MASAUNI:SERIKALI INATAMBUA NA KUTHAMINI MCHANGO WA DINI ZOTE

Na Mwandishi wetu.

  Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni amesema Serikali inatambua na kuthamini mchango wa Dini zote katika kujenga maadili mema ndani ya jamii ya Watanzania hivyo kila mmoja amaowajibu wa kusaidia katika kutekeleza jukumu la malezi.

Amesema vijana wakifundishwa mila na desturi sahihi na kushika mafundisho ya dini, na wakawa na hofu ya Mwenyezi Mungu, maovu mengi yatapungua hapa nchini kwani mustakabali wa taifa unaujengwa na sisi wenyewe kwa kusaidiana kuilea jamii katika maadili mema hasa kwa vijana ambao ndio viongozi watarajiwa wa taifa.

Waziri Masauni ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Kikwajuni, Zanzibar, ameyasema hayo katika mahafali ya Chuo cha Kislamu cha MPF Zanzibar Februari 22, 2025 ambapo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho.

“Kuifundisha jamii ni jambo la kuenziwa kwa vile umma wa sasa umekumbwa na vishawishi vibaya ambavyo kwa njia moja ama nyingine huwatoa watu kwenye mwelekeo. 

Vishawishi vibaya vinaonekana dhahiri katika jamii. Sasa tunaposimama kuichunga jamii, yote kiujumla na mmomonyoko wa maadili si tu tunawasaidia wao waweze kutimiza ndoto zao bali ni kwa ustawi wa taifa letu kwa ujumla ili kufikia malengo tuliojiwekea. 

“Kipekee nitumie nafasi hii kuwashukuru viongozi wetu wakuu, Mhe. Dkt. Samia Suluhu Hassan, Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania na Mhe. Dkt. Hussein Ali Mwinyi, Rais wa Zanzibar na Mwenyekiti wa Baraza la Mapinduzi kwa miongozo na maelekezo mbalimbali wanayotupatia ambayo yameendelea kuleta mafanikio ya maisha bora kwetu Watanzania. 

“Kuhusu madarasa ya Sayansi ya Malezi ya Nafsi, napenda kumuambia Amir na Kiongozi Mkuu wa MPF karibuni Madina nami ni miongoni mwa Annsar. Hivyo basi nipo tayari kwa ajili ya kufanya kazi kwa karibu nawe na timu yako katika eneo hili na huku tukipata mwongozo na msaada kutoka kwa Mlezi wetu wa Zanzibar Mheshimiwa Mufti Mkuu wa Zanzibar Samahat Sheikh Saleh Omar Kaab.” amesema Waziri Masauni.

Amesema anafarijika kuona MPF kupitia Amir Mkuu na Kiongozi kwa namna wanavyotafsiri kwa vitendo maono ya Marais wetu, kwenye eneo la kuyajenga maadili ya vijana, wazee na watoto ambapo pia ni sehemu ya kujenga ufanisi wa watu wetu kwenye maisha yao mmoja mmoja na jumla kama Taifa.

 “Naomba niendelee kuwashukuru ndugu zangu wa MPF kwa kazi wanazofanya na hapa pia naomba kuweka bayana kuwa mimi ni Mshawishi wa MPF. Hakika mara ya kwanza kupata habari zenu na kuona kwa ufupi juhudi na mafanikio yake nikakubali kuwa mshawishi wao bila kusita na huku sikuwa najua kuwa juhudi zao pia zipo Zanzibar tena jimboni kwangu.”

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akizungumza katika mahafali ya Chuo cha Kislamu cha MPF Zanzibar Februari 22, 2025 ambapo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibari, Sheikh Abbu Simba na kulia kwake ni Amiri Mkuu wa Chuo cha MPF, Omar Othman Msuya.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais (Muungano na Mazingira) Mhe. Mhandisi Hamad Yusuf Masauni akimkabidhi cheti Asha Ali Hassan mhitimu katika mahafali ya Chuo cha Kislamu cha MPF Zanzibar Februari 22, 2025 ambapo alikuwa mgeni rasmi katika mahafali ya kwanza ya chuo hicho. Kushoto kwake ni Kaimu Mkurugenzi Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibari, Sheikh Abbu Simba na kulia kwake ni Amiri Mkuu wa Chuo cha MPF, Omar Othman Msuya.

Picha za pamoja katika makundi mbalimbali za matukio

Related Posts