Dar es Salaam. Rais wa Baraza la Maaskofu Katoliki Tanzania (TEC), Wolfgang Pisa amewataka Wakatoliki wamwombee Papa Francis.
Askofu Pisa ambaye pia ni Askofu wa Jimbo la Lindi, ametoa wito huo jana Jumamosi Februari 22, 2025, akisema, “Kama mnavyofahamu Baba Mtakatifu wetu Fransisko alilazwa Gemelli Polyclinic, Roma tangu Februari 14, 2025 kwa shida ya afya.
“Naomba tumkumbuke kwenye maadhimisho yetu ya Jumapili ya 7 ya mwaka kesho (leo), Februari 23, au siku zitakazofuata,” imeleza taarifa iliyolewa na Askofu Pisa na kuongeza,
“Kama Baraza la Maaskofu na Kanisa zima la Tanzania, kwa maombezi ya Maria Mkingiwa Dhambi ya Asili msimamizi wa nchi yetu, tunamwombea Baba Mtakatifu Fransisko apone haraka na kabisa.”
Vatican imesema Papa Francis ambaye amelazwa hospitalini kwa zaidi ya wiki moja sasa, bado yuko katika hali ya ‘mahututi’ huku akikumbwa na changamoto katika mfumo wa upumuaji.
“Asubuhi ya leo (jana), Papa Francis alipata changamoto ya kupumua kwa kiwango kikubwa, ambayo pia ilihitaji matumizi ya oksijeni kwa kiwango cha juu,” iliandika taarifa ya Vatican kuhusu hali ya Papa.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki duniani aligunduliwa kuugua nimonia kwenye mapafu yote na maambukizi ya njia ya upumuaji yaliyochangiwa na vimelea mchanganyiko.
Jarida la ‘Everyday Health’ limechapisha kuhusiana na maambukizi yanayomtesa kiongozi huyo kuwa huweza kusababishwa na aina tofauti za bakteria, virusi au vimelea vingine ndani ya mapafu.
Nimonia hutokea pale maambukizi ya bakteria, virusi au fangasi yanaposababisha kuvimba na kujazana kwa majimaji kwenye mapafu.
Maambukizi hayo yanaweza kuathiri pafu moja au yote mawili kwa wakati mmoja, hali hiyo kitaalamu ndiyo inaitwa ‘bilateral pneumonia’.
Kwa mujibu wa jarida hilo, limetaja visababishi vya kawaida vya nimonia ni pamoja na mafua ya msimu, Uviko-19 na ugonjwa wa pneumococcal unaosababishwa na maambukizi ya bakteria aina ya “streptococcus pneumoniae.”
“Dalili za nimonia ni pamoja na upumuaji wa shida, homa, kikohozi kinachotoa makohozi ya manjano, kijani au yenye damu. Kwa watu wazee dalili zinaweza pia kujumuisha mabadiliko ya ghafla ya hali ya akili, kukosa hamu ya kula na uchovu,” limeandika jarida hilo.
Profesa mshiriki na Mkurugenzi wa Tiba ya Upumuaji katika Chuo Kikuu cha Johns Hopkins, Dk Meredith McCormack, anasema: “Antibiotiki au dawa za kuua bacteria ndio matibabu makuu. Wakati mwingine tunatumia dawa ya kuvuta inhalers au steroids hasa kwa wagonjwa wenye historia ya pumu au magonjwa sugu ya mapafu.”
Kulingana na Chama cha Mapafu cha Marekani, watu wengi wenye nimonia wanaweza kudhibiti dalili kwa kunywa maji mengi, kupumzika vya kutosha na kutumia dawa za kushusha homa na kikohozi.
“Matibabu saidizi ni muhimu,” anasema Dk McCormack huku akiongeza; “Hii inaweza kujumuisha kuwapa wagonjwa oksijeni au hata msaada wa mashine za kupumulia kwa wale walioko kwenye hali mbaya.”
Endelea kufuatilia Mwananchi.