Dodoma. Joto la uchaguzi limeanza kupamba moto, huku baadhi ya wabunge 19 waliofukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakionyesha mwelekeo wa wapi watakwenda katika uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025.
Wabunge hao 19, akiwemo Halima Mdee, walivuliwa uanachama wa Chadema Novemba 27, 2020, wakituhumiwa kwa usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni jijini Dodoma kuapishwa.
Mdee na wenzake walikata rufaa Baraza Kuu la Chadema dhidi ya uamuzi huo wa Kamati Kuu. Baraza Kuu lililokutana Mei 11, 2022 ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam lilitupilia mbali rufaa yao.
Baada ya uamuzi wa Baraza Kuu, waliamua kwenda mahakamani ambako walikuwa na ombi la kufungua shauri Mahakama Kuu. Kesi ilichukua hatua mbalimbali na ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu lililobariki kuvuliwa uanachama Mdee na wenzake.
Mbali na Mdee, aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko, pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.
Katika orodha hiyo, wamo pia Hawa Subira Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi, Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, na Katibu Mkuu wa Bawacha-Bara, Jesca Kishoa.
Pia, aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo.
Wengine waliofukuzwa Chadema ni Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.
Miongoni mwa wabunge hao 19, wamekuwa wakitoka hadharani kuonyesha kuunga mkono kazi zinazofanywa chini ya utekelezaji wa Ilani ya Uchaguzi ya Chama cha Mapinduzi (CCM) ndani na nje ya Bunge.
Katika mkutano wa 18 uliomalizika Februari 14, 2025, Mbunge Ester Bulaya alisimama na kupongeza uchaguzi wa Chadema na mkakati wao, lakini baadhi ya waliopata nafasi ya kuchangia hawakusema chochote kuhusu chama hicho.
Chadema ilifanya mkutano mkuu wa uchaguzi Januari 21 na kumalizika Januari 22, 2025, katika ukumbi wa mikutano ya Mlimani City jijini Dar es Salaam.
Katika uchaguzi huo, Freeman Mbowe aliyekiongoza chama hicho kwa miaka 21 alishindwa na Makamu wake-Bara, Tundu Lissu aliyepata kura 513 sawa na asilimia 51.5, huku Mbowe akipata kura 482 sawa na asilimia 48.3. Charles Odero alipata kura moja kati ya kura 999 zilizopigwa na kura tatu kuharibika.
Februari 13, 2025, Bulaya aliuzungumzia uchaguzi huo wa Chadema wakati wa mjadala wa taarifa ya Kamati ya Kudumu ya Bunge ya Hesabu za Serikali za Mitaa (LAAC) kwa kipindi cha Februari 2024 hadi Januari 2025.
“Kwa moyo wa dhati kabisa, napenda kukipongeza Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa kuonyesha nini maana ya uchaguzi huru na haki, kumpongeza Mheshimiwa Freeman Aikael Mbowe kwa kubeba gharama za demokrasia kwa kukubali kushindwa na kukubali matokeo.
“Naomba niwaambie kuwa Tundu Lissu alikuwa Makamu Mwenyekiti, Mnadhimu wa Kambi ya Upinzani, Mwanasheria Mkuu wa chama; ana uwezo wa kukiongoza chama na kutufikisha kwenye demokrasia ya kweli. Mheshimiwa Makamu, John Heche alikuwa Mwenyekiti wa Bavicha, Mjumbe wa Kamati Kuu zaidi ya miaka 10; ana uwezo wa kuwa Makamu Mwenyekiti na kumshauri Mwenyekiti vyema na kuhakikisha tunafika kwenye demokrasia ya kweli,” alisema Bulaya.
Kwa nyakati tofauti, Mbowe na Lissu walipokuwa wakiulizwa hatma ya kina Mdee, walisema suala hilo lilishamalizika ndani ya chama hicho, na kama wanataka kurejea, wafuate utaratibu kwa kuomba upya uanachama.
