Arusha. Serikali imetangaza mpango wa kupiga marufuku uingizaji wa vifaa vya kielektroniki kutoka nje ya nchi ili kuhamasisha uzalishaji wa ndani na kuvutia wawekezaji katika sekta ya teknolojia.
Hatua hiyo inalenga kuimarisha viwanda vya ndani na kupanua soko la vifaa vya Teknolojia ya Habari na Mawasiliano (Tehama), ikiwemo simu za mkononi, kompyuta mpakato, na vifaa vingine vya kielektroniki.
Akizungumza leo Jumapili, Februari 23, 2025, jijini Arusha, Mkurugenzi Mkuu wa Tume ya Tehama, Dk Mkundwe Mwasaga, amesema Serikali ina dhamira ya kuendeleza uchumi wa kidigitali kwa kutegemea uzalishaji wa ndani badala ya kuagiza bidhaa kutoka nje.
“Tunaendelea na jitihada za kuvutia wawekezaji wa kutosha kuanzisha viwanda vya Tehama hapa nchini. Tukifikia hatua ya kujitosheleza, tutakuwa tayari kusitisha uagizaji wa vifaa hivi kutoka nje,” amesema Dk Mwasaga alipokuwa akitembelea kiwanda cha Tanztech Electronics Limited, kilichopo Arusha.
Dk Mwasaga amesisitiza kuwa mpango huo utaimarisha uchumi wa kidigitali unaojitegemea na kupunguza utegemezi wa teknolojia za kigeni.
Pia, utatoa fursa kwa wajasiriamali wa ndani kubuni mifumo na suluhisho za kidigitali zinazokidhi mahitaji ya sekta mbalimbali kama kilimo, mifugo, na biashara.
“Kwa kutengeneza vifaa hapa nchini, itakuwa rahisi pia kuunda programu za kidigitali zinazotatua changamoto za kijamii na kiuchumi. Hii ni hatua muhimu kuelekea uchumi wa kidigitali wa kweli,” amesema.
Aidha, Dk Mwasaga amesema mpango huo utachangia kuimarisha usalama wa taifa kwa kudhibiti taarifa nyeti kwa urahisi zaidi.
Akimpongeza Mkurugenzi Mtendaji wa Tanztech Electronics Limited, Gurveer Hans, kwa juhudi za kuanzisha uzalishaji wa vifaa vya kielektroniki nchini, ameahidi ushirikiano wa Serikali katika kukabiliana na changamoto zilizopo ili kufanikisha malengo ya kukuza sekta hiyo.
Kwa upande wake, Hans amesema moja ya changamoto kubwa kwa viwanda vya ndani ni mzigo wa kodi unaotozwa mara kadhaa katika mnyororo wa uzalishaji na usambazaji wa bidhaa.
“Tunaagiza malighafi kutoka kwa washirika wetu wa China, lakini tunakabiliwa na kodi kubwa ambazo hufanya bidhaa za ndani kuwa ghali kwa watumiaji. Tunaomba Serikali kupunguza kodi hizi ili kuleta unafuu kwa Watanzania,” amesema Hans.
Naye DkGeorge Mulamula amesema mpango huo ni sehemu ya mkakati mpana wa Serikali wa kujenga uchumi wa kidigitali endelevu kwa kuwekeza katika uzalishaji wa ndani na kuwawezesha wajasiriamali wa sekta ya Tehama.
“Hatua hii itaiweka Tanzania katika nafasi bora ya ubunifu wa kiteknolojia na kuleta maendeleo katika sekta muhimu kama kilimo, afya, elimu, na biashara. Ni fursa kwa wawekezaji kushirikiana na serikali kuhakikisha mafanikio ya mpango huu,” amesema Dk Mulamula.