ACT- Wazalendo yaviita vyama kupambania mageuzi mfumo wa uchaguzi

Dar es Salaam. Zikiwa zimepita siku chache tangu Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), kutoa tamko la kutaka marekebisho ya mfumo wa uchaguzi katika kipindi hiki cha kuelekea uchaguzi mkuu Chama cha ACT Wazalendo nacho kimekuja na azimio la kutaka mageuzi ya mfumo wa uchaguzi.

Mwenyekiti wa Chadema, Tundu Lissu Jumatano Februari 12,2025 alieleza dhamira ya chama hicho kutaka mabadiliko kwenye mfumo wa uchaguzi ili kuhakikisha mchakato huo unakuwa huru na haki.

Akizungumza leo Februari 24,2025 mbele ya waandishi wa habari Katibu Mkuu wa ACT Wazalendo, Ado Shaibu amesema wameshaviandikia barua vyama vya NCCR-Mageuzi, ADC, Chama cha Wananchi (CUF) na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) kwa ajili ya kushikamana kupambania suala hilo.

Hatua hiyo inakuja baada ya Halmashauri Kuu ya chama hicho kukutana jana jijini Dar es Salaam.

“Halmashauri Kuu imeazimia kwamba kipaumbele cha chama kwa sasa ni kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini utakaohakikisha haki na kuheshimiwa maamuzi na matakwa ya wananchi.

“Aidha, Halmashauri Kuu imeelekeza kwamba suala la kushiriki ama kutoshiriki uchaguzi kabla ya kufanyika marekebisho yanayotakiwa litaamuliwa na kamati ya uongozi ya Taifa katika wakati muafaka,” amebainisha.

Amesema katika kutekeleza hilo, Halmashauri Kuu imeelekeza kuwa chama kiendeleze ushirikiano na vyama vingine makini vya upinzani na wadau wengine muhimu wa demokrasia ikiwemo asasi za kiraia na viongozi wa dini,  kujenga vuguvugu la kitaifa la kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini.

“Chama kijikite katika kupigania maboresho ya mfumo wa uchaguzi nchini ikiwemo kufanyika kwa mabadiliko madogo ya katiba, kuundwa kwa tume huru ya uchaguzi na kupinga kwa nguvu zote kura ya mapema kwa upande wa Zanzibar.”

Akizungumza zaidi amesema vyama hivyo vinapaswa kuja na kauli ya pamoja, akitolea mfano Chadema walishaiandikia barua na wanawasiliana nayo kwa ajili ya kujadiliana na viongozi na hadi sasa kuna mazungumzo mbalimbali yanaendelea kati yao.

Amesema chama hicho hakitakubali tofauti ndogondogo za ushindani wa kisiasa na migongano ziwagawanye, bali kimeazimia kiendeleze ushirikiano na vyama vingine kujenga vuguvugu la kupigania maboresho.

“Wameonesha utayari tumeanza kukutana na kujadiliana tunashikamana kila chama kina fikra zake hivyo mwisho wa siku vyama vyote vinatoka na msimamo mmoja,” amesema Shaibu.

Awali wakati vyama hivyo vikionesha nia ya kuwa pamoja vyama kama Chama cha National League for Democracy (NLD), kimesema hakina mpango wa kushiriki muungano wa upinzani kwa sababu mwaka 2015 kilishiriki ushirikiano ulioshindwa kuheshimu makubaliano.

Katibu Mkuu wa chama hicho, Doyo Hassan Doyo, Februari 22, 2025 aliiambia Mwananchi kuwa hakuna sheria inayoruhusu vyama kuungana, hivyo badala ya kuzungumzia muungano, kinachohitajika ni mabadiliko ya sheria ili kuweka mfumo wa kugawana rasilimali za uchaguzi.

