NYOTA wa Kitanzania, Clement Mzize ndilo jina ambalo linatembea kwa sasa vinywani mwa mashabiki wa Yanga, nyota yake ikizidi kung’ara kutokana na mchango wake katika kikosi hicho cha mabingwa watetezi wa Ligi Kuu Bara, ambapo tayari keshahusika na mabao 10 na asisti zake tatu.
Lakini, unapomtafakari Mzize, mshambuliaji nyota mzawa mwenye umri mdogo anayetesa katika kikosi hicho akifanya vizuri kwa sasa, elewa kwamba mezani kwake na mabosi wa klabu hiyo kuna ofa kibao zinazoitaka saini yake ili akakipige nje ya mipaka ya Tanzania ambako kuna timu za kuanzia Afrika Kaskazini hadi Kusini zinamtaka.
Lakini, wakati huo pia elewa kwamba misimu ya hivi karibuni kumekuwa na ushindani baina ya wazawa na wageni kuwania kiatu cha ufungaji bora, awamu hii anayepewa nafasi kubwa ni Mzize anayebebwa na aina ya mabao aliyoyafunga.
Staa wa zamani wa Simba, Yanga na Taifa Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ amesema: “Mzize amekuwa na mwendelezo mzuri tangu apandishwe kutoka Yanga B, jambo la msingi ajue anataka nini, naamini atafanikiwa na kufanya makubwa, naona ana nafasi ya kukichukua kiatu endapo akiwa na muendelezo wa kiwango chake.”
Kanuni ya 11 (Vikombe na Tuzo) 13.1 inayosema mabao yalifungwa kwa njia kawaida yatahesabika kwa pointi mbili, mabao yaliyofungwa kwa njia ya penalti yatahesabiwa kwa pointi moja, hivyo ikitokea wafungaji wakagongana atakayechukua kiatu itatumika kanuni hiyo kuamua.
Kanuni hiyo iliboreshwa msimu wa 2022/23 baada ya aliyekuwa straika wa Yanga Fiston Mayele na mchezaji wa zamani wa Simba, Said Ntibazonkiza ‘Saido’ kila mmoja kufunga mabao 17 ingawa Saido baadhi ya mabao yake yalikuwa ya penalti.
Katika mabao 10 ya Mzize hakuna alilofunga kwa penalti hivyo ana pointi 20, wakati mabao tisa ya mshambuliaji wa Simba raia wa Cameroon, Leonel Ateba manne yakiwa ya penalti na sita kafunga kawaida hivyo anakuwa na pointi 16.
Mzize amekuwa na muendelezo mzuri kwani msimu uliopita alicheza dakika 1299, alifunga mabao sita, asisti 7, alicheza mechi 29, mipira iliyolenga lango 23 na iliyotoka nje 18, kiwango kilichozishawishi timu za nje kuhitaji huduma yake kama Wydad AC Kaizer Chiefs ya Afrika Kusini.
Misimu ya hivi karibuni kumekuwa na kupokezana kuchukua kiatu baina ya wazawa na wageni, jambo ambalo wadau wanaona Mzize akikaza buti anaweza akaendeleza kile walichokifanya wenzake.
Msimu wa 2020/21 aliyekuwa mshambuliaji wa Simba, John Bocco na sasa anacheza JKT Tanzania,alimaliza na mabao 16, akapokea kijiti George Mpole akiwa Geita msimu wa 2021/22 akimaliza na mabao 17, baada ya hapo 2022/23 wakachukua Mayele na Saido kila mmoja akifunga mabao 17 na uliopita 2023/24 alichukua Stephane Aziz Ki wa Yanga alimaliza na mabao 21.
Kabla ya Bocco na Mpole kutamba kama wazawa nyuma yake alitamba Meddie Kagere akiwa Simba (2018/19, mabao 23, 2019/20 mabao 22) na 2017/18 alichukua Emmanuel Okwi wa Simba kwa mabao 19 rekodi zinazoonyesha jinsi ambavyo wazawa na wageni wanapokezana kuchukua kiatu cha ufungaji bora.
Beki wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Nurdin Bakari alisema hivi karibuni ameona ushindani wa wazawa na wageni jinsi wanavyoshindana kuchukua kiatu cha ufungaji bora, akimtaka Mzize kuongeza bidii ili iwe msimu wa kuandika rekodi yake.
“Mzize kwa sasa anafanya vizuri, ajitunze na apambane kuhakikisha anaingia katika kitabu cha wafungaji bora wa misimu tofauti, kwani kuna vitu katika mpira havijirudii,” alisema beki huyo.
Mchezaji mwingine aliyechangia hiyo ni kiungo wa zamani wa Simba, Yanga na Stars, Haruna Moshi ‘Boban’ alisema “Mzize amekuwa na muendelezo mzuri tangu apandishwe kutoka Yanga B, jambo la msingi ajue anataka nini, naamini atafanikiwa na kufanya makubwa, naona ana nafasi ya kukichukua kiatu endapo akiwa na muendelezo wa kiwango chake.”