Na Mwandishi Wetu,Mbeya
SERIKALI imewataka waratibu wa Mfuko wa Maendeleo ya Jamii nchini (TASAF) kuandaa kanzi data za wanafunzi wanaohitimu elimu ya juu ambao wanaonufaika na mfuko huo kupitia program hiyo ili kujua maendelo yao na kuwakwamua kiuchumi.
Pia imewataka kuandaa orodha ya wanafunzi wanaohitimu elimu ya msingi kupitia mpango huo kuiwasilisha ofisi ya Waziri Mkuu ili kupelekwa katika Vyuo vya ufundi (VETA) ikieleza kuwa mkakati wa Serikali ni kubadili maisha ya wananchi wa kipato cha chini.
Akizungumza wakati wa ziara ya kukagua miradi inayotekelezwa kupitia program ya TASAF jijini hapa, Naibu Waziri Ofisi ya Rais, Menejimenti ya Utumishi na Utawala bora, Deus Sangu amesema mkakati wa serikali ni kuona wanufaika wa Tasaf wanabadili maisha yao.
Amesema ameridhishwa na utekelezaji wa TASAF katika miradi mbalimbali ikiwamo miundombinu ya barabara na maji katika Kata za Iziwa na Tembela akieleza kuwa serikali itaendelea kuboresha maisha wananchi kwa kuwasogezea maendeleo.
“Andaeni kanzi data za wanufaika wa program hii elimu ya juu tujue maendeleo yao, lakini watambue na kuwatambulisha wale wa elimu ya msingi, leteni orodha yao Ofisi ya Waziri Mkuu waweze kupelekwa Vyuo vya Ufundi Stadi (VETA), tusiwaache hawa bila msimamo”
“Lakini hawa wanaoonekana kunufaika tayari kupitia mpango wa Tasaf, wasiachwe wafuatiliwe na ikiwezekana wapewe mikopo ya asilimia 10 inayotolewa na Halmashauri, lengo ni kuona wanaondoka katika maisha ya chini,” amesema Sangu.
Akieleza zaidi amesema wakati wa kuanzisha mpango huo kwa kushirikiana na Bodi ya mikopo ya elimu ya juu walianza na idadi ndogo ya 623, lakini hadi mwaka huu walifikia wanufaika 11,654.
Kuhusu barabara zinazojengwa kwa nguvu ya wananchi kupitia program ya TASAF amesema watawashirikisha Wakala wa Barabara za Mjini na Vijijini(TARURA) kwa ajili ya kuziendeleza ili kuwarahishia wananchi katika kutekeleza shughuli za kiuchumi.
“Nimeona miundombinu ya maji na barabara, nipongeze waratibu wa TASAF na Serikali ya Mkoa wa Mbeya.Niwahakikishie Serikali itaendelea kuboresha mpango huu, Rais DK. Samia Suluhu Hassan amedhamiria kuleta mabadiliko katika nyanja zote” amesema Naibu Waziri Sangu,
Kwa upande wake mmoja wa wanufaika wa TASAF, Msafiri Msafiri amesema kabla ya kuingizwa katika mpango huo, familia yake haikuwa na uhakika wa maisha ikiwamo chakula na elimu akieleza kuwa kwa sasa amebadili hali ya maisha na kujiinua kiuchumi amesema baada kuwa katika mpango huo kwa sasa maisha yanakwenda vizuri.
“Chakula ilikuwa ni mlo mmoja na muda mwingine niliwaza tunakula nini, lakini kwa sasa ninayo miradi ya kilimo, ufugaji na watoto wanaenda shule, nimeshirikishwa maeneo mengi ikiwamo mafunzo na elimu ya uchumi na fedha,” amesema Msafiri.
Naye Efrazia Simon mkazi wa Relini Kata ya Tembela amesema mradi wa maji katika mtaa huo unaenda kuwanufaisha na kuondoa kero na changamoto ya kufuata huduma hiyo umbali mrefu haswa wakati wa kiangazi.
“Kuna muda maji hukata hivyo wananchi wote wa Kata hii hadi Kata jirani ya Mwakibete hunufaika, tupongeze kuwapo mpango huu wa TASAF ambao umegusa mtu mmoja mmoja na makundi kwa ujumla” amesema Efrazia.
Mmoja wa wanafunzi wahitimu wa Chuo Kikuu Teku, Obeid Mwasaga ambaye ni mnufaika, amesema alikosa mkopo baada ya kujiunga na Chuo Kikuu Dodoma, ambapo alifikia hatua ya kufuta usajili wake kutokana na maisha kuwa magumu akiwa mwaka wa pili hadi alipowasilisha barua ya utambulisho wa TASAF.
“Nashukuru kupitia program hiyo kwa sasa nimemaliza Chuo Kikuu Teku, nilipata mkopo asilimia 100, japokuwa sijapata ajira nimefanya usahili wa ualimu tahasusi ya Baiolojia na Kemia naomba sisi wahitimu wanufaika wa mpango huu tutazamwe” amesema Mwasaga.
Kwa upande wake Kaimu Mkurugenzi wa Halmashauri ya Jiji la Mbeya, Annamary Joseph amesema maelekezo yaliyotolewa watayatekeleza kuhakikisha walengwa wote wanafikiwa kutokana na malengo ya mpango huo.
“Halmashauri ya Jiji la Mbeya itaendelea kusimamia vyema mpango huu lakini kuwapa nafasi wale wanufaika na kuwatambua na kuwatambulisha, tunaenda kutekeleza yote yaliyoelekezwa na Serikali,” amesema Annamary.