WATAALAM WA KISHERIA PWANI WAHAMASIWA KUTOA HAKI KWA WANANCHI KUPITIA MAMA SAMIA LEGAL AID

SERIKALI imewajumuisha wataalam zaidi ya 40 wa kisheria kutoka halmashauri tisa mkoani Pwani kwa lengo la kutoa elimu ya kisheria na utatuzi wa migogoro kwa wananchi, ili kurahisisha utendaji katika utekelezaji wa kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia (Mama Samia Legal Aid), inayotarajiwa kuanza Februari 25, mwaka huu, mkoani humo.

Akifungua mafunzo hayo, Katibu Tawala wa Mkoa wa Pwani, ambaye pia ni Skauti Mkuu wa Tanzania, Rashid Mchata, alitoa wito kwa wataalam hao kuwajibika kwa kutoa haki katika utekelezaji wa zoezi hilo.

Kadhalika, aliwataka wataalam hao wanaoshughulikia masuala ya kisheria kuhakikisha hawasababishi migogoro inayoweza kuleta mivutano baina ya wananchi na serikali.

“Huduma hii ni hatua kubwa ya Serikali katika kuhakikisha wananchi, hasa wale wasio na uwezo wa kugharamia wanasheria na walioko maeneo ya mbali, wanapata msaada wa kisheria ikiwemo masuala ya ndoa, mirathi, ardhi na ukatili wa kijinsia,” anasisitiza Mchatta.

Awali, Mkurugenzi wa Msaada wa Kisheria kutoka Wizara ya Katiba na Sheria, Angela Anatory, alieleza kuwa wananchi wengi wanahitaji msaada wa kisheria kutokana na umbali na uhaba wa fedha, ndipo serikali iliona umuhimu wa kuanzisha kampeni hiyo.

Nao baadhi ya wataalam wa kisheria walioshiriki mafunzo hayo, Paschal Machango kutoka dawati la jinsia na watoto Mkuranga, alipongeza ujio wa Mama Samia Legal Aid na juhudi zinazofanywa kuhakikisha haki inapatikana kwa Watanzania.

Huduma hii, inayotolewa chini ya Wizara ya Katiba na Sheria, imeshatekelezwa katika mikoa 19, na sasa Pwani inakuwa mkoa wa 20 kunufaika.

Katika mkoa wa Pwani, kampeni itakuwa kwa siku tisa, kuanzia tarehe 25 Februari hadi 5 Machi 2025, ikilenga kuwafikia wananchi wengi kadri inavyowezekana.

 

Related Posts