Taarifa ambazo Mwananchi inazo ni kwamba, katika kundi hilo la wabunge 19, wapo ambao watatafuta majukwaa mengine ya kisiasa, kama vile kujiunga na vyama vingine kama CCM na ACT-Wazalendo. Wapo wengine wanapanga mikakati ya kurejea Chadema na wengine kujiweka kando na siasa.
Hata baadhi ya wanachama na viongozi wa Chadema wamekuwa na mitazamo tofauti juu ya kina Mdee na wenzake. Wapo wanaoona ni watu muhimu wasamehewe na kurejea kundini na wengine wakitaka wasisamehewe. Hilo limekuwa likiibua mivutano.
Katika shughuli mbalimbali za kiserikali na CCM, baadhi yao wamekuwa wakionekana na hata matamshi yao yamekuwa yakiibua mijadala. Ndani ya Bunge, wapo ambao wamekuwa wakiunga na kupongeza kazi kubwa inayofanywa na Serikali inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Mathalani, wabunge wawili wa kundi hilo, Nusrat Hanje na Jesca Kishoa, ambao wanatoka mkoa wa Singida, wametajwa kuweka wazi wakiyatamani majimbo Singida Mashariki (Hanje) huku Kishoa akitaka kutupa karata kwa mara nyingine Iramba Mashariki, ambalo linaongozwa na Waziri wa Fedha, Dk Mwigulu Nchemba.
Wiki iliyopita, Kishoa alifanya ziara mkoani Singida akiwa amevalia mavazi yenye rangi ya kijani, huku nyimbo zilizokuwa zinapigwa zikikuwa za CCM kama vile “Namletaaa Rais, Namletaaa Mwenyekiti.”
Kishoa amesema anafanya hivyo siyo kwa sababu anautaka ubunge, atatangaza baadaye. Katika ziara hiyo, alikuwa akitoa misaada mbalimbali na akasema hatoi kwa sababu ya uchaguzi au kugombea ubunge.
Akiwa Kata ya Nkalakala Jimbo la Mkalama, Kishoa alisema, “Badhi ya watu walinishauri nisitoe fedha hizi (Sh6 Milioni) kwa wananchi badala yake nizitoe kwa wajumbe, mimi nimeona nitoe moja kwa moja ziwaendelee walenga.”
Kishoa katika ziara hiyo ya Februari 16,2025 alikuwa ameongoza na viongozi wa matawi na Kata wa CCM, mbali na kukabidhi fedha, alitoa mitungi ya gesi kwa akina mama na taulo za kike kwa wasichana wa shule za msingi na Sekondari huku akisifia kazi nzuri za maendeleo alizosema zinafanywa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Naye Mbunge wa Viti Maalumu, Nusrat Hanje, yeye ametangaza kwa viongozi wa dini akiomba wamsaidie katika nia yake ya kugombea ubunge jimbo la Singida Mashariki.
Kwa sasa jimbo la Singida Mashariki linaongozwa na Miraj Mtaturu, ambaye alichaguliwa kumalizia kipindi cha Tundu Lissu aliyekuwa Ubelgiji akiuguza majeraha ya kupigwa risasi Septemba 2017 jijini Dodoma.
Katika hotuba aliyoitoa kwa viongozi wa dini aliowaita nyumbani kwake, Hanje hakutaja chama kipi atakachopitia katika safari ya kuusaka ubunge, lakini alisisitiza kwamba lazima atagombea na kuahidi hatawatupa.
Huku akitumia vitabu vya Mungu katika historia ya kijana Yusufu na kuvalia gauni lenye picha za Rais, Hanje pia alimsifu Rais Samia Suluhu Hassan kwamba anafanya kazi kubwa ya kuwasaidia Watanzania na akaomba aungwe mkono.
“Ndugu zangu mimi ni mtu wenu wa hapa, mimi mwananenu na familia yangu ipo hapa, nifananisheni na hadithi ya kwenye vitabu kwa yule kijana Yusufu ambaye alipitia magumu mengi mwisho akawa mfalme, sitawaangusha na wala sitafuti kujitajirisha ila tutagawana nitakachopata,” amesema Hanje alipowaita viongozi wa dini nyumbani kwake.
