Hali ya Papa Francis yabadilika, Vatican yadai ‘yuko mahututi’

Rome. Vatican imesema Papa Francis, ambaye amelazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki moja, bado yuko katika hali ya “mahututi” huku akipatwa na changamoto katika mfumo wa upumuaji, ‘pumu.’

“Asubuhi ya leo (jana), Papa Francis alipata changamoto ya kupumua kwa kiwango kikubwa, ambayo pia ilihitaji matumizi ya oksijeni kwa kiwango cha juu,” iliandika taarifa ya Vatican kuhusu hali ya kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki aliyelazwa Hospitali ya Gemelli mjini Roma.

Taarifa hiyo pia imesema, ingawa Papa Francis alikuwa macho huku akitumia kiti cha kusukumwa kwa mikono, alipoketi kwenye kiti hicho alidai kupata maumivu makali mwilini mwake zaidi ya Ijumaa.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, kiongozi huyo wa kiroho pia aliongezewa damu ili kutibu tatizo la anemia lililomkumba.

Mapema Jumamosi, Vatican ilisema atabaki hospitalini baada ya kukumbwa na nimonia na hataweza kuongoza sala ya kila wiki ya Angelus, ikiwa ni mara ya tatu tu katika karibu miaka 12 ya huduma yake kama Papa.

Hali ya Papa ilionekana kuwa inaimarika mapema wiki hii, huku Vatican ikieleza kuwa alikuwa akionyesha matumaini kwenye matibabu ya nimonia.

“Je, Papa yuko nje ya hatari? Hapana. Milango yote miwili iko wazi. Je, yuko kwenye hatari ya kifo cha ghafla? Hapana. Tiba inahitaji muda kufanya kazi,” alisema Sergio Alfieri, ambaye ni daktari wa upasuaji aliyemfanyia upasuaji Papa hapo awali.

Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki alilazwa hospitalini jijini Roma Februari 14 na awali alifanyiwa vipimo vya maambukizi kwenye njia ya upumuaji. Baadaye aligunduliwa kuwa na nimonia katika mapafu yote mawili baada ya kufanyiwa kipimo cha CT.

Francis, ambaye anatoka Argentina, ana udhaifu wa kupumua. Akiwa kijana, aliwahi kuugua nimonia kali iliyosababisha kuondolewa kwa sehemu ya pafu lake moja.

Mwaka 2021, madaktari pia walimfanyia upasuaji wa kuondoa sehemu ya utumbo mpana kutokana na ugonjwa uitwao Diverticulitis, ambao unaweza kusababisha uvimbe au maambukizi ya utumbo.

Alilazwa hospitalini kwa sababu ya changamoto ya bronchitis mwaka 2023, na katika miezi ya hivi karibuni alikumbwa na ajali mbili ambapo aliumia kidevu na mkono wake.

Huu ni muda wa tatu mrefu zaidi kwa Papa Francis kuutumia hospitalini tangu achaguliwe kuwa Papa.

Madaktari wake wamemshauri kupumzika kabisa. Hata hivyo, akiwa hospitalini alikuwa anaendelea na baadhi ya kazi, ikiwa ni pamoja na siku mbili za kwanza hospitalini ambapo alipiga simu yake ya kila siku kwa Mchungaji Gabriel Romanelli na msaidizi wake, Padre Yusuf Asad, huko kaskazini mwa Gaza.

Wamekuwa wakiwasiliana mara kwa mara tangu Israeli ilipoanzisha mashambulizi yake eneo la Gaza nchini Palestina dhidi ya Hamas Oktoba 7, 2023.

Francis pia ameendelea kusaini maamuzi akiwa hospitalini, msemaji wa Vatican Matteo Bruni aliambia CNN.

Hadi sasa, ni wasaidizi wake wa karibu pekee waliomtembelea, msemaji huyo wa Vatican aliieleza CNN.

Jumatano, Waziri Mkuu wa Italia, Giorgia Meloni, alimtembelea na kumjulia hali kwa dakika 20.

“Tulitania kama kawaida. Hajapoteza ucheshi wake wa kawaida,” waziri mkuu huyo alisema katika taarifa yake kwa umma.

Taarifa zinadai kuwa waumini wamekusanyika nje ya miji mikuu ya Italia na Argentina na kwenye makanisa wakiwa na mishumaa ili kumuombea kiongozi huyo arejee kwenye hali ya utimamu wa kiafya.

“Daima tunamweka katika nia zetu,” alisema Rodomina Valdez, raia wa Argentina (45) katika Kanisa Kuu la Metropolitan, jijini Buenos Aires nchini humo.

“Lakini tunachoweza kufanya ni kumweka katika sala zetu na kutoa kafara au hata kufanya toba kwa njia yoyote,” aliongeza.

Imeandikwa na Mgongo Kaitira kwa msaada wa mashirika.

Related Posts