KOCHA wa Mbeya City, Salum Mayanga amesema hadi sasa timu hiyo kutoka jijini Mbeya iko katika uelekeo mzuri kutokana na nafasi iliyopo na kuwataka nyota wa kikosi hicho kuongeza umakini zaidi katika maeneo ya ulinzi na ushambuliaji.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mayanga alisema safu ya ushambuliaji inaonyesha matumaini ingawa changamoto anayoendelea kukabiliana nayo ni kutengeneza balansi nzuri eneo la ulinzi, kutokana na kutoridhishwa nalo kwa kiasi kikubwa.
“Ukiangalia safu ya ushambuliaji katika timu zote nne za juu utaona tunashika nafasi ya pili kwa kufunga mabao mengi ila shida ipo eneo la ulinzi kwa sababu tumeruhusu zaidi ya wapinzani wetu wote, tunapaswa kubadilisha hali hii kwa haraka.”
Mayanga aliyejiunga na timu hiyo baada ya kuachana na Mtibwa Sugar Agosti 5, 2023, alisema kasi ya washindani wao inampa nafasi nzuri ya wao pia kuendelea kupambana katika kila mchezo, huku akieleza safari ya Ligi Kuu hakuna mwenye uhakika.
Timu hiyo kabla ya mchezo wa jana ugenini dhidi ya TMA ya jijini Arusha, imecheza michezo 19 na imeshinda 11, sare sita na kupoteza miwili, ikiwa nafasi ya nne na pointi 39, nyuma ya vinara Mtibwa Sugar inayoongoza na pointi zake 48.