Arusha. Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo amefichua taarifa za wizi wa fedha kiasi cha Sh252 milioni zilizobambikwa kwenye mahitaji ya manunuzi ya eneo la ekari sita kwa ajili ya ujenzi wa shule katika kata ya Muriet jijini Arusha.
Wizi huo unadaiwa kutaka kutekelezwa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya jiji la Arusha, baada ya kudai Sh552 milioni zilitakiwa kulipwa katika ununuzi wa eneo hilo badala ya thamani halisi ya Sh300 milioni.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara wa wananchi wa Mtaa wa Muriet Mashariki kwenye eneo hilo lililonunuliwa leo Jumapili Februari 23, 2025.
Amesema eneo hilo lilikuwa linunuliwe mda mrefu lakini kutokana na mvutano wa kuokoa fedha za serikali, ilisababisha lichelewe.
Eneo hilo ambalo lilipangwa kununuliwa mwaka 2022, hatimaye limefanikiwa kununuliwa Desemba 2024.
“Tunatambua changamoto mnazopitia, lakini mojawapo ilikuwa ni jaribio la ufisadi katika suala la fedha, hali iliyotufanya kusimama kidete kuzuia wizi wa zaidi ya Sh252 milioni. Baadhi ya watendaji wasio waaminifu walidai kuwa eneo hilo linauzwa kwa Sh552 milioni badala ya thamani yake halisi ya Sh300 milioni,” amesema Gambo, na kuongeza:
“Tulichukua hatua hii kwa sababu tunatambua juhudi kubwa zinazofanywa na Rais wetu, Samia Suluhu Hassan, katika kutafuta fedha kwa ajili ya maendeleo ya Watanzania. Hivyo, ni wajibu wetu kama wasaidizi wake kuhakikisha fedha hizo zinasimamiwa na kutumika kwa malengo yaliyokusudiwa.”
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Maendeleo ya Jamii wa Jiji la Arusha, Issaya Doita ameleza namna njama hizo zilivyogunduliwa.
Amesema mwaka 2022, walipokea maombi ya uhitaji wa shule katika eneo la Muriet Mashariki, na baraza la madiwani likaidhinisha ajenda hiyo. Hata hivyo, tathmini ya awali ya wataalamu wa ununuzi ilionyesha eneo hilo linagharimu Sh552 milioni.
“Wengi wetu tulishangazwa na bei hiyo kwa kuwa eneo lenyewe liko pembezoni. Baadhi yetu, wakiwamo wabunge, tulifanya uchunguzi wa kina na kugundua mnyororo wa madalali waliokuwa wakishirikiana na baadhi ya watendaji wa halmashauri na madiwani kupandisha bei. Tulitoa taarifa kwa Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) na hatua za kisheria zikachukuliwa. Hatimaye, eneo lilinunuliwa kwa gharama halisi ya Sh300 milioni kwa kushirikiana na mkurugenzi wa wakati huo, Juma Hamsini,” amesema.
Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude ameeleza kuridhishwa kwake na hatua zilizochukuliwa kuhakikisha eneo hilo linanunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa shule.
“Sasa eneo lipo, kinachofuata ni kuhakikisha ujenzi wa shule unakamilika haraka ili kupunguza changamoto wanazokumbana nazo wananchi, ikiwemo watoto kutembea umbali mrefu na kuhatarisha maisha yao kutokana na ajali za barabarani,” amesema.
Mmoja wa wakazi wa mtaa huo, Rukia Mohames ameishukuru serikali kwa kufanikisha ununuzi wa eneo hilo, lakini ameomba ujenzi wa shule uanze haraka.
“Tunashukuru kwa hatua hii, lakini watoto wetu bado wanakabiliwa na changamoto kubwa ya kusafiri zaidi ya kilomita 20 kwenda shule, wakihatarisha maisha yao na kuongezewa mzigo wa gharama za usafiri kwa kutumia daladala mbili hadi tatu,” amesema.
Diwani wa kata hiyo, Francis Mbise amesema Sh252 milioni kilichosalia kimependekezwa kutumika kuanza ujenzi wa shule huku wakisubiri bajeti zaidi.
“Jumatatu tunaanza kikao cha mapendekezo ya bajeti ya mwaka 2025/2026, na tunaamini kuwa bajeti hiyo itaidhinishwa ili tuanze ujenzi wa shule mara moja,” amesema.