Hatua ya kuvunja uhusiano wa kimapenzi au talaka kwenye ndoa huwa ngumu kwa wanaume ikilinganishwa na wanawake, watafiti wamebaini.
Watafiti kutoka Chuo Kikuu cha Humboldt, Berlin Ujerumani, wamegundua kuwa wanaume huthamini na wanajali sana kuwa kwenye uhusiano kuliko wanawake.
Utafiti huu unayeyusha dhana ambayo imekuwepo kuwa wanawake ndio huridhika sana kuwa kwenye mapenzi kuliko wanaume.
Hata hivyo, wanaume huhisi sana upweke na huathirika kabisa kisaikolojia ikilinganishwa na wanawake baada ya mapenzi kuisha kwa mujibu wa utafiti huu mpya.
Kuibuka na hoja hii, wanayasansi zaidi ya 50 kutoka Chuo Kikuu cha Humboldt, walizamia na kutathmini tofauti za kijinsia kwenye uhusiano kati ya wanaume na wanawake.
Wanaume baada ya ‘kuachwa’ huanza kumsaka mpenzi mwingine kwa sababu wanasaka faraja na manufaa waliyokuwa nayo kwenye penzi la zamani.
“Tunafahamu kuwa wanawake hupata msaada au ushauri wa kisaikolojia kutokana na mazingira ya kijamii. Hii ni kinyume kwa wanaume ambao hisia zao hutegemea sana kuwa katika uhusiano na wanawake,” utafiti huo unaeleza.
“Kwa kifupi, uhusiano thabiti huwa ni muhimu kisaikolojia kwa wanaume kuliko wanawake,” unaongeza kusema utafiti huo.
Upweke na mara nyingi kukosa manufaa ambayo yalikuwepo kabla ya kuvunjika kwa uhusiano wa kimapenzi, ndio huwaponza wanaume.
Pia ni rahisi wanawake kuwaendea mama, rafiki, baba, mtaalamu wa afya ya kiakili au mwanafamilia yeyote ili hisia zao zitulizwe baada ya kuvunjika kwa uhusiano.
Wanaume nao mara nyingi hujitenga na kuendelea na maisha yao huku wakiumia ndani kwa ndani bila kutoa hadharaani yale wanayopitia.
Ni jambo ambalo limekuwepo tangu utotoni katika jamii kuwa wanawake wapo radhi kuzungumzia matatizo yao na kusaidiana kihisia kuliko wanaume.
Utafiti huu unaongezea kwa zile za nyuma ambazo zimeweka wanaume kama nguzo katika uhusiano kuliko wanawake.
Tafiti za awali pia zimeonyesha mwanaume anapokuwa kwenye uhusiano, huimarisha afya ya akili. Hii ndiyo maana wanaume ambao wapo kwenye ndoa, imebainika huwa hawazeeki mapema ikilinganishwa na makapera.