Arusha. Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania (TPHPA) imepandisha ada za vyeti vya afya ya mazao kwa zaidi ya asilimia 460, jambo linaloleta changamoto kubwa kwa sekta ya usafirishaji wa mazao ya kilimo nchini.
Muundo wa ada uliorekebishwa, ambao umesababisha ongezeko la zaidi ya mara nne kwa baadhi ya makundi ya shehena, umeibua malalamiko makubwa na mjadala miongoni mwa wasafarishaji na wadau wa sekta hiyo.
Kwa mfumo huu mpya wa ada, gharama zinazohusiana na kupata cheti cha afya ya mazao na ukaguzi zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Awali, gharama ya ithibati shehena ya kontena ilijumuisha ada ya chei cha afya ya mazao ya Sh 40,500 na ada ya ukaguzi ya Sh 17,847, jumla ya Sh 58,347.
Sasa, wauzaji wanakutana na ongezeko kubwa linalofikia hadi Sh 331,320.
Jumla hii mpya inajumuisha ada ya ukaguzi ya Sh 201,320 kwa cheti cha usafirishaji wa shehena zaidi ya kilogramu 1000, pamoja na ada ya Sh 130,000 kwa cheti cha afya ya mazao kwa ajili ya kusafirishwa kwenye masoko ya nje.
“Awali, kwa shehena inayohitaji Sh 49,000, kwa mfano shehena 29, jumla ya gharama ilikuwa karibu Sh 1.4 milioni. Kwa viwango vipya, inagharimu Sh 7.3 milioni. Hiyo ni ongezeko la Sh 5.9 milioni—kiasi kikubwa cha ongezeko,” alionyesha muuzaji wa mazao ya kilimo aliyezungumza kwa kutotaja jina lake.
Ongezeko la ada linahusiana na shehena zisizo za kontena, hasa zinazosafirishwa kupitia viwanja vya ndege, ambapo gharama pia zimeongezeka kwa kiasi kikubwa.
Kabla ya mabadiliko, ada ya ukaguzi wa mazao na cheti cha afya ya mimea ilikuwa Sh 45,900.
Kwa muundo mpya, wauzaji wanakutana na ada mpya ya jumla ya Sh 155,000 kwa cheti cha afya ya mazao yanayosafirishwa kwenye shehena zinazozidi kilogram 1000.
Wauzaji wamepaza sauti ya malalamiko, wakionya kuwa ongezeko hili la ada linatishia ushindani wa bidhaa za kilimo za Tanzania katika soko la dunia.
Wengi wameonyesha wasiwasi kuhusu ongezeko la gharama, ambazo zinatishia ukuaji wa biashara ndogo na za kati.
“Ongezeko hili ni kubwa na linatishia uwepo wa biashara ndogo na za kati katika sekta yetu kwani ada hizi zinaathiri moja kwa moja bei za bidhaa zetu na uwezo wetu wa kushindana duniani,” aliongeza.
Athari ya haraka ya mabadiliko haya ni changamoto kubwa ya kifedha kwa wauzaji, ambao wanatahadharisha kuwa Tanzania inaweza kupoteza sehemu ya soko katika maeneo muhimu ya usafirishaji ikiwa suala hili halitatuliwi.
Ulinganifu wa gharama za ukaguzi na vyeti vya afya ya mazao wa kanda ya Afrika ya Mashariki unaonyesha Tanzania kuwa na gharama kubwa zaidi kuliko nchi wanachama wa jumuiya hiyo.
Nchini Rwanda, kupata cheti cha afya ya mazao kinagharimu RwF 200 pekee, sawa na Shilingi ya Kitanzania 364.1, kinyume na ada kubwa ya Tanzania.
Nchini Uganda, ada ni 5,000 Shilingi za Uganda, ambazo ni sawa na shilingi za kitanzania 3,348, ambayo ni chini kabisa kuliko hata gharama za zamani za Tanzania.
Kwa upande mwingine, wauzaji wa Kenya wanatozwa ShK600 (KES) sawa na Sh11,880 kwa kila cheti cha afya ya mazao, kiasi kinachotoa faida ya ushindani kwa bidhaa za kilimo za Kenya katika masoko ya kimataifa kuliko zile za Tanzania.
Mkurugenzi Mkuu wa TPHPA, Profesa Joseph Ndunguru akizungumza na Mwananchi kwa simu leo Jumapili Februari 23, 2025 jijini Arusha ameelezea ongezeko la ada za vyeti vya afya ya mazao na ukaguzi kama hatua ya kimkakati ya kuongeza fedha zinazohitajika kuboresha huduma kwa wauzaji.
Profesa Ndunguru amesema, “Kuongeza ada ni muhimu ili kuboresha huduma zetu ziweze kuwasaidia wauzaji kufikia viwango vya masoko ya kanda na kimataifa.”
Amesema muundo wa ada, ambao ulirekebishwa kwa mara ya mwisho mwaka 1996, sasa hauwezi kutosha kuendesha shughuli za TPHPA katika mazingira ya kilimo yanayozidi kuwa ya kibiashara.
Uanzishwaji wa TPHPA ulikuwa na lengo la kufuata viwango vya Mkataba wa Kimataifa wa Ulinzi wa Mimea (IPPC) kwa hatua za usafi na afya ya mimea.
Zaidi ya hayo, Profesa Ndunguru amesema mamlaka imepata mashine tano za kisasa za High-Performance Liquid Chromatography (HPLC).
Mabadiliko haya katika uwezo wa maabara yanahakikisha ufanisi bora na uchambuzi kamili wa kemikali.
Kwa hiyo, TPHPA sasa inaweza kupima sampuli za ubora za mazao 2,000 kwa wiki, kupunguza muda na gharama kwa wauzaji ambao awali walilazimika kutuma sampuli nje ya nchi kwa ajili ya kupimwa.
“Kutekeleza maboresho haya ni muhimu kwetu kutoa vyeti vya phytosanitary sahihi, ili bidhaa zetu ziweze kufikia viwango vya masoko ya kimataifa na kudumisha sifa ya nchi,” amesema Profesa Ndunguru.