wa madrasa.
Amesema JUQUSUTA itoke katika sifa na vigezo vya sasa vya kuwapata walimu wa madrasa ili kuwasaidia watoto wa Kiislamu,badala ya kuwakaririsha Qu’ran kwa Kiarabu,itumike lugha ya Kiingereza kuwawezesha kushindana kimataifa.
“Uendelezaji wa Qu’ran kwa Kiarabu hautakuwa na tija,tengenezeni mifumo mipya ya ujenzi wa walimu wa madrasa waendane na hali ya sasa, tuwafundishe Kiingereza watoto wa Kiislamu hapo tutakuwa tumewasaidia,”amesema Yasin na kuongeza;
“BAKWATA na JUQUSUTA tuwajengee walimu stadi za kiuchumi wawe na ujuzi na maarifa mengine,yatakayowafanya watengeneze mbinu ya kujikimu ili kuzifanya madrasa ziwe endelevu badala ya kuzitegemea kuendesha maisha yao.”
Pia, amesisitiza kuimarisha stadi za kiuchumi kwa walimu wa madrasa ili kuweza kufikia malengo ya kimaendeleo ya BAKWATA na uislamu, huku akitahadharisha endapo wataendelea kutegemea mfumo wa sasa, walimu wa madrasa watakuwa tegemezi na hawatakuwa na uwezo wa kujikimu kiuchumi.
Akizungumzia umuhimu wa matumizi ya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (TEHAMA) amesema ni fursa kwa maendeleo ya Uislamu, na akazitaka taasisi hizo kuandaa mikakati ya kuwawezesha vijana na walimu katika nyanja hizo.
Kwa upande wake, Mlezi wa JUQUSUTA Sheikh Hasani Kabeke, amesema kongamano hilo linawalenga vijana wa Kiislamu,ambao wengi wao wapo mitaani na wanakosa ajira au nafasi ya kushiriki kwenye maendeleo ya jamii.
Ameonya kuhusu hatari ya vijana kushawishika kufanya fujo au kuhusika na maandamano ya kisiasa,akisema kuwa lengo la kongamano ni kulinda amani na utulivu wakati wa uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika mwaka.
“Mwaka huu umepambana na Uchaguzi Mkuu,tuna mada mbalimbali na walengwa ni vijana na kwa nini vijana.Vijana wa Kiislamu wengi wao wako mitaani hawana ajira ,”amesema.
Sheikh huyo wa Mkoa wa Mwanza,ameonya kuelekea uchaguzi mkuu asitokee mtu wa kuwahamasisha vijana kuandamana,kufanya fujo na kugomea uchaguzi, wakatae kwani watakaodhurika ni vijana walio mitaani wakiwemo waislamu.
“Tunaowajibu wa kuwalinda na kukemea vijana kwa sababu lengo letu ni kulinda amani na utulivu na kjuiombea nchi kama ilivyo kauli mbiu ya kongamano hili ‘Kuna Maisha baada ya Uchaguzi;Linda Amani,Chagua kwa Hekima’,amesema Sheikh Kabeke na kuongeza;
“Kuiombea nchi hasa aliyepewa dhamana ya kuiongoza.Rais Dk.Samia Suluhu Hassan,hatumwombei kwa vile ni Mwislamu,la tunamwombea kwa vile ni Rais wan chi kama walivyombewa wengine (Hayati Baba wa Taifa Mwalimu Julisu Nyerere na wengine”.
Amesema Rais Samia ni mtawala na kiongozi, hivyo asionewe kwa sababu ya imani yake na nchi inaombewa ipite salama katika uchaguzi mkuu wa mwaka huu ikiwemo kuiepusha na fujo na kila aina ya ghasia.
“Ninatoa wito kwa jamii ya Kiislamu kuungana ili kuhakikisha vijana wanapata elimu bora, ujuzi na fursa za kiuchumi waweze kujitegemea na kuwa na mchango mzuri katika maendeleo ya taifa,”amesema Sheikh Kabeke.