USHINDI katika dakika 90 Jumapili hii kwenye Uwanja wa Lake Tanganyika, Kigoma baina ya Mashujaa na Yanga una maana kubwa kwa timu hizo kulingana na msimamo wa Ligi Kuu ulivyo kwa sasa.
Kushindwa kupata pointi tatu katika mechi hiyo ambayo itaanza saa 10:00 jioni kutakuwa na athari kubwa kwa timu ambayo itapoteza mchezo huo ambao ni wa nne kuzikutanisha timu hizo kwenye Ligi Kuu.
Kwa Yanga, ushindi utaihakikishia kuendelea kuongoza msimamo wa ligi ambapo itafikisha pointi 55 lakini pia itakuwa inajiweka katika mazingira yasiyo ya presha kuelekea mechi ya Kariakoo Dabi dhidi ya Simba kwani baada ya hii itacheza mechi moja dhidi ya Pamba na baada ya hapo itakabiliana na mtani wake, Machi 8 mwaka huu.
Ushindi wa Yanga pia hapana shaka utaiongezea presha Simba ambayo iko nyuma yake kwa pointi mbili hivi sasa huku Jumatatu ikitarajiwa kucheza mechi ngumu dhidi ya Azam FC kwenye Uwanja wa KMC Complex, Mwenge Dar es Salaam.
Kinyume na hapo kama itatoka sare au kupoteza, Yanga itajiweka yenyewe katika presha kuelekea mechi ya Kariakoo Dabi lakini pia itaongeza hali ya kujiamini kwa Simba ambayo ina faida ya kuwa na mechi moja mkononi.
Kwa Mashujaa ikipata ushindi, itafikisha pointi 26 ambazo zinaweza kuisogeza juu kwa nafasi moja hadi nafasi ya sita lakini kama itaangusha pointi, bado haitakuwa kwenye mazingira salama katika msimamo wa ligi.
Ni tofauti ya pointi tano tu ambayo inaitenganisha Mashujaa FC na timu iliyopo katika mstari wa kushuka daraja kwa sasa hivyo inalazimika kupata ushindi ili angalau iongeze pengo la pointi dhidi ya timu zilizo chini yake.
Katika Ligi Kuu Tanzania Bara, timu hizo zimekutana mara tatu ambapo Yanga imefanikiwa kuibuka na ushindi katika mechi hizo zote ambapo mechi ya kwanza ilipata ushindi wa mabao 2-1 ya pili ikashinda kwa bao 1-0 na ya tatu ikapata ushindi wa mabao 3-2.
Katika mchezo huo, Yanga itapaswa kumchunga zaidi mshambuliaji wa Mashujaa FC, David Ulomi ambaye hadi sasa amepachika mabao manne katika Ligi Kuu.
Ulomi ameonyesha uwezo mkubwa wa kufunga kwa mashuti ya mbali na ndiye kinara wa timu hiyo katika kufumania nyavu.
Safu ya ulinzi ya Mashujaa hapana shaka itakuwa na kibarua kigumu mbele ya safu ya ushambuliaji ya Yanga ambayo imekuwa moto wa kuotea mbali katika kufumania nyavu na hata kupiga pasi za mwisho.
Tishio zaidi kwa Mashujaa ni Clement Mzize ambaye anaongoza kwa kufunga mabao Ligi Kuu akiwa nayo 10 na Prince Dube ambaye hadi sasa amefumania nyavu mara tisa.
Yanga inaingia katika mechi hii ikiwa inashika nafasi ya pili kwa kuvuna idadi kubwa ya pointi ugenini ambapo katika mechi tisa ilizocheza viwanja vya ugenini, imekusanya pointi 25 ambapo imepata ushindi mara nane na kutoka sare moja.
Mashujaa yenyewe imekuwa na matokeo ya kawaida nyumbani ambapo katika mechi 10 ilizocheza Lake Tanganyika msimu huu, imeshinda nne, kutoka sare nne na kupoteza mbili.
Kocha wa Yanga, Hamdi Miloud amesema kuwa kilichowapeleka Kigoma ni ushindi na sio matokeo mengine.
“Kuhusu mchezo tunajua itakuwa ngumu na tunawajua wapinzani wetu na tunawaheshimu. Hatupo hapa kupumzika. Tupo hapa kushinda na kupata pointi tatu dhidi ya Mashujaa,” alisema Hamdi.
Kocha wa Mashujaa, Mohamed Abdallah ‘Baresi’ alisema nafasi ambayo wapo kwenye msimamo wa ligi unawalazimisha wao kuhakikisha wanapata matokeo mazuri.
“Tunacheza na timu kubwa ambayo ina wachezaji wa kuamua matokeo. Lakini na sisi tumejipanga kwa namna ya kuweza kukabiliana nao. Tunafahamu sisi bado hatupo salama kuna pointi ambazo tunahitaji kuongeza na wenzetu wanahitaji kuwa juu zaidi,” alisema Baresi.
Kabla ya mchezo wa Mashujaa na Yanga kutakuwa na mechi moja itakayochezwa mchana saa 8:00 mchana na saa 1:00 usiku kutakuwa na mchezo mwingine mmoja.
Mchezo wa kwanza wa Ligi Kuu kwa Jumapili utakuwa baina ya Singida Black Stars dhidi ya Pamba Jiji FC ambao utachezwa kwenye Uwanja wa CCM Liti, Singida.
Jumapili itamalizwa na mechi ya saa moja usiku baina ya Namungo FC na Coastal Union katika Uwanja wa Majaliwa, Ruangwa Lindi.