Dar es Salaam. Kampuni ya Ujenzi na Ukarabati wa Miundombinu ya Usafirishaji na Usambazaji wa Umeme nchini (ETDCO) imebuka mshindi katika kipengele cha mkandarasi bora wa ujenzi wa miundombinu ya umeme, katika Tuzo za Zanzibar International Construction Awards (ZICA), zilizofanyika usiku wa kuamkia leo Jumapili, huko Zanzibar.
Akizungumza wakati akikabidhi tuzo kwa washindi jana Jumamosi Februari 22,2025 Waziri wa Ujenzi, Mawasiliano na Uchukuzi Zanzibar, Dk Khalid Salum Mohamed, amesema sekta ya ujenzi ni msingi mkuu wa maendeleo ya kiuchumi na kijamii, huku akiwataka washiriki wote kutumia tuzo hizo kama chachu ya kuendelea kufanya kazi kwa bidii ili kufikia viwango vinavyohitajika na kuleta tija kwa Taifa.
Kaimu Meneja Mkuu wa ETDCO, Sadock Mugendi ameishukuru ZICA kwa kutambua mchango wao katika sekta ya ujenzi wa miundombinu ya umeme nchini, huku akiahidi kuendelea kutoa huduma zenye viwango ili kukuza uchumi wa nchi.
“ETDCO tumejipanga kuhakiksha tunaboresha matumizi ya teknolojia kwa kununua mashine za kisasa pamoja na kuwajengea uwezo wataalamu ili kufikia viwango vinavyohitajika kimataifa,” amesema Mugendi.
Amesema ETDCO ni kampuni tanzu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco) iliyopewa jukumu la kutekeleza miradi ya ujenzi na ukarabati wa miundombinu ya umeme kupitia wadau mbalimbali ukiwamo Wakala wa Nishati Vijijini (REA) na kampuni binafsi.
Katika tuzo hizo jumla ya washiriki 150 na waliingia kwenye kinyang’anyiro na ETDCO ikawa miongoni mwa washindi 30 waliotunukiwa tuzo hizo kutokana na ufanisi wa kazi pamoja na juhudi za kuhakikisha miundombinu ya usafirishaji na usambazaji wa umeme inakuwa bora na salama.
Mugendi amesema lengo ni kutaka Watanzania wapate umeme wa uhakika wakati wote ili kuchochea maendeleo ya uchumi kwa wananchi.
Mmoja wa waliohudhuria utoaji wa tuzo hizo, Zainabu Mohhamed amesema mbali ya kupatiwa tuzo, kampuni hiyo inapaswa kuongeza juhudi ya kukarabati na kujenga miundombinu hiyo ya umeme ili hali ya upatikanaji wa umeme wa uhakika iwe imara.
“ETDCO wanastahili kupata tuzo kwa hili ya upatikanaji wa umeme ilivyo sasa, japokuwa bado haijatengamaa, lakini imeanza kuleta matumaini ukulinganisha na kule tulikotoka,” amesema.