Mbunge wa Singida Mashariki (CCM), Mtaturu amesema taarifa za mbunge huyo kutaka kugombea jimbo hilo amezisikia, lakini akasema wananchi wa jimbo hilo hawako tayari kuongozwa na mbunge mtalii.
“Nimemsikia jana aliweka mkutano katika nyumba aliyopanga hivi karibuni ya dada mmoja ambaye alikuwa OCD wetu, sasa yupo Arusha. Yeye Hanje kwao ni Kata ya Sepuka Jimbo la Singida Magharibi, kwa hiyo atambue hatuna ukame wa wagombea hadi tukaazime,” amesema Mtaturu.
Hata hivyo, Mtaturu amesema hakuna dhambi kama amechagua jimbo hilo, anamkaribisha na wananchi watapima wenyewe nani anawafaa na ambaye amefanya kazi nzuri na kusimamia miradi iliyopelekwa na Serikali.
Katika mahojiano maalumu na Mwananchi hivi karibuni, Sophia Mwakagenda alipoulizwa hatima yake kisiasa ndani ya Chadema na kuelekea uchaguzi mkuu alisema:
“Tulishinda kesi na tupo bungeni kama wabunge wa Chadema, hivyo kwenye uchaguzi mkuu ujao nitagombea Rungwe kwa tiketi ya Chadema.”
Mwenyekiti wa CCM Mkoa wa Singida, Martha Mlata, amesema hana taarifa kuhusu wabunge hao kufanya mikutano inayohusisha sera za CCM.
Mlata pia amesema hajapokea wala kuwa na taarifa kama kuna mbunge yeyote kutoka chama cha upinzani ambaye yuko tayari kujiunga na CCM na kama yupo, kanuni zinaelekeza wanapaswa kuomba vikao vya ngazi ya chini.
“Labda kwa wenyeviti wa wilaya huko, lakini kwangu sijapokea taarifa kama kuna mbunge anataka kujiunga na CCM akitokea upinzani na wala hajatambulishwa kwangu isipokuwa wakija, basi wanapaswa kuanzia ngazi ya chini,” amesema Mlata.
Sheikh Salum Ngaa, ambaye alikuwa miongoni mwa viongozi wa dini waliohudhuria hafla hiyo nyumbani kwa Hanje, amekiri kusanyiko hilo likibeba viongozi wa dini kutoka pande zote za jimbo, lakini walikuwapo pia ndugu wa mbunge huyo.
Sheikh katika jambo hilo wakiongozwa na maneno ya utangulizi kutoka kwa babu yake Hanje.
“Mimi ni Sheikh wa Kata ya Ikungi, lakini ni Mwenyekiti wa Kamati ya Maridhiano ya wilaya hii, pale tulikuwa tunamwombea dua ili kumkinga na mabalaa, lakini tuliomba kwa ajili ya amani, tulimwombea Rais na tukaomba kwa ajili ya mvua na kweli siku hiyo ilinyesha,” amesema Ngaa.
Akizungumzia kauli ya kugombea, amesema babu ya Hanje mzaa mama yake alitangaza hadharani kuwa binti huyo wakati ukifika atagonbea kupitia Chama cha Mapinduzi na wanaamini itakuwa hivyo.
Mmoja wa mawakili ambaye aliomba asitajwe kwa madai ya kimaslahi, amesema kutangaza kugombea si dhambi na si kosa, isipokuwa masharti yanayowekwa na vyama ndiyo tatizo.
Mtaalamu huyo katika sheria ambaye amesema atagombea moja ya majimbo kanda ya ziwa, amesema baadhi ya nchi zinaruhusu mtu kutangaza nia hata kama bado mwaka mmoja, lakini hofu ya vyama kwa Tanzania ndiyo hufanya uchaguzi uwe kama siri.