Watanzania wang’ara Kilimanjaro International Marathon

WANARIADHA wa Kitanzania wamenga’ra katika mbio za Kimataifa za Kilimanjaro mwaka huu wa 2025 ambapo Hamis Misai am3ishinda nafasi ya kwanza mbio za kilomita 42.2 kwa muda wa saa 2:20:45, katika mbio zilizofanyika katika uwanja wa chuo kikuu cha ushirika Moshi (MoCU), Moshi, mkoani Kilimanjaro.

Nafasi ya pili imechukuliwa na Aloyce Simbu wa Tanzania aliekimibia kwa muda wa saa 2:21:17, mbele ya Mkenya Abraham Kipkosgei wa Kenya aliekimbia kwa muda wa saa 2:24:12.

Kwa upande wa wanawake nafasi ya kwanza imechukuliwa na Jacinta Chepkoech wa Kenya aliekimbia kwa muda wa saa 2:45:39, akifuatiwa na Agnes Musabyimana kutoka Rwanda aliekimbia kwa muda wa saa 3:00:07 na nafasi ya tatu imechukuliwa na Neema Sanka wa Tanzania aliekimbia kwa muda wa saa 3:00:49.

Kwa upande wa mbio za kilomita 21.1 za Yas Kilimanjaro marathon half-marathon, mshindi alikuwa ni Mtanzania Failuna Matanga aliekimbia kwa saa 1:17:37 na kumtangulia Irine Wawuda wa Kenya aliekimbia kwa muda wa saa 1:18:44 mbele ya Mtanzania Neema Festo aliekimbia kwa muda wa saa 1:21:38.

Akihitimisha mbio hizo ambazo zimeingia msimu wa 23 mwaka huu, Naibu Waziri Mkuu na ambaye pia ni Waziri wa Nishati Dotto Biteko ametoa rai kwa wadau wa maendeleo kushirikiana na wandaajiwa Mbio za Kilimanjaro International Marathon ili kutumia mashindano hayo kuinua sekta ya utalii nchini.

“Taarifa zinaonyesha kuwa ushiriki katika mashindano haya unaongezeka kila mwaka; kwa mfano mwaka 2024 jumla ya washiriki walioshiriki mbio hizo walikuwa 12, 800 na mwaka huu idadi hiyo imefikia zaidi ya 20,000, ni wazi kuwa yana mvuto ambao ukitumiwa vyema katika kukuza utalii sekta hiyo itakuwa kwa kasi kubwa”, amesema.

Aidha amewataka wananchi kuendelea kushiriki maozezi mara kwa mara ili kuboresha afya zao na pia kuepuka maradhi yasiyoambukiza ambayo yamekuwa ni tishio ndani ya jamii katika miaka ya hivi karibuni,

“Pia nitoe rai kwa wananchi wote kuhakikisha wanakuwa na nidhamu katika ulaji wao ili kuepuka pamoja na athari zingine, maradhi yasioambukiza”, amesema.

Aidha amewapongeza wadhamini wa mashindano hayo wakiwemo wafadhili wakuu Kilimanjaro Premium Lager na wadhamini wa mbio za kilomita 21 kampuni ya Yas Tanzania kwa kufanya mashindano hayo kuwa na mafanikio makubwa kwa kipindi chote cha miaka zaidi ya 20.

Amewataja wadhamini wengine kuwa ni pamoja na wadhamini wa mbio za kilomita 5 CRDB Bank, Simba Cement, Kilimanajro Water, TotalEnergies, TPC Sugar, Garda World Security CMC Motors, Hoteli za Salinero Kilimanjaro, Hotel za Kibo Palace na Hoteli za Keys.

Awali akimkaribisha Naibu Waziri Mkuu, Waziri wa Habari, Uatmaduni, Sanaa na Michezo Palamagamba Kabudi amesema mashindano ya Kilimanjaro Marathon yamepiga hatua kubwa katika kukuza michezo hapa nchini.

“Hatuna budi Serikali na wadau wengine wa michezo na maendeleo kwa ujumla kuunga mkono juhudi zinazofanywa na wandaaji wa mbio hizi pamoja na wadhamini wake kutokana na umuhimu wa mbio hizi katika kukuza sekta ya michezo, utalii pamoja Uchumi wa Taifa kwa ujumla”.

Kwa upande wake mkurugenzi mkazi wa kampuni ya bia TBL ambao ni wa wadhamini wakuu kupitia bia yao ya Kilimanjaro Premium Lager Michelle Kilpin ameahidi kuwa kampuni hiyo itaendele kuwa mshirika mkubwa wa mbio hizo ambazo alisema umaarufu wake unazidi kukua kila mwaka.

“Tunajivunia kuwa sehemu na mhusika mkuu wa tukio hili maarufu kitaifa na kimataifa; tunawashukuru wadhamini wengine tunaoshirikiana nao katika kuanikisha mbio hizi na ahadi yetu ni kuwa tutaendelea kushirikiana nao katika kufanikisha mashindano haya yazidi kuweko kwa muda mrefu ujao”, amesema.

Naye mwakilishi wa Yas Tanzania ambao ni wadhamini wa mbio za kilomita 21.1 za Yas half-Kilimanjaro marathon Innocent Rwetabura amesema kuwa kampuni hiyo inajivunia kuwa sehemu ya mbio za Kilimanjaro marathon ambazo alisema zimeipaisha Tanzania kwenye nyanja za kimataifa kupitia sekta ya michezo.

“Tumekuwa wadhamini wa mbio hizi kwa muda wa miaka 10 sasa na mafanikio yake yanaonekana, nichukue fursa hii kkuahidi kwa niaba ya uongozi wa kampuni ya kuwa tutaendelea kuwa sehemu ya mafanikil haya kupitia udhamini wetu ili kuendeleza mafanikio haya ambayo ni muhimu kwa Taifa letu”, amesema.
 

Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko (katikati), akimkabidhi mfano wa hundi mshindi wa kwanza Yas Half marathon, Failuna Matanga, katika Mashindano ya Kilimanjaro Marahton yaliofanyika leo Februari 23, 2025 katika Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi Mkoani Kilimanjaro
 

 Naibu Waziri Mkuu, Dkt. Doto Biteko (katikati), akiongoza mbio za Kilimanjaro Maratho  zilizofanyika leo Februari 23, 2025 katika Chuo Kikuu cha Ushirika, Moshi Mkoani Kilimanjaro


Related Posts