Lissu atoa msimamo pingamizi la kina Mnyika, Lema

Dar es Salaam. Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu amejitosa kuzungumzia sakata la barua ya malalamiko kuhusu uteuzi alioufanya wa viongozi watendaji wa juu na wajumbe wa kamati kuu akisema haina mashiko yoyote.

Barua hiyo ni ya kada wake, Lembrus Mchome, aliyoiandika kwenda kwa Katibu Mkuu wa Chadema na nakala kuituma Ofisi ya Msajili wa Vyama vya Siasa anapinga uteuzi wa viongozi hao uliofanywa na Lissu, Januari 22, 2025, akidai umekiuka katiba ya chama hicho.

Mchome, ambaye ni Mwenyekiti wa Chadema Wilaya ya Mwanga, Mkoa wa Kilimanjaro, amesema uteuzi wa vigogo hao uliidhinishwa bila akidi ya kikao cha baraza kuu kutimia.

Kwa mujibu wa Mchome, viongozi waliopatikana katika utaratibu huo ni pamoja na Katibu Mkuu, John Mnyika, Aman Golugwa (Naibu Katibu Mkuu – Bara) na Ally Ibrahim Juma (Naibu Katibu Mkuu – Zanzibar).

Katika barua hiyo, Mchome amesema wajumbe wa kamati kuu walioteuliwa na kuidhinishwa na kikao hicho ni Godbless Lema, Rose Mayemba, Salma Kasanzu, Hafidh Ally Saleh na Dk Rugemeleza Nshala, akidai uteuzi wao ni batili.

Tangu Februari 18, 2025, Mchome alipowasilisha barua hiyo yeye mwenyewe makao makuu ya Chadema, Mikocheni jijini Dar es Salaam na kuituma ofisi ya msajili wa vyama vya siasa kumekuwa na mijadala mikali ndani na nje ya chama hicho.

Mchome amedai ili akidi ya kikao kilichowaidhinisha vigogo hao kikamilike, kilipaswa kuwa na wajumbe 309, badala ya 85 waliokuwepo ambao ni sawa asilimia 20.6.

Mijadala hiyo imekwenda mbali zaidi na kukitahadhalisha chama hicho kuwa huenda kukajikuta katika migogoro wa uongozi hususan majibu ya Naibu Msajili wa Vyama vya Siasa, Sisty Nyahoza alipozungumza na Mwananchi akikiri kuipokea na kusema kilichoandikwa kina mantiki.

Nyahoza alikwenda mbali akisema kama mlalamikaji (Mchome) hataridhika na majibu atakayopewa na Chadema atawasilisha katika ofisi ya msajili kwa sababu mambo ya katiba hayaishii ndani ya chama.

 Februari 20, 2025, Naibu Katibu Mkuu wa Chadema Bara, Aman Golugwa alipoulizwa na Mwananchi kipi kinaendelea juu ya barua hiyo alisema: “Ni barua ambayo haina mambo magumu. Ni barua itakayojibiwa kwa page (kurasa) moja tu, itakuwa imejitosheleza. Itakavyofanyiwa kazi, atajibiwa mhusika aliyeandika. Utaratibu wa kiutawala, barua itakwenda kwa mhusika.

 ‘Muulizeni alikuwepo?’

 Leo Jumapili, Februari 23, 2025, Lissu amefanya mahojiano maalumu na Mwananchi nyumbani kwake, Tegeta jijini Dar es Salaam. Pamoja na mambo mengine ameulizwa swali juu ya barua hiyo na tahadhari zinazotolewa wasije kuingia kwenye mgogoro kama ulivyoshuhudiwa kwa vyama vingine.

 Lissu amesema anajua anachokifanya kada huyo ni kuwapotezea muda au hajui vizuri Katiba ya chama hicho kwani wana orodha yote ya wajumbe wa Baraza Kuu lililokutana Januari 22, 2025 katika ukumbi wa Mlimani City.

Lissu alishinda kwa kura 513, ambazo ni asilimia 51.5, huku Mbowe akipata kura 482, sawa na asilimia 48.3. Charles Odero alishindwa na kura moja.

Katika maelezo yake, Lissu amesema: “Moja ya swali ambalo mnapaswa kumuuliza (Mchome) alikuwepo? Alikuwepo siku hiyo, yeye si ni mjumbe wa Baraza kuu je, alikuwa wapi? Kama hakuwepo sasa alijuaje kuwa akidi haikutimia?”

Baraza hilo lilikutana saa chache kupita baada ya mkutano mkuu kumalizika ukumbini hapo ambapo Lissu aliibuka mshindi wa uenyekiti dhidi ya mshindani wake mkubwa Freeman Mbowe ambaye alikiongoza chama hicho kwa miaka 21.

Lissu ambaye kitaaluma ni mwanasheria amesema Mchome anaruhusiwa kupeleka hoja yake kokote, lakini chama hicho kitaenda kumjibu kwani wanachojua ni kwamba anataka kuwapotezea muda.

