Abiria aliyekuwa akisafiri Mwanza- Dar afariki njiani

Morogoro. Abiria Godfrey David Mbaga aliyekuwa akisafiri kutoka mkoani Mwanza kwenda jijini Dar es Salaam kwa basi la Kampuni ya Ally’s ameshindwa kufika alilokuwa anakwenda baada ya kufariki dunia eneo la Mikese, mkoani Morogoro.

Akizungumza na waandishi wa habari leo Jumatatu, Februari 24, 2025, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro, Alex Mkama amesema tukio hilo limetokea jana Jumapili ambapo mkazi huyo wa Mwanza mwenye umri kati ya miaka 25 hadi 30 alifariki dunia.

Amesema wakati wakiwa safarini walipofika eneo la Mikese, Wilaya na Mkoa wa Morogoro abiria huyo alianza kujisikia vibaya na kufikishwa hospitali kwa matibabu lakini hakupata nafuu na hatimaye alifariki dunia.

“Kwa sasa mwili wake umehifadhiwa chumba cha maiti katika Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro kusubiri ndugu wa marehemu kwa ajili ya utambuzi na uchunguzi,” amesema.

Katika tukio lingine Kamanda Mkama amesema asubuhi ya leo Jumatatu, katika eneo la Cape Town Mtaa wa Kambi Tano Kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro, mwili wa mtoto Ester Banzi (10), mwanafunzi wa darasa la tano katika Shule ya Msingi Juhudi umekutwa kwenye dimbwi la maji.

Inaelezwa kuwa jana Jumapili zilitolewa taarifa za kutoonekana kwa mtoto huyo katika kituo cha Polisi Kihonda na jitihada za kumtafuta zilifanyika hadi mwili wake  ulipopatikana akiwa anaelea juu ya dimbwi hilo.

“Tunaendelea kufanya uchunguzi ili kujua huyo mtoto alifariki katika mazingira gani na niwasihi wazazi na walezi kuwa wavumilivu na watulivu wakati tukiendelea na uchunguzi,” amesema kamanda Mkama.

Amesema mwili wa mtoto huyo umehifadhiwa chumba cha maiti Hospitali ya Rufaa Mkoa wa Morogoro.

Kufuatia tukio hilo, Jeshi la Polisi mkoani humo,  linatoa wito kwa ndugu jamaa na marafiki wanaomfahamu marehemu aliyefariki kwenye basi wafike kutambua na kuchukua mwili kwa hatua za mazishi.

Vilevile, Jeshi la Polisi Mkoa wa Morogoro linawataka wananchi kutoa ushirikiano kwa kutoa taarifa zitakazosaidia kubaini sababu au kifo cha mtoto Ester.

Related Posts