Haya ndio matarajio ya Serikali mashindano ya Qur’an

Dar es Salaam. Waziri Mkuu wa Tanzania, Kassim Majaliwa, amesema Serikali inatarajia kuona elimu ya Qur’an ikianza kutolewa mapema kwa watoto wadogo ili kuwapa misingi bora ya maadili.

Amesema hayo leo Jumapili Februari 23, 2025, kwenye mashindano ya dunia ya kuhifadhi Qur’an yaliyofanyika Uwanja wa Benjamin Mkapa, Dar es Salaam.

“Mashindano haya yataendelea kuleta maendeleo ya kiroho kwa vijana wetu na kuhamasisha jamii kwa ujumla wake. Pia Serikali tutaendelea kushirikiana na Jumuiya hii na taasisi za kiislamu zinazoendesha mashindano hayo kwa leongo la kuhamasisha na kukuza shughuli za kidini,” amesema.

Majaliwa alisema mashindano hayo yatakuza maendeleo ya kiroho na kuhamasisha jamii kuanzisha madrasa kwa watoto.

Amesisitiza kuwa elimu ya dini ni jukumu letu sote, na ametoa wito kwa viongozi wa dini kuimarisha elimu ya dini katika shule, vyuo, na taasisi mbalimbali ili kuandaa vijana wenye maadili.

“Nitoe wito kwa viongozi wa madhehebu ya dini kuendelea kufundisha na kuimarisha elimu ya dini katika shule vyuo na taasisi mbalimbali ili kuwapata vijana walio bora na kwa kuwaandaa kuwa watu wema,” amesema.

Aidha, amehimiza viongozi wa dini kuendelea kuhamasisha amani na utulivu nchini ikiwa ni tunu muhimu na hususani katika kipindi hiki cha kuelekea Uchaguzi Mkuu.

Awali, Mufti wa Tanzania, Abubakar Zuber, alisisitiza umuhimu wa kudumisha amani katika taifa.

Katika mashindano hayo, Nadhiru Ishengoma kutoka Mbagala Chamazi, Dar es Salaam, alishinda gari.

Washiriki 17 walishiriki kutoka nchi mbalimbali, ikiwemo Jordan, Yemen, Marekani, Syria, Kuwait, Kenya, Uganda, na Tanzania.

Related Posts