Walipekua simu za wenza wao yakawakuta haya

Mimi sasa hivi sigusi simu… ya mwanamume? Nilishakoma, yaani hizo ndizo zilinibebesha sana mabegi. Simu? Hapana sigusi kabisa.”

Huyo ni Rachel Fanuel, mkazi wa Ilemela jijini Mwanza, akielezea jinsi ndoa yake ilivyonusurika kuvunjika zaidi ya mara 10, chanzo kikiwa ni kukagua simu ya mume wake kila akiiacha sehemu ya wazi.

Rachel (40), mama wa watoto watatu, anasema kilichookoa ndoa yake ni busara za wazazi na familia yake ambao kila mara alipokuwa akirudi nyumbani kwao baada ya kugombana na mume wake kutokana na kufumania mawasiliano ya michepuko yake, walimrudisha kwake kutatua ugomvi huo.

“Kuna siku nikachukua namba ya dada niliyoiona katika simu ya mume wangu, alinichamba wakati mume ni wa kwangu, lakini mwishowe aliachwa baada ya mume wangu kujua amenitukana,” anasema.

Anasema tabia yake ya kufuatilia mawasiliano ya mume wake siyo tu ilimfanya aishi maisha magumu kwa kuumia moyoni, kutokuwa na raha lakini pia ilimfanya kuona kama anaonewa hadi na familia yake ambayo mara kwa mara ilimrudisha kuendelea kuishi na baba watoto wake.

“Yaani hadi leo simu ikiita namuita baba…simu inaita akiniuliza nani anapiga namjibu sijui namba inaishia ngapi, yaani nikimpa natoka na ndani nisisikilize tu maongezi, maana shetani anakuwa kama kafanya hivi (anaonesha ishara ya kusikiliza mazungumzo)…unamsikia anakwambia sikiliza maongezi sikiliza maongezi,” anasema na kuongeza:

“Halafu simu za hivyo unazigundua mapema tu unamkamata, lakini sasa hivi nikiona namba ngeni nampa halafu mimi huyo naondoka, kama alikuwa chumbani naenda sebuleni.”

Anasema kutokana na kufumania mawasiliano ya kimapenzi kwenye simu ya mume wake ambayo mengine alikuwa akiwasiliana na kutoka kimapenzi na majirani zake, muda mwingine alikuwa anapigwa kwa kuwa kila akifumania alikuwa akimsimanga kwa maneno makali.

“Kuna makosa kiasi kwamba ukimwambia mtu anasema dada una roho ngumu…ukiachana na familia yangu, kingine kilichonisaidia kwenye ndoa baada ya familia kunirudisha kila nikirudi nyumbani, ni kutojali matendo yake,” anaeleza.

Anasema kutokana na magumu aliyopitia kutokana na kushika simu ya mumewe, hivi sasa hakuna tukio analoweza kufanyiwa na mume wake likambebesha mabegi, kwa kuwa anaamini hakuna mwanamume ambaye hachepuki na kufuatilia simu ni kujiumiza tu na mwishowe kusambaratisha familia.

“Yaani asingekuwaga mama yangu ningekuwa nimeshaachika. Nahisi ningekuwa na mwanamume mwingine, ilikuwa nikifika nyumbani Kahama (Mkoa wa Shinyanga) saa 12 naambiwa lala ila nikifika saa nane mchana narudishwa maana usafiri wa kurudi Mwanza bado upo,” anasema.

Anasema wakati huo alijikuta akiomba katika madhehebu mbalimbali ili mume wake aache tabia ya kuwa na wanawake, akiamini huenda kuna nguvu za kishirikina lakini ilishindikana na kudai kuwa tatizo hilo liliisha baada ya kuanza kujitambua.

“Yaani niliomba dini zote unazozijua kupitia runinga, maji ya Mwamposa niliyanywa kama nini nilihisi labda nimerogwa sijielewi. Nilivyokuja kujitambua, na kujua nafasi yangu ndani ya nyumba mambo yalibadilika hadi sasa naishi kwa amani. 