 “Mchome kwanza hakuwepo kwenye kikao, nataka kumuambia akidi ilitimia, kama wajumbe ni 412 akidi ya kiwango hicho ni 206, lakini walioorodhesha majina yao walikuwa 234 unasemaje walikuwa 85 unawatoa wapi, kwa hiyo atajibiwa akienda kwa msajili tutamfuata huko huko tutaenda kumuambia unasikiliza maneno ya watu ambao wanaokoteza okoteza,” amesema.

Katika kusisitiza hilo Lissu amesema: “Kwanza Mchome hakuwepo kwenye kikao na kwa sababu hakuwepo katika kikao anazungumza mambo aidha ya kuambiwa na kama anaambiwa inawezekana ameambiwa na watu ambao hawajui sawasawa au ameibua mambo yake kichwani…tumeangalia orodha yote Mchome hakuwepo.”

 Katika maelezo yake Lissu amefafanua kwa kusema kilichofanyika kwenye baraza lililofanyika Januari 22, mwaka huu kwanza wote waliokuwepo waliandika majina yao kwenye orodha ya mahudhurio katika kila kanda na wasio kuwa na kanda kwa maana ya wajumbe wa kamati kuu nao waliandika majina yao.

“Wote waliandika majina na tunaorodha yote jina la Lembrus Mchome halipo… hakuwepo na kwa sababu hakuwepo anazungumza vitu ambavyo havijui ile orodha ya wajumbe wa baraza kuu waliondikisha majina walikuwa ni wajumbe 234,” amesema.

Alipoulizwa Mchome anajenga hoja hata kama hakuwepo anatumia sehemu ya vipande vya video vinavyowaonesha baadhi ambao si wajumbe wa Baraza Kuu wakiwathibitisha viongozi hao aliowateua. Katika hilo Lissu amesema hao anaowataja hawapo kwenye orodha ya majina waliojiandikisha na wala si wajumbe wa Baraza Kuu.

Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, akisoma Gazeti la Mwananchi la leo Jumapili, Februari 23, 2025, akiwa nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam.

Lissu amesema anachokifanya Mchome ni kuwapotezea muda na hata majina aliyoyataja kwenye barua yake ikiwemo Lilian Masiyaga na Dk Nyamatari Tengecha jibu la hoja hiyo ni rahisi.

“Hao aliowataja wapo kwenye orodha hiyo ya Baraza Kuu? Kama wapo ana hoja kama hawapo anajipotosha kwa sababu ushahidi wa ushiriki wao ni orodha ya majina na tuna orodha ya waliohudhuria na nimeangalia hakuna jina la Lilian na hakuna jina la Dk Nyamatari ni hoja ya bure,” amesema.

Kuhusu masuala ya akidi amesema kikao hicho kilikuwa kinalenga uamuzi na katika barua yake Mchome hajasema kilikuwa kikao cha uchaguzi huku akidai aliisoma barua yake kwa umakini.

“Kilikuwa kikao cha uamuzi, ambapo ilitakiwa kiwe na akidi ya asilimia 75 ya wajumbe wote. Hivyo, hoja hiyo ni bure na inaonesha mtu ambaye ama hajui katiba ya chama au anapotosha makusudi. Ikiwa ameomba ushauri, basi ameishia kupotoshwa, kwa sababu ile barua imeandikwa kitaalamu na kama ameshauriwa amepotoshwa,” amesema.

Lissu amesema katiba ya chama hicho kwenye masuala yanayohusu akidi inasema kwenye uamuzi wa kisera, uchaguzi na mabadiliko ya Katiba akidi inapaswa kuzingatiwa kwa asilimia 75 ya wajumbe wote.

 “Katika kipengele cha maamuzi ya kisera Katiba yenyewe inasema kama mkutano mkuu ndiyo unaoamua sera ya chama, Katiba ya chama ndiyo unaochagua viongozi wa kuu wa chama, sasa mkutano wa uchaguzi au wa uamuzi wa kisera au mabadiliko ya Kikatiba unahitaji akidi ya asilimia 75,” amesema.

 Kuhusu mkutano wa Baraza Kuu, Lissu amesema huo ni mkutano wa kawaida wa chama wa kupitisha wajumbe wa Kamati Kuu, Katibu Mkuu, kutengeneza miongozo ya baraza, kanuni za chama huku akieleza hizo ni shughuli za baraza za kawaida.

“Sio mkutano wa uamuzi ya kisera, sio mkutano wa uchaguzi na mabadiliko ya Katiba sasa haya maneno ya Mchome, Mjumbe wa Baraza Kuu ameyatoa wapi aidha hajui Katiba au amepotoshwa na wanaomshauri au anajua anapotosha kwa kifupi ni hoja ya bure kabisa,” amesema.

Related Posts