Rais Samia ataja sababu ya ziara yake Tanga

Mkata. Rais Samia Suluhu Hassan amesema dhamira ya ziara yake Mkoa wa Tanga ni kuona namna Sh3.1 trilioni zilizotolewa na Serikali zilivyotumika kutekeleza miradi ya sekta mbalimbali za maendeleo.

Amesema miongoni mwa miradi hiyo ni  ya miundombinu,  sekta ya afya,  elimu ambayo msingi wake ni kutoa huduma kwa wananchi na kukuza uchumi wa Taifa.

Kiasi hicho cha fedha kilichotajwa na Rais Samia ndicho kilichotolewa na Serikali kugharimia miradi ya maendeleo na kimkakati katika mkoa wa Tanga.

Rais Samia amesema hayo leo Jumapili, Februari 23, 2025 alipohutubia mkutano wa hadhara wananchi wa Wilaya ya Handeni mkoani Tanga, ikiwa ni mwanzo wa ziara yake ya siku tisa mkoani hapa.

Mkuu huyo wa nchi amesema Mkoa wa Tanga umepokea Sh3.1 trilioni kwa ajili ya utekelezaji wa miradi mbalimbali, hivyo ziara yake inalenga kujionea fedha hizo zimefanya kazi gani.

“Ziara yangu hii imelenga kuangalia Sh3.1 trilioni zimefanya kazi gani. Nitakwenda kila wilaya kukagua miradi mbalimbali ya maendeleo na natarajia kuzungumza na wananchi,” amesema Rais Samia.

Hata hivyo, amesema hiyo ni ziara yake ya kwanza akiwa Rais katika mkoa huo, tangu alipozulu mkoani humo akiwa Makamu wa Rais, Machi 2021.

“Wakati ule nilipokuja ziara kwa wiki nzima kama nilivyokuja safari hii, nilianza na wilaya hii na wakati huu nimekuja naanza na wilaya hii,” amesema akichombeza ‘hodi Tanga’ akiitikiwa na wananchi karibu.

Mwanzo wa ziara hiyo, Rais Samia ameweka jiwe la msingi la ufunguzi wa Hospitali ya Halmashauri ya Wilaya ya Handeni.

Ingawa ni hospitali ya wilaya, Rais Samia  amesema ujenzi wake umefanyika kwa hadhi ya mkoa na tayari wajawazito 900 wameshahudumiwa, kati yao 300 wamefanyiwa upasuaji.

Amemtaka Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Tawala za Mikoa na Serikali za Mitaa (Tamisemi), kutenga Sh240 bilioni kwa ajili ya ujenzi wa jengo la mifupa.

Hata hivyo, amekiri matokeo ya utekelezwaji wa kazi hiyo ni aliyekuwa Waziri wa Afya, Ummy Mwalimu, akisema alisaidia kusimamia.

Katika hotuba yake hiyo, Rais Samia amesema tamanio lake ni kuona wanufaika wa miradi inayotekelezwa ndio wanaosema kuhusu yaliyofanywa na Serikali.

Hata hivyo, ameahidi kuzishughulikia changamoto mbalimbali ikiwamo ya upungufu wa umeme na ufinyu wa barabara.

“Hilo la barabara kwa sababu Waziri yupo (Abdallah Ulega) ameshalichukua na ataona namna ya kufanyia kazi,” amesema.

Akijibu ombi la Mbunge wa Handeni Vijijini, John Salu aliyeomba Handeni Vijijini ipandishwe hadhi kuwa wilaya, Rais Samia amesema hilo litategemea kukua kwa uchumi.

Rais Samia amesema uchumi wa sasa haujafikia kukata maeneo mapya ya utawala, pengine kufikia mwaka 2026/27 hali ikiimarika hilo litafanyika.

Rais Samia ametumia jukwaa hilo kuwaeleza wananchi  kuwa mwaka huu utafanyika uchaguzi mkuu, hivyo kila mwenye sifa ya kupiga kura akajiandikishe au kurekebisha taarifa zake.

Akizungumza katika mkutano huo, Mwenyekiti wa Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Tanga, Rajabu Abdulrahman amesema kwa sababu ya upanuzi uliofanyika katika Bandari ya Tanga, safari za magari zimeongezeka.

Kuongezeka kwa safari hizo, amesema kumesababisha mfululizo wa matukio ya ajali katika Barabara ya Segera hadi Chalinze.

Mwenyekiti huyo ambaye ni mjumbe wa kamati kuu ya CCM, amemwomba Rais Samia asaidie kuhakikisha barabara hiyo inaboreshwa ili kupunguza matukio hayo.

Waziri wa Tamisemi, Mohamed Mchengerwa amesema ujenzi wa Hospitali ya Wilaya ya Handeni, umesaidia wakazi wa kata 21 wilayani humo, kupata huduma za matibabu.

Katika sekta ya elimu, amesema kiwango cha usajili wa vijana kimeongezeka mkoani Tanga na Sh43 bilioni zinatolewa kwa ajili ya elimu bila malipo kila mwezi.

Related Posts