Mwanamume anawahi kurudi nampa huduma zote mke anazotakiwa kumpa mume wake. Nadhani hata yeye akaona ni ujinga kuendelea kuwa na wanawake wengine nje,” anasema na kuongeza:

“Narudia kusema, hakuna mwanamume ambaye hachepuki, muhimu kama wanawake tujue upungufu wetu unaotufanya wachepuke kisha tujirekebishe, kufuatilia mawasiliano yao hatujengi, tunabomoa.”
 

Kwa upande wake, Jumanne Miraji anaeleza alivyokaribia kutoa uhai wa mtu, kisa kukagua simu ya mkewe.

“Nilikuwa na tabia sana ya kufungua simu, na kwa nini niifungue? Simu ya mke wangu ni ya kwangu na nina haki zote na mamlaka yote…nina haki ya kujua anawasiliana na nani,” anasimulia.

Jumanne, baba wa watoto watatu anasema kushika simu ya mke wake ilikuwa ni kujipoza, kutokana na hofu ya kuibiwa mali yake, kwani kila mara alikuta ujumbe wa salamu za watu asiowafahamu na baadhi wakimtongoza mke wake.

“Kifupi nina roho ndogo…namuuliza hii namba ya nani na wakati fulani ulikuwa wapi, basi atakachonijibu anakula mtama, anakula ngumi, anakula kichwa, tunajaza watu mambo hadharani,” anaeleza.

Anasema kushika simu ya mke wake kulimlazimisha anunue kifaa cha kumfuatilia, ndipo hapo wazo la kutaka kumuua lilimjia baada ya kuthibitisha kweli mke wake anatoka nje ya ndoa.

Anasema kifaa hicho kilimpeleka hadi alipokuwa mke wake na mwanamume mwingine, alivyowaona wakiwa wanakunywa kwenye duka la vinywaji na kufurahi, alihisi kuchanganyikiwa na kufuata panga alilonunua nyumbani kwake kwa ajili ya kuwakatakata, lakini alizuiwa na rafiki zake aliokutana nao njiani.

“Nilishanunua panga la Sh35,000 nikawaambia wataalamu wa kunoa…we noa mbele na nyuma. Panga hili lilikaa chini ya uvungu wa kitanda…kuna siku alikuwa amelala (mke wake) mi nikatamani nitenganishe kichwa na kiwiliwili, lakini basi tu naona malaika wakanisimamia nikapiga moyo konde, nikaona hapana, kama nitamuua familia yangu watadhalilika na mwishowe nitaenda jela.

“Kwa hiyo nikajitahidi kwa hilo, nikaona kumuacha siyo suluhisho wala kuua. Mwishowe suluhisho nikajitahidi kumpigapiga. Ilipofika kipindi nikakua kimawazo nikaamua sasa kudharau, maana kinachokuja nitaua au nitauawa, nikaona kujipoza ni kujiimarisha kimoyo, nikajitahidi kusali sana na kufunga…nikaamua nimuachie Mwenyezi Mungu,”,anaeleza.

Anasema kwa sasa hajui kama mke wake ameacha mawasiliano na wanaume wengine.

“Maana mimi sihusiki nazo kabisa, simu yake ni yake na yangu ni yangu, kwa sasa tumeamua kuishi maisha hayo ili kuepusha kinachoweza kutokea hapo mbele,” anasema.
 

Kukosa uaminifu chanzo ndoa kuvunjika

Kwa mujibu wa takwimu za Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (Rita), katika kipindi cha miaka mitatu kuanzia mwaka 2019 hadi 2021, kulikuwa na talaka 1,503, huku ukosefu wa uaminifu baina ya wanandoa ukitajwa kuwa miongoni mwa vichocheo vya talaka hizo.

Sababu nyingine za talaka hizo ni ukatili na kutelekeza familia.
Hata hivyo, katika hotuba ya Waziri wa Maendeleo ya Jamii, Jinsia, Wanawake na Makundi Maalumu, Dk Dorothy Gwajima kuhusu makadirio ya mapato na matumizi ya fedha kwa mwaka 2024/25, alisema wizara hiyo kupitia maofisa ustawi wa jamii, imeendelea kuratibu huduma za usuluhishi wa migogoro ya ndoa na familia ambapo hadi Aprili 2024, mashauri yaliyoshughulikiwa yalikuwa 31,380, ikilinganishwa mashauri 28,773 yaliyoshughulikiwa mwaka 2022/2023.
 

