KONA YA MZAZI: Mwandae mtoto hivi kuishinda vita ya rika balehe

Rika balehe ni kipindi cha mpito kinachobeba changamoto nyingi kwa vijana, ikiwa ni pamoja na mabadiliko ya kimwili, kihisia, na kijamii.

Balehe ni hatua muhimu katika maisha ya kijana na wazazi wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwaongoza watoto wao kwa upendo, hekima na uvumilivu.

Lakini inaelezwa ndiyo kipindi cha kuwapatia elimu sahihi, kuwaelekeza kwenye maadili na kushirikiana nao kwa karibu, vijana wataweza kuepuka matendo maovu na kubaki kuwa watu wenye nidhamu, heshima na maadili katika jamii.

 Hivyo wazazi hasa wa kizazi cha sasa, wakilitambua hili, wanapaswa kuwa mstari wa mbele katika kuwaelekeza watoto wao kusudi waepuke matendo maovu yakiwamo ya uzinzi, na badala yake wajikite katika maadili.

Kuna siku nilizungumza na mtaalamu mmoja wa malezi, Jakson Kalikamkana nikamuhoji, katika hali kama hii, mzazi afanyaje ili amsaidie mwanaye asitumbukia katika balaa.

Akasema kuna zipo njia kadhaa ambazo mzazi anaweza kutumia kumsaidia mwanawe kubaki kijana mwema.

Nazo ni pamoja na kujenga uhusiano wa karibu na mtoto wake kwa kumfanya ahisi kuwa sehemu ya familia.

Muda wa mazungumzo na ushirikiano kati ya mzazi na mtoto hutoa nafasi ya kuelewa changamoto anazopitia na kumpa mwongozo sahihi.

Anasema mzazi kuwa rafiki wa mtoto wako kutamfanya ajisikie huru kushiriki matatizo yake na kupata ushauri bora kutoka kwako.

Lakini pia jitahidi kumuelimisha kuhusu mabadiliko ya mwili na hisia, kwa sababu wataalamu wa afya ya uzazi wanasema wakati wa balehe, vijana hukumbwa na mabadiliko mengi ya mwili na hisia.

Hivyo wazazi wanapaswa kuwaelimisha kuhusu mabadiliko hayo ili wasitafute majibu kutoka kwa vyanzo visivyo sahihi.

Elimu sahihi juu ya jinsia na athari za matendo kama uzinzi huwasaidia kufanya uamuzi wa busara.

Kumbuka pia dini na maadili vinaweza kuwa mwongozo mzuri kwa kijana anayeingia katika rika la balehe. Kwa hiyo kitendo cha kuwaongoza vijana katika imani ya dini na kuwafundisha misingi ya maadili, huwasaidia kutofautisha mema na mabaya.

Na kumbuka kuwa watoto hujifunza kwa kuiga. Wazazi wanapaswa kuwa mfano wa kuigwa kwa kuishi maisha mema.

Wazazi wanapodumisha heshima, uaminifu na kujiheshimu, watoto wao wana uwezekano mkubwa wa kufuata nyayo hizo.

Ila inaelezwa pia katika kipindi cha balehe ndicho pia wazazi mnakumbushwa kumfundisha mtoto namna ya kuchagua marafiki wema wa kushirikiana naye.

Kalikamkana anasema mara nyingi vijana huharibiwa pia na aina ya  ushawishi wa kufanya mambo ya hovyo katika umri wa balehe.

Hivyo mzazi anapaswa kufuatilia aina ya marafiki wa mtoto wake na kuhakikisha wana tabia nzuri.

Anasema mzazi asisite kumshauri mwanawe kuhusu jinsi ya kuchagua marafiki wazuri na athari za kuhusiana na watu wabaya, kutamsaidia kuzingatia maadili.

Akizungumzia namna ya kumuelimisha juu ya athari za matendo maovu, Kalikamkana anasema kijana anapaswa kufahamu madhara ya matendo maovu kama vile uzinzi, matumizi ya dawa ya kulevya na tabia nyingine zisizofaa.

Katika kumuelimisha, anasema mzazi anaweza kutumia mifano halisi ya maisha na kuwaelezea matokeo mabaya ya tabia hizo, kama vile mimba zisizotarajiwa, magonjwa ya zinaa na uharibifu wa ndoto za maisha yao.

Katika hili liko wazi, vijana wengi siku hizi hujikuta kwenye majaribu kwa sababu hawana ujasiri wa kukataa mambo mabaya.

Kwa hiyo mzazi anapaswa kumfundisha mtoto wake jinsi ya kusema “hapana” kwa mambo yanayoweza kumdhuru na kumfanya ajiingize katika matatizo.

Na katika hili, elimu ni silaha muhimu kwa kijana. Kama atakuwa kapata elimu bora, itawasaidia kuelewa thamani yao, kupanga malengo ya maisha na kuepuka mambo yanayoweza kuwaharibia mustakabali wao.

Kwa hiyo wazazi mnapaswa kutambua kuwa balehe ni hatua muhimu katika maisha ya vijana.

Mnapaswa kuwa mstari wa mbele  kuwaongoza kwa upendo, hekima na uvumilivu huku mkizingatia kuwapatia elimu sahihi, kuwaelekeza kwenye maadili na kushirikiana nao kwa karibu.

Kwa kufanya hivi, itawasaidia kuepuka matendo maovu na kubaki kuwa watu wenye nidhamu, heshima na maadili siku zote.

Related Posts