Shinyanga. Mkazi wa kata ya Kitangili iliyopo katika Halmashauri ya Manispaa ya Shinyanga, Daniel Mussa Mageni (27) anadiwa kufariki dunia kwa kupigwa shoti ya umeme wakati akijaribu kuiba nyaya za umeme kwenye transfoma iliyopo kitongoji cha Isenegeja, Kijiji cha Isela wilayani Shinyanga.
Tukio hilo limetokea leo Februari 24, 2025 baada ya shuhuda, John Shija kumkuta kijana huyo amefariki pembeni ya transfoma hiyo iliyopo jirani na zahanati ya Isela na vifaa alivyokuwa akitumia kukata nyaya vikiwa katika eneo hilo.
“Nilipokuwa napita kuelekea kwenye shughuli zangu, nimekuta kijana huyu ameanguka pembeni ya transfoma, nikatoa taarifa kwa uongozi wa kijiji,” amedai Shija.

Mwenyekiti wa Kitongoji cha Isegeneja, Amina Hamis Bwire amedai Mageni amefariki saa mbili asubuhi baada ya kupigwa na shoti ya umeme wakati akijaribu kuhujumu miundombinu ya Shirika la Umeme Tanzania (Tanesco).
“Kijana huyu amebainika kuwa amefariki saa mbili asubuhi baada ya kujaribu kuiba nyaya kutoka kwenye transfoma. Mwananchi mmoja amemkuta akifanya uharibifu huo, ndipo akaleta taarifa kwangu na nikawapigia watu wa Tanesco na Polisi,” amedai Amina.
Kwa upande wake, Mhandisi Mwandamizi wa Tanesco Mkoa wa Shinyanga, Anthony Tarimo, akizungumza kwa niaba ya Meneja wa Tanesco mkoani humo, amedai kijana huyo amefariki dunia wakati akiingilia njia ya umeme mkubwa katika transfoma hiyo,
“Kitaalamu ameingilia njia ya umeme mkubwa, ameingilia usalama wa Transfoma na kupata ajali hiyo pia alijaribu kuiba nyaya za shaba zinazolinda usalama wa Transfoma ndipo alipopigwa shoti” amedai Tarimo.
Tarimo amewataka wananchi kuwa waangalifu na kuacha vitendo vya kuhujumu miundombinu ya umeme, huku akisisitiza kuwa ulinzi wa miundombinu hiyo ni jukumu la kila mmoja.
“Ulinzi wa miundombinu ya umeme ni jukumu letu sote, toeni taarifa kuhusu wanaohujumu pia wananchi epukeni kusogea kwenye transfoma na njia za umeme kwani ni hatari, ukiangalia hata hapa kwenye hii transfoma kuna onyo kabisa kwamba ni hatari,” amesema Mhandisi Tarimo.

Kamanda wa Jeshi la Polisi Mkoa wa Shinyanga, Janeth Magomi amethibitisha kutokea kwa tukio hilo nakuendelea na uchunguzi wa awali na mwili wa marehemu ulichukuliwa na kupelekwa katika chumba cha kuhifadhia maiti kwa uchunguzi zaidi.
“Tukio hilo limebainika leo saa mbili asubuhi baada ya kijana huyo kujaribu kuiba nyaya za umeme kutoka kwenye transfoma, ndipo akapigwa shoti. Mwili wake amechukuliwa kwa ajili ya uchunguzi, baada ya hapo utakabidhiwa kwa familia kwa ajili ya taratibu za mazishi,” amedai.