‘Mifumo ya maisha inachochea kukosa maadili’

Unguja. Imeelezwa kuwa mifumo ya maisha inachangia kuporomoka kwa maadili kwa vijana na kuleta uvunjifu wa amani.

Akizungumza wakati wa utoaji wa vyeti kwa vijana waliohitimu mafunzo ya sayansi ya malezi ya nafsi na kuzindua programu ya tuishi kizamani Februari 23, 2025 Mkurugenzi Mkuu  Ofisi ya Mufti Mkuu Zanzibar, Sheikh Abbu Simba amesema kilio kikubwa cha jamii kwa sasa ni kuondokewa na maadili kwa vijana.

“Kilio cha kukosa maadili kimekuwa kikubwa sana tunaomba jumuiya zinazoshughulika na vijana zije tushirikiane pamoja kushughulikia changamoto hizi, ofisi ya mufti milango yake ipo wazi,” amesema.

Waziri wa Nchi Ofisi ya Makamu wa Rais, Muungano na Mazingira, Hamad Yusuf Masauni ambaye alikuwa mgeni rasmi amesema changamoto ya kukosa maadili inatokana na mifumo ya maisha.

“Leo ni siku muhimu sana, tunaukaribisha mwezi Mtukufu wa Ramadhani kwa staili mahususi ya kuonesha juhudi zetu za kujenga maadili mema ya vijana ambao ndio tegemeo la mustakbali wa nchi yetu,” amesema Masauni.

Amesema iwapo jamii ikiwa na maadili na umoja, hata kazi ya Serikali inakuwa  nyepesi kwa kuwa inapata fursa nzuri kushughulikia maendeleo na kukuza uchumi wa mwananchi mmoja mmoja na Taifa kwa jumla.

Masauni amesema kuwafunda wanajamii ni jambo la kuenziwa kwa vile umma wa sasa umekumbwa na vishawishi vibaya ambavyo kwa njia moja au nyingine huwatoa watu kwenye mwelekeo.

“Vishawishi vibaya vinaonekana dhahiri kwa wanajamii wote. Sasa tunaposimama kuichunga jamii yote kijumla na mmomonyoko wa maadili, si tu tunawasaidia wao waweze kutimiza ndoto zao bali ni kwa ustawi wa Taifa letu kwa jumla ili kufikia malengo tuliojiwekea,” amesema.

Naye Kiongozi Mkuu wa Taasisi ya Muslim Propelling Family (MPF), Omar Othman Msuya amesema vijana wakifundishwa mila na desturi sahihi na kushika mafundisho ya dini kisha wakawa na hofu ya Mwenyezi Mungu, maovu mengi yatapungua hapa nchini.

Baadhi ya vijana walikabidhiwa vyeti akiwamo Raya Kombo omar ambaye amesema taaluma waliopitia wanaenda kuineza kwa wengine ili iwe chachu ya kuleta mabadiliko.

Related Posts