Sungusungu wadaiwa kumvunja mwanakijiji mguu kwa kipigo

Kahama. Jeshi la Polisi mkoani Shinyanga linawashikilia sungusungu wawili kwa tuhuma za kumpiga hadi kumvunja mguu mkazi wa Kijiji cha Mbika Wilayani Kahama, John Julius (34) kwa madai ya kuiba mlango wa mwajiri wake.

Akizungumza na Mwananchi leo Jumapili Februari 23, 2024 kamanda wa polisi mkoani humo, Janeth Magomi amewataja wanaoshikiliwa ni Bundala Dalali na Issack Kulwa ambao ni walinzi wa jadi, akieleza upelelezi wa tukio hilo bado unaendelea na utakapokamilika watafikishwa mahakamani.

“Niwaombe wananchi kuacha kujichukulia sheria mkononi na kama mtu amekamatwa kwa tuhuma ya wizi ni bora akafikishwa polisi,” amesema Magomi.

Shuhuda wa tukio hilo, Magema Kafuku amesema John alishambuliwa na sungusungu hao baada ya kutuhumiwa kuiba mlango wa mwajiri wake aliyefahamika kwa jina la Mwajuma Haruna kwa kupigwa fimbo sehemu mbalimbali za mwili wake.

Akisimulia jinsi alivyoshambuliwa akiwa amelazwa Kituo cha Afya Ushetu, Julius amesema alipigwa na Sungusungu baada ya kuchukua mlango wa mwajiri wake kwa makubaliano aliposhindwa kumlipa Sh20,000 kama ujira wake baada ya kumlimia shamba. “Tulikubaliana nichukue mlango akipata hela atakuja kuukomboa, lakini nilipouchukua alipiga kelele za mwizi ndipo Sungusungu wakaja wakaniadhibu kwa kunipiga sana kama mwizi na mafimbo,”amesema Julius.

Mwenyekiti wa Kijiji cha Mbika, Benedicto Mlangani amesema alipokea taarifa za Julius kupigwa Febuari 15, mwaka huu akiwa hoi hajitambui ndipo akaelekeza apelekwe Kituo cha Afya Ushetu ili kunusuru uhai wake.

“Tumebaini John alipigwa kimakosa walikuwa wanadaiana fedha na mwajiri wake ambaye kwa sasa tunamshikilia ili agharamie matibabu yake, lakini walipaswa kumfikisha ofisini kwangu na sio kumuadhibu,” amesema Mlangani.

Naye Mganga Mfawidhi wa Kituo cha Afya Ushetu, Dk William Msigale amekiri kumpokea Julius  kituoni hapo akiwa na majeraha sehemu mbalimbali za mwili wake.

Amesema  amepatiwa matibabu lakini   wanampa rufaa kwenda Hospitali ya Halmashauri ya Ushetu kupiga X-Ray kutokana na mguu wake kuonekana umevunjika.

Related Posts