Pia, Mwenyekiti wa Alliance for Democratic Change (ADC), Shaban Itutu, ameweka bayana kuwa chama chake kitashiriki uchaguzi huku kikiendelea kudai mabadiliko ya sheria za uchaguzi na katiba mpya

Nacho, Chama cha NCCR- Mageuzi kimesema kitashiriki uchaguzi mkuu  huku kikiweka msimamo kwamba hakitaungana na chama chochote katika uchaguzi huo kwa kuwa hakijasahau  maumivu ambayo waliyapata katika uchaguzi wa mwaka 2015

Chama hicho ni moja ya vyama vilivyounda Umoja wa Katiba ya Wananchi (Ukawa) mwaka 2015 ikihusisha Chadema, Chama cha Wananchi (CUF), NCCR na NLD.

Katika umoja huo waliamua kusimamisha mgombea mmoja katika nafasi za ubunge na udiwani na kumuunga mkono kwa kuangalia eneo ambalo chama kinakubalika  kama moja ya njia ya kukikabili Chama cha Mapinduzi (CCM).

Ikumbukwe wakati joto la kuelekea uchaguzi linaendelea kufukuta katika uchaguzi wa mwaka 2015, Ukawa  ulitikisa nchi wakati ulipomsimamisha mgombea urais hayati Edward Lowassa.

Hata hivyo, barua zilizoandikwa na ACT kuhusu mapambano ya mageuzi ya mfumo wa uchaguzi ni uthibitisho wa kuunganisha nguvu kama iliyotikisa mwaka 2015 ingawa sheria hairuhusu, ila kwa mujibu wa ACT muungano wanaoupigania ni kuboresha mfumo kabla ya uchaguzi.

Akizungumza na Mwananchi Mkurugenzi wa sheria na uchaguzi wa ADC, John Mbogo amesema wao hawana shida kufanya ushirikiano ila kitu wanachokiepuka ni ubinafsi ambao unaonekana kwa baadhi ya vyama vikubwa ambavyo vinaamini uamuzi ni wa kwao wenyewe bila ushirikiano

“Lakini sisi hatutaki mtu atutumie kwa ajili ya kujaza namba na sisi ni chama kikubwa tunajiamini na tuna uwezo wa kufanya kitu kikubwa. Kufanya ushirikiano na vyama vingine je, tukubaliane ushirikiano utakuaje tunafanya katika mfumo upi ndio tutakaa chini,” amesema.

Amesema, kwa sasa ni ngumu kusema kwa undani lakini tutakaa mezani tuone tunafanyaje tuweke mchakato mezani na tutapeleka katika mfumo wa kisheria tuangalie tunabanwa katika sheria zipi za uchaguzi.

“Sisi tuko tayari twende katika mfumo wa kisheria tuendeshe katika mpangilio wa kisheria na tukiona kila kitu kinaruhusu basi tuko tayari,” amesema Mbogo.

Kwa upande wake Makamu Mwenyekiti wa Chama cha NCCR-Mageuzi, Joseph Selasini amesema kwanza dhumuni lao limekuwa siku zote kupigania mfumo bora tangu kuanza kwa chama hicho.

“NCCR tunaamini katika mashauriano na kama wao wameona ni vyema kushauriana sisi hatukatai wala hatuchagui chama cha kushauriana nacho, kwani ni faida kwa wananchi na Taifa kwa ujumla.”

 “Mfano hakuna ukweli kwamba chama kimoja cha siasa kinachopambana na vingine 18 kipate asilimia 99. Tunataka tunapoendelea kwenye ushirikiano huo tuanzie pale tulipoishia,” amesema Selasini.

Akizungumzia hatua hiyo ya ACT,  mchambuzi wa masuala ya siasa na mhadhiri kutoka Chuo Kikuu cha Dodoma (Udom), Dk Paul Loisulie amesema inaleta sura mpya ya upinzani wa Tanzania hasa katika vyama vikubwa.

Amesema kama kweli wameamua kuja na hatua hiyo watapata mafanikio kwa sababu siku zote umoja ni nguvu na utengano ni udhaifu.

“Kingekuwa ni chama kimoja pekee ingekuwa ngumu lakini hatua hii inaenda kuleta urahisi na wanathibitisha hoja ya Chadema iko sawa.

“Wanahalalisha kwamba kuna changamoto ya mifumo yetu ya uchaguzi hivyo wanaongeza nguvu kupigania maboresho,” amesema mhadhiri huyo.

Related Posts