Dar es Salaam. Benki ya Absa Tanzania imesema itaendelea kuunga mkono juhudi mbalimbali zenye lengo la kuhakikisha wanawake wa Tanzania wanapiga hatua za kimaendeleo mahali pa kazi.
Hayo yamesemwa Ijumaa ya Februari 21, 2025 na Mkurugenzi Mtendaji wa benki hiyo, Obedi Laiser, jijini Dar es Salaam, wakati wa maadhimisho ya miaka kumi na mahafali ya kumi ya programu ya Mwanamke Kiongozi, unaoratibiwa na Chama cha Waajiri Tanzania (ATE).
“Sisi Absa tuna kitu tunaita ahadi yetu ya chapa inayosema ‘Stori yako ina thamani’, kwa kuendana na ahadi yetu hii tunaamini kwamba stori za wanawake wa Tanzania zina thamani na ndio maana tuliamua kuungana na ATE kusapoti jambo ili kama wadhamini, lakini pia tumekua wadau wa karibu na ATE kwa miaka kumi tumeweza kuweka wahitimu wengi, leo hii tukiwa na wahitimu kama wanne.
“Sababu kubwa inayotufanya tuendelee kuunga mkono juhudi hizi ni kwamba kwenye miaka hivi karibuni tumekuwa na mafanikio makubwa katika utendaji, wale ambao mnafuatilia nadhani mtakuwa mashahidi na sababu kubwa ya kwanini tumefanikiwa kwa kiasi kikubwa ni kwa sababu tumekuwa na viongozi wanawake kwenye timu ya uongozi,” amesema.
Akieleza kwa mfano amesema benki hiyo ina idara mbalimbali kama vile idara nne za biashara, kati ya hizo, tatu zinaongozwa na wakurugenzi wanawake, wamepata promosheni hivi karibuni kuingia katika ngazi ya ukurugenzi.
Mmoja wa wahitimu wa programu hiyo, kutoka Benki ya Absa, Ikunda Kishimbo, ambayo tokea ianzishwe jumla ya washiriki 462 kutoka sekta binafsi na umma wamehitimu, amesema programu hiyo imewajengea washiriki kujiamini na kuwapa uwezo wa kiutendaji katika maeneo yao ya kazi.
Mafunzo yanayotolewa kupitia Programu ya Mwanamke Kiongozi pamoja na kuwa na lengo la kuongeza ujuzi wa wanawake viongozi, lakini pia yanasaidia kuongeza msukumo wa suala la usawa wa kijinsia katika mahali pa kazi.
Katika mahafali hayo, Rais Samia Suluhu Hassan alikuwa mgeni rasmi ambapo kwenye hotuba yake aliwataka wanawake wanaopata elimu au nafasi za uongozi kuhakikisha hawazitumii kuvuruga familia, badala yake wazisimamie vyema ili jamii iendelee kuwa na imani kwa mtoto wa kike.
Amesema endapo wanawake waliofanikiwa kupata elimu wataitumia vibaya pamoja na nafasi zao za uongozi watatia doa jitihada za kumkwamua mtoto wa kike na kuongeza imani potofu dhidi ya ajenda ya usawa wa kijinsia.
“Nendeni mkawe chachu ya maendeleo katika jamii, elimu na stadi za uongozi mnazopata zikainufaishe jamii, familia na Taifa kwa jumla. Haitegemewi kuwa usomi au nafasi ya uongozi unayoipata mwanamke iwe sababu ya kuvuruga familia au kuharibu watoto wako.
“Kwa hiyo ninyi mliobahatika kupata fursa ya elimu au kuwa viongozi wa maeneo mbalimbali mna dhima kubwa kuhakikisha jamii inaendelea kuwa na imani na amani katika maeneo tunayoishi, lakini pia imani katika elimu ya mtoto wa kike,” alisema.
Mkuu huyo wa nchi alisisitiza elimu na nafasi za uongozi wanazopata wanawake zisiwafanye wakasahau wajibu wao wa kijamii wa malezi na makuzi ya watoto, akieleza endapo wajibu huo utasahauliwa kutakuwa na athari kubwa.