Wananchi waitwa kujiandikisha daftari la kudumu la wapigakura

Unguja. Wakati awamu ya pili ya uandikishaji wa daftari la kudumu la wapigakura ikianza mikoa ya Unguja, Tume ya Uchaguzi Zanzibar (ZEC), imewataka wananchi wenye sifa kujiandikisha ili wapate uhalali wa kuwachagua viongozi wanaowataka.

Akizungumza baada ya kutembelea vituo vya uandikishaji Wilaya ya Kaskazini A Mkoa wa Kaskazini Unguja leo Februari 23, 2025 Mwenyekiti wa ZEC, Jaji George Joseph Kazi amesema matarajio ya tume, watu wote wenye sifa wajitokeze kuandikisha.

“Hatua hiyo itawawezesha kupata haki yao ya msingi ya kupigakura na kuwachagua viongozi wanaowataka katika uchaguzi mkuu unaotarajiwa kufanyika Oktoba mwaka huu,” amesema Jaji Joseph.

ZEC imeanza uandikishaji wapigakura wapya awamu ya pili upande wa Unguja na inatarajia kuwaandikisha 78, 922 Zanzibar nzima kwa mujibu sensa ya watu na makazi ya mwaka 2022.

Uandikishaji huo, kila wilaya utatumia siku tatu kwa wilaya zote saba.

Jaji Joseph amesema ZEC inafanya utaratibu wa kutembelea vituo vyote kuangalia uandikishaji huo kusikiliza changamoto na kuzitafutia ufumbuzi ili kila mwenye haki apate haki yake.

“Hali ni nzuri, kuna amani ya kutosha na watu wengi wamejitokeza kujiandikisha na hakuna changamoto kubwa isipokuwa changamoto ndogondogo.

“Hata hivyo, baadhi ya changamoto ndogondogo zilizobainika katika baadhi ya vituo ni kushindwa kusoma alama za vidole lakini zimeshughulikiwa,” amesema Jaji Joseph.

Jaji Kazi amewataka wasimamizi wa vituo inapotokea changamoto hiyo watoe taarifa  ili itatuliwe haraka, kwa kuwa kuna wataalamu wa teknolojia.

Baadhi ya mawakala wa vituo viliyotembelewa wamesema uandikishaji unaendelea vyema na hakuna changamoto kubwa zilizojitokeza isipokuwa baadhi ya wananchi vidole vyao kushindwa kusoma lakini wanashughulikiwa.

Wakala wa Chama cha ACT- Wazalendo, Shehia ya Matemwe, Aziz Khamis amesema bado wanaendelea kuandikisha japokuwa kuna wananchi vidole vimegoma lakini wameshghulikiwa.

Naye wakala wa Chama cha CCK, Abdulla Mussa amesema  Shehia ya Mbuyu Tende wananchi wamejitokeza wachache lakini wanaimani wataendela kujitokeza kadri muda unavyokwenda.

“Utaratibu ni mzuri unafika hapa unaelekezwa kisha unaandikishwa na mtu hatumii muda mrefu,” amesema Ali Akubu, mkazi wa eneo hilo.

Mkazi mwingine, Asha Makame Pili ameipongeza ZEC kwa utaratibu mzuri waliouweka akisema hakuna usumbufu wowote wanaoupata na mwananchi anapata huduma na kuondoka.

Amesema hatua hiyo itawawezesha kupata haki yao na kuchagua kiongozi sahihi ili waendelee kuharakisha huduma za kijamii.

Related Posts