WAKATI Simba na Azam zikishuka uwanjani kesho jioni katika Mzizima Derby, vinara na watetezi wa Ligi Kuu Bara, Yanga jana ilimaliza kazi kwa kuweka rekodi nyingine ya kupata ushindi mkubwa Uwanja wa Lake Tanganyika baada ya kuifyatua Mashujaa kwa mabao 5-0.
Kabla ya kipigo hicho, Mashujaa ilikuwa haijawahi kufungwa idadi kama hiyo tangu ipande daraja msimu uliopita uwanja wa nyumbani, kwani kipigo kikubwa zaidi mjini humo ilikuwa 3-0 kutoka kwa Azam FC msimu uliopita.
Katika mchezo huo uliopigwa kuanzia saa 10:00 jioni, ilishuhudiwa mabao yote matano yakiwekwa wavuni na nyota wa kigeni, huku mtokea benchi, Clatous Chama akitupia mawili na kumfanya afikishe mabao matatu, wakati Prince Dube alifunga bao la 10 kwa msimu huu akiwa na kikosi hicho.

Ushindi huo wa 18 umeifanya Yanga kufikisha pointi 55 baada ya mechi 21 na ikiwa haina presha yoyote kwa sasa licha ya wapinzani wao, Simba na Azam zikipepetana usiku wa kesho, kwani hata zikishinda haziwezi kuing’oa kileleni.
Mashujaa iliyotoka kushinda mabao 2-0 dhidi ya Pamba Jiji baada ya awali kucheza dakika 720 bila kuonja ushindi, ilicheza kwa nidhamu kipindi cha kwanza na kufungwa bao moja tu, kabla ya kipindi cha pili kuelemewa na kasi ya ‘Gusa Achia Pro Max’ ya vijana wa Yanga iliyo chini ya Miloud Hamdi.

Haikuwa kazi ngumu kwa Yanga kupata ushindi huo kwani ikitawala mchezo huo kwa dakika zote 90, japo kipindi cha kwanza ilipoteza nafasi nyingi ilizotengeneza na kwenda mapumziko ikiwa na bao moja tu lililofungwa na Duke Abuya dakika ya 31 baada ya mbeki wa Mashujaa kujichanganya wakati wa kuokoa mpira langoni mwao na mfungaji kumpiga tobo, kipa Patrick Munthali.
Mashujaa inayofundishwa na Kocha Abdallah Mohammed ‘Baresi’ ilijitahidi kuibana Yanga na kufanya isipigwe nyingi katika kipindi hicho cha kwanza.
Kipindi cha pili kilianza kwa Yanga kuwashtukiza wenyeji kwa kufunga bao la pili kupitia kichwa cha Prince Dube aliyemalizia krosi tamu ya Pacome Zouzoua aliyeupiga mwingi jana na kuchaguliwa Nyota wa Mchezo.
Bao hilo la dakika ya 48 kwa Dube limemfanya afikishe mabao 10 akiungana na Clement Mzize anayekipiga naye Yanga na nyota wa Simba Jean Charles Ahoua wakichuana katika orodha ya wafungaji wa Ligi Kuu kwa sasa ligi ikimalizia raundi ya 21.

Kiungo Pacome alikuwa moto mbaya kwa Mashujaa akitoa asisti mbili kwa Dube alilofunga kwa kichwa krosi aliyopiga kwa mguu wa kushoto kisha kupiga frikikii iliyounganishwa wavuni na Khalid Aucho likiwa bao lake la kwanza alililoitoa kwa Maxi Nzengeli aliyemuahidi mapema kama angefunga jana angempa Sh100,000.
Pacome alikuwa akiwachukua na kuwageuka mabeki wa Mashujaa kwa dakika zote 90 alizokuwa uwanjani.
Kabla ya mchezo huo kulikuwa na maneno mengi juu ya Chama hana furaha ndani ya Yanga, hivyo kufuta picha akiwa na jezi za timu hiyo lakini jana akaingia dakika ya 69 akichukua nafasi ya Stephanie Aziz KI na kwenda kupiga mabao mawili dakika za 74 na 83 ikiwa ni ndani ya dakika tisa tu.
Mabao hayo aliyotengenezewa na Duke Abuya na Maxi Nzengeli aliyeingia naye muda huohuo yanamfanya Mzambia huyo fundi kufikisha mabao matatu na asisti mbili tangu asajiliwe na Yanga msimu huu akitokea Simba.

Huu unakuwa ushindi mkubwa wa nne kwa Yanga mkubwa ambapo imezifunga Fountain Gate (5-0), KenGold (6-1) na dhidi ya KMC (6-1) na kuifanya hadi sasa ikiwa imecheza mechi 21 kufikisha mabao 55 sawa na pointi ilizonazo na sasa inaifuata Pamba Jiji iliyoinyoa mabao 4-0 jijini Dar es Salaam.
Katika mechi ya mapema saa 8:00 mchana Singida Black Stars ikiwa nyumbani Uwanja wa Liti, Singida ilibanwa na kutoka sare ya mabao 2-2 na Pamba Jiji, straika Jonathan Sowah akifunga kwa penalti akifikisha bao la nne tangu asajiliwe dirisha dogo, huku Serge Pokou akifunga bao la kwanza akiwa na kikosi hicho, huku mabao ya wageni yakiwekwa na Mkenya Mathew Momanyi aliyefunga mara mbili.