Sababu za Aisha Masaka kutocheza Twiga Stars

WIKIENDI iliyopita timu ya taifa ‘Twiga Stars’ ilipata ushindi wa mabao 3-1 dhidi ya Ikweta Guinea ya kufuzu kwa fainali za Mataifa ya Afrika kwa wanawake (WAFCON) mwakani nchini Morocco, lakini mshambuliaji wa timu hiyo, Aisha Masaka hakuonekana uwanjani.

Masaka anayekipiga Brighton & Hove Albion ya Uingereza hajaonekana uwanjani kwa takribani miezi miwili sasa, tangu alipopata jeraha la bega Novemba 09 mwaka jana kwenye mchezo wa Ligi Kuu England dhidi ya Arsenal.

Taarifa ya daktari wa timu hiyo ilieleza jeraha la Masaka lingemuweka nje kwa miezi mitatu akitarajiwa kurudi mwishoni mwa mwezi huu ambao alikuwa tayari kaanza mazoezi binafsi na ya uwanjani.

Hata hivyo, inaelezwa sababu ya nyota huyo kutojiunga na timu licha ya kuitwa kwenye kikosi cha Stars chini ya Kocha Bakari Shime ni pamoja na kuwa chini ya uangalizi wa klabu yake na bado hajapona vizuri.

Mmoja wa watu wa karibu wa Masaka aliliambia Mwanaspoti; “Aliitwa wakati ambao tayari kaumia hivyo hata Kocha wa Stars alikuwa anafahamu, madaktari wa Brighton walieleza kuna vitu bado hajapona kwa hiyo ikaamuliwa asiondoke kwanza na kama mambo yatakwenda sawa anaweza akaunganisha Guinea ingawa pia anaweza asicheze,” alisema.

“Walikubaliana na kuna mawili huenda ajiunge na timu kwenye mchezo wa pili au asalia England, pia eneo hilo lina machaguo mengi, kocha ameona hakuna haja ya kumtumia ilihali hajapona vizuri.”

Katika kikosi cha Stars kuna washambuliaji kama Clara Luvanga (Al Nassr), Opah Clement (Juarez), Stumai Abdallah (JKT Queens), Aisha Mnunka (Simba) na Asha Ramadhan (Yanga Princess).

Related Posts