ALAF yafanya kweli Kilimanjaro International Marathon

 

KAMPUNI ya ALAF Limited imeahidi kuendelea kuwawezesha wafanyakazi wake kuimarisha afya ya mwili na akili ili kuzidisha ufanisi wao wawapo kazini

Meneja Rasilimali Watu wa ALAF Jumbe Onjero ameeleza hayo hivi karibunj wakati akitoa taarifa kwa Naibu Waziri Mkuu na Waziri wa Nishati,. Dkt.Doto Biteko alipotembelea banda la kampuni hiyo kwenye Maonyesho ya The People’s Expo.

Maonyesho hayo yalikuwa ni sehemu ya matukio yanayohusiana na mbio za kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon yaliyofanyika Jumapili Februari 23, 2025, katika Uwanja wa Chuo Kikuu cha Ushirika Moshi (MoCU) mjini Moshi mjini, mkoani Kilimanjaro.

Amesema walidhamini zaidi ya washiriki 50 katika mbio za mwaka huu na kwamba ushiriki wao umekuwa jambo zuri na la kukumbukwa, ambapo wafanyakazi wa kampuni hiyo walishiriki katika vipengele vyote vya mbio hizo ambazo ni kilomita 42.2 za Kilimanjaro Premium Lager, mbio za kilomita 21.1 maarufu kama YAS half marathon na mbio za kujifurahisha za kilomita 5 zinazodhaminiwa na CRDB Bank.

“Tutaendelea kuunga mkono mbio hizi kwa lengo la kuinua sekta ya michezo sambamba na kuhakikisha wafanyakazi wetu wanafanya mazoezi yatakayoimarisha afya zao kupitia mbio za Kilimanjaro International Marathon”, amesema.

Amesema hivi karibuni ALAF ilizindua klabu yake ya jogging inayojumuisha wafanyakazi kutoka vitengo mbalimbali vya kampuni hiyo ambapo wafanyakazi wataendelea kufanya mazoezi kwa ajili ya kushiriki mbio mbio za Kimataifa za Kilimanjaro Premium Lager International Marathon.

Kuhusu Maonesho yanayoendana na mbio hizo, amesema hii ni mara ya kwanza kwa ALAF kushiriki katika hafla hiyo inayokutanisha zaidi ya watu 20,000 kwa wakati mmoja.

“Mbio hizi pamoja na maonyesho haya ni moja ya matukio makubwa nchini Tanzania na kama kampuni iliyojizatiti kuboresha maisha ya watu kupitia bidhaa na huduma zake kwa ujumla, tulipata fursa ya kuwasiliana moja kwa moja na wateja wetu na kujibu maswali kuhusiana na huduma zetu,” amesema.

Aidha amebainisha kuwa maonyesho hayo yalikuwa ni fursa nzuri kwa kampuni hiyo kuwafahamisha wateja wake wa mwishoni mwa mwaka jana, ALAF imeanza uzalishaji wa mabati ya rangi kupitia mtambo wake mpya wa mabati ya rangi.

Kampuni ya ALAF Limited (ALAF) ni kampuni inayoongoza kwa utengenezaji wa vifaa vya chuma vyenye ubora wa hali ya juu ambavyo ni maalum kwa ajili kuezekea paa za nyumba.

Tangu kuanzishwa kwake mwaka wa 1960, ALAF imeendelea kutoa mchango mkubwa katika sekta ya ujenzi hapa nchini.

Shughuli za ALAF hazihusiani na uzalishaji wa vifaa vya chuma za kuezekea tu bali pia inajihusisha na uzalishaji wa koili za chuma zilionakshiwa kwa rangi kwa ajili ya matumizi mablimbali kwenye sekta ya ujenzi pamoja na mirija ya chuma na mabomba kwa ajili ya matumizi mbalimbali.

Related Posts