Medo afutwa kazi Kagera Sugar

KLABU ya Kagera Sugar imechukua maamuzi magumu ya pili msimu huu kwa kuamua kumfuta kazi kocha mkuu wa timu, Mellis Medo.

Kagera imechukua uamuzi huo baada ya kocha huyo kuiongoza katika mechi 14 za Ligi Kuu Bara tangu alipotangazwa kuwa kocha wa timu hiyo Oktoba 17, 2024.

Medo aliyejiunga na Kagera akitokea Mtibwa Sugar ndani ya mechi 14 ameshinda  mbili pekee, akipoteza saba na kutoka sare tano.

Kocha huyo raia wa Marekani aliajiriwa na Kagera kuchukua nafasi ya Paul Nkata kutoka Uganda aliyetangulia kufukuzwa akiwa amewaongoza wakata miwa hao katika michezo saba ya kwanza akishinda mmoja pekee.

Ingawa Kagera bado haijatangaza rasmi, lakini Mwanaspoti linafahamu kuwa, Medo ameshaondolewa wakati huu timu hiyo ikiwa imesharudi nyumbani mjini Bukoba, Kagera kuanza maisha mapya bila ya kocha hiyo.

Mchezo wa mwisho ambao umehitimisha siku 129 za Medo ndani ya Kagera ni ule dhidi Ya JKT Tanzania waliopokea kipigo cha mabao 2-0 ambapo baada ya mechi hiyo kocha huyo alibakizwa jijini Dar es Salaam kwa kumalizana na mabosi wa timu hiyo wakati  kikosi hicho kikirudi Bukoba.

Ndani ya mechi hizo 14 Kagera imeruhusu mabao 22 ikifunga 13 pekee ikiendelea kusalia nafasi ya 15 katika msimamo wa Ligi wenye timu 16 ikimiliki pointi 15 baada ya kucheza mechi 2 hadi sasa.

Kagera ilipanda Ligi Kuu tangu mwaka 2005 na ni moja ya timu ambazo haijawahi kushuka daraja tangu wakati huo, japo haijawahi kutwaa ubingwa wa michuano hiyo zaidi ya Kombe la Tusker iliyolinyakua mwaka 2008.

Related Posts