Morogoro. Baba mzazi wa mtoto Esther, aliyekutwa amekufa kwenye dimbwi la maji, Isaya Banzi ameeleza namna binti yake alivyopotea kabla na mwili wake kukutwa kwenye dimbwi hilo eneo la Cape town mtaa wa kambi tano kata ya Lukobe Manispaa ya Morogoro.
Banzi ambaye ni dereva wa bodaboda amedai juzi Februari 22, 2025 alimpeleka binti yake huyo kwa Mchungaji, Michael Nyanda kwa lengo la kwenda kumfanyia maombi kutokana na tatizo la kusinzia hasa akiwa darasa.
“Mchungaji alikuwa akifanya maombi kwenye kanisa lake ambalo lipo jirani na nyumba anayoishi, nilipomfikisha nilimuacha kwa mchungaji ili aweze kumfanyia maombi, mimi nilirudi kulala nyumbani na ilipofika jana asubuhi kabla sijaenda kwenye shughuli zangu za bodaboda nilimpigia mchungaji kujua mwanangu anaendeleaje, lakini hakupokea simu wala kujibu ujumbe hadi ilipofika saa 10 jioni ndipo aliponitumia ujumbe kuwa tayari ameshamaliza maombi tangu asubuhi na ameshamruhusu mtoto kurudi nyumbani,” amedai Banzi.
Ameongeza, “Baada ya kupata ujumbe wa mchungaji kuwa kamruhusu mtoto kurudi nyumbani nilifanya mawasiliano na mama yake mlezi kujua kama amefika nyumbani lakini niliambiwa hajarudi, na hapo ndio kazi ya kumtafuta ilipoanza lakini hatukuweza kumpata mpaka Februari 24 alfajiri ndipo nilipojulishwa na mwenyekiti kuwa mwili wa binti yangu umekutwa ukielea kwenye dimbwi la maji,”
Banzi amesema tatizo la binti yake kusinzia lilimuanza tangu mwaka 2023 na amehangaika kumtibu katika maeneo mbalimbali hadi ilipofika juzi ambapo alipompeleka kwa mchungaji huyo kwa ajili ya maombi.
“Mwanzoni kabisa tatizo hili la kusinzia lilipomuanza alikuwa pia akipata hali kama bumbuazi, unaweza kumsemesha na asikujibu zaidi ya kukuangalia hadi haja ndogo inamtoka bila mwenyewe kujijua, lakini pamoja na hali hiyo alikuwa anakwenda mwenyewe shule na kurudi hakuwahi kuanguka hata siku moja,” amesema Banzi.
Amesema kifo cha binti yake kimempa maswali mengi huku akiwa hajui kimesababishwa na nini hasa kutokana na mazingira ulipokutwa mwili wake.
“Kitu kingine kinachonipa maswali ni kwamba yale maji kwenye dimbwi sio ya kumuua mtu hasa binti mwenye umri kama huu wa miaka 10, halafu eneo ulipokutwa mwili jana tulipita eneo hilohilo wakati tunamtafuta binti yangu na hatukumuona. Sasa najiuliza kama alianguka au alizama mwenyewe kwa nini mwili hatukuona mapema wakati tunatafuta,” amesema Banzi.
Banzi amesema pamoja na mazingira hayo ya utata lakini pia anajiuliza kwa nini mchungaji hakumpa mapema taarifa za kumruhusu binti huyo baada ya kumaliza maombi na kwa nini hakupokea simu wala kujibu ujumbe alipomuuliza hali ya binti yale.
“Siwezi kusema mchungaji ndio amefanya tukio hili lakini mazingira ya tukio ndio yenye utata, maana huyu mchungaji ni mwenyeji na tayari amesaidia watu wengi waliokuwa na matatizo na mimi mwenyewe hao waliosaidiwa nawajua maana baadhi nilikuwa wananikodi kama bodaboda kuwapeleka kwenye kanisa lake, isipokuwa naliomba Jeshi la Polisi kufanya uchunguzi wa kina ili nijue kilichomuua binti yangu, mi sina ugomvi na mtu hivyo siamini kama inaweza kuwa kisasi,” ameeleza Banzi.
Akieleza mazingira aliyokuwa akiishi na binti yake huyo Banzi amesema mama (mzazi mwenzake) walishaachana miaka mingi hivyo mtoto huyo alikuwa akimlea mwenyewe kