Dar es Salaam. Tarehe 24 Februari 2025: Serikali imeipongeza Benki ya CRDB kwa kudhamini Mashindano ya 33 ya Kimataifa ya Kuhifadhi Quran yaliyofanyika Uwanja wa Benjamini Mkapa jijini Dar es Salaam.
Pongezi hizo zimeetolewa na Waziri Mkuu, Mheshimiwa Kassim Majaliwa aliyemwakilishwa Rais Samia Suluhu Hassan ambaye ameanza ziara ya kikazi mkoani Tanga. Hata hivyo, Rais Samia alipita uwanjani hapo na kutoa baraka zake kwa washiriki.
Mashindano hayo yanayohusisha vipengele viwili kikiwamo cha watoto wenye umri chini ya miaka 13 na vijana wenye zaidi ya miaka 13, huwakutanisha washiriki kutoka maeneo tofauti duniani jambo ambalo Waziri Mkuu Majaliwa amesema linasaidia kuitangaza Tanzania.
“Mashindano haya yanahamasisha usomaji wa Quran Takufu, yanatoa fursa ya kujenga maadili mema, umoja, upendo na mshikamano pamoja na kuitangaza Tanzania kimataifa. Kupitia mashindano haya tunaimarisha diplomasia na biashara ikiwamo sekta ya utalii,” amesema Mheshimiwa Waziri Mkuu Majaliwa na kuongeza:
“Nawapongeza Benki ya CRDB kupitia dirisha lenu la Al Barakah kwani mmetoa mchango mkubwa wa kufanikisha mashindano haya. Nawapongeza sana kwani ninyi pamoja na makampuni mengine mmeiwezesha shughuli hii kubwa ya kuwalea watoto katika misingi ya dini.”
Mheshimiwa Majaliwa amesema mashindano haya yanayowakutanisha Waislamu kutoka kila pembe ya dunia kuja kukumbushana umuhimu wa kusoma na kuitunza Quran Tukufu yanaikumbusha jamii kujenga utamaduni wa kukisoma kitabu hicho na vijana wanaoshiriki ni baraka kubwa mbele za Mwenyezi Mungu.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela amesema wakati wote taasisi hii kubwa ya fedha nchini inajielekeza katika kukidhi mahitaji na matarajio ya wateja wake ndio maana huwa inajitahidi kubuni bidhaa zinazoendana na mahitaji ya soko.
Amesema dini ni nyenzo muhimu ya kujenga jamii yenye maadili, kuhamasisha amani na utulivu katika nchi yetu jambo linalowezesha sekta binafsi kufanya biashara na kutekeleza mipango yake katika kila uwekezaji.
“Tunatambua kuwapo kwa wateja wetu wanaohitaji huduma za benki zinazoendana na matakwa ya dini zao hivyo tulianzisha dirisha la Al Barakah ambalo lina huduma zinazofuata misingi ya sharia ambayo nguzo muhimu katika Uislamu. Dirisha hili ni muhimu kwa Waislamu wanaofanya biashara au uwekezaji mwingine, wanaotaka kwenda hija au umrah na malengo mengine tofauti,” amesema Nsekela.
Washindi sita wametangazwa katika kilele cha mashindano hayo. Katika kundi la wakubwa, Mohamed Amin Hassan kutoka nchini Marekani aliibuka kidedea akifuatiwa na Islaam Ali Shalouf kutoka Libya pamoja na Malak Abdulaziz Al-Rabee wa Saudi Arabia.
Kwa watoto wenye umri chini ya miaka 13, Zayd El Bakkali (13) wa Morocco aliongoza akifuatiwa na Yusuf Yasin (11) wa Uganda na Mohamed Yacine (8) wa Algeria.
Ukiacha washindi hao, waumini waliojitokeza uwanjani hapo nao walizawadiwa akiwamo mmoja aliyeondoka na gari, wanne waliopata ufadhili wa kwenda hija wakilipiwa kila kitu ikiwamo safari itakayogharimu kiasi cha shilingi milioni 35, bajaji tatu, pikipiki 10 na simu 20 za kisasa.
Mwenyekiti wa Jumuiya ya Kuhifadhi Quran Tanzania, Sheikh Othman Ali Kaporo amesema kaulimbiu ya mwaka huu inasema ‘Quran ni amani’ ikiujulisha ulimwengu kwamba Quran inapinga ugaidi na mambo yote maovu katika jamii.