Dar es Salaam. Chama cha ACT Wazalendo kimeamua kusukuma ajenda ya kuundwa kwa jukwaa la pamoja la vyama vya siasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba mwaka huu.
Chama hicho kinaeleza kumekuwepo na hila za kuwatia wananchi hofu, hivyo ni muhimu kwa vyama makini kushirikiana ili kupambana na changamoto hizo.
Hata hivyo, hoja hiyo imepokewa kwa mitazamo tofauti na vyama vingine.
Chama cha National League for Democracy (NLD), kimesema hakina mpango wa kushiriki muungano wa upinzani kwa sababu mwaka 2015 kilishiriki ushirikiano ulioshindwa kuheshimu makubaliano.
Katibu Mkuu wa NLD, Doyo Hassan Doyo, akizungumza na Mwananchi jana Februari 22 2025, amesisitiza kuwa hakuna sheria inayoruhusu vyama kuungana, hivyo badala ya kuzungumzia muungano, kinachohitajika ni mabadiliko ya sheria ili kuweka mfumo wa kugawana rasilimali za uchaguzi.
Mwenyekiti wa Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu, pia ameweka bayana kuwa chama chake kitashiriki uchaguzi huku kikiendelea kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi na Katiba mpya. Kauli mbiu ya chama hicho ni “Kama Mbwai na Iwe Mbwai”, ikiashiria kuwa watashiriki kwa masharti yao wenyewe.
Kwa upande wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo ( Chadema), Mwenyekiti wake Taifa, Tundu Lissu, alishaweka msimamo kama ACT Wazalenda inataka ushirikiano, iwaunge mkono kwenye kampeni yao ya ‘No Reform, No Election” (Bila Mabadiliko, Hakuna Uchaguzi). Lissu alisema vyama vinapaswa kuungana kwa misingi ya makubaliano yanayohakikisha usawa, badala ya kushiriki uchaguzi katika mazingira yasiyo huru na haki.
Akizungumza na Waandishi wa Habari kabla ya kufungua mkutano wa kamati kuu ya chama hicho Dar es Salaam, Kiongozi Mkuu wa ACT Wazalendo Dorothy Semu amesema wana jukumu la kusukuma ajenda ya kuwa na muungano wa vyama makini kuelekea uchaguzi mkuu.
“Kuna hujuma na hila zinazotumiwa kukatisha tamaa wananchi, hali hii inatufanya kuwa na jukumu kubwa la kusukuma agenda ya kuwa na jukwaa la pamoja la vyama makini, tunahitaji pia kufanya shughuli za pamoja kuimarisha umoja wetu utakaotuletea tija yenye mabadiliko”amesema.
Dorothy amesema uchaguzi unaofanyika hutawaliwa na vipigo, kamatakamata ya wagombea na utekaji wa wananchi na wa wapigakura wanaopiga uchaguzi usiohalali.
“Vyombo vya dola vimeendelea kuipendelea CCM,nimeona wananchi na wanachama wakipoteza matumaini ya mwenendo wa uchaguzi wetu, pamoja na hayo yote ni muhimu kukumbushana uchaguzi ni kama vita,vita ina majira yake, kuna wakati wa faraja,ushindi na kuna wakati wa kuvunjika ari, jemedari mzuri katika vita ni kutambua hali halisi katika vita na kuchukua hatua zaidi,jemedari hapaswi kukata tamaa,”amesema.
Kwa mujibu wa Chama cha Wananchi (CUF), kitaamua baadaye kuhusu kushirikiana na vyama vingine baada ya kutathmini faida na hasara za ushirikiano huo.
Mjadala kuhusu muungano wa vyama vya upinzani kuelekea uchaguzi mkuu unaendelea huku kila chama kikiweka wazi msimamo wake. Wakati ACT Wazalendo wanasisitiza ushirikiano, vyama vingine kama NLD, NCCR Mageuzi na Chadema vina mtazamo tofauti, jambo linaloleta changamoto katika kuunda umoja wa upinzani wa pamoja.