Wanachosema washauri masuala ya ndoa, wazee

Mshauri wa masuala ya uhusiano na ndoa jijini Mwanza, Swaumu Mrisho anasema kutojiamini ndiyo sababu ya wanawake wengi kukimbilia kukagua simu za wenza wao na mwishowe kuanza migogoro na ndoa kuvunjika.

“Huko kutojiamini kunasababisha wengi wanapotea na kupoteza ndoa, kimsingi ni kuwashauri tu wajiamini, lakini pia watulie kwenye ndoa zao, kwa sababu wanawake ndio kitulizo cha waume, wanaweza kuwa wengi, lakini kwa sababu ya nidhamu mmoja akawapiku wenzake,” anaeleza.

Anasema wenza wanapoingia kwenye ndoa kwa mara ya kwanza wanapaswa kujengeana imani.

Anasema wanawake wengi wanapoingia ndani ya ndoa, wanazitumia simu vibaya, ndiyo maana wanaamini katika kukagua simu za wenzao, huku wakiamini wenzao wanatumia simu katika mambo ya usaliti.

“Wanasahau kuwa katika masuala ya ndoa watu wameoana lakini wanatoka katika malezi tofauti na kuna watu alikuwa anawasiliana nao na hawezi tu kuacha kuwasiliana kwa sababu ameoa. Anaweza kuyaacha mawasiliano kulingana na wewe unavyomlea ndani na akasahau na akaacha kabisa kupokea simu za wengine.

“Lakini kutokana na kumbana, kumchunguza, vurugu, mwanamke kukosa adabu, kunamsukuma yeye mwenyewe kufikiria kwamba kumbe kule nilikoacha kuna umuhimu zaidi,” anasema Swaumu.

Anasema njia sahihi ya kuepusha migogoro ya aina hiyo ni kuacha kuchunguza simu, akidai kabla ya simu watu waliishi, walichepuka, lakini kulikuwa na nidhamu na kuikumbusha jamii kuwa, simu haina umuhimu sababu imekuwa ni kigombanishi kikubwa kwenye familia.

“Mara nyingi anayechukua simu kusearch (kukagua) yeye mwenyewe ana tabia hiyo, wanaishi kwa kutoaminiana ndani ya nyumba, lakini ukimwamini mwenzio maisha yanaendelea bila kuangalia nyuma,” anaongeza.

Mzee Sudi Simba (84) anasema tabia ya kushika simu siyo tu inaweza kuudhi, lakini pia ndio chanzo cha migogoro mingi ya ndoa kwa kizazi hiki.

“Hakuna haja ya kushika simu, maana yake unaweza ukakuta mtu kamtania mwenza wako au ikapigwa tu wewe ukapokea ukasikia aaah ‘nimekumisi’, kumbe anayesema hivyo siyo hata mpenzi wake, ni mtu tu wanataniana, ila wewe ukaamua kubeba mabegi kuvunja ndoa,” anasema.

Anasema enzi za ujana wake, wazee wao walizuia kushika barua za wenza wao kwa kuwa kipindi hicho mawasiliano kwa asilimia kubwa, yalikuwa kwa njia ya barua ili kuepusha migogoro inayoweza kutokea kwa kutoelewa au kuelewa kilichoandikwa.

Naye, Mratibu wa Elimu ya Afya Mkoa wa Mwanza, Leonard Byakato anasema tabia ya kupekua simu ya mwenza mara kwa mara, inaweza kumuathiri mkaguaji kiakili kutokana na wivu wa kimapenzi.

“Inabidi apate mtu wa kum counsel (kumshauri kitaalamu) vizuri kwamba ni vitu gani labda uache ni vitu gani ufanye, kwa kuwa athari ya tabia kama hiyo inaweza kusababisha kuachana au kudhuru mtu mwingine,” anasema.

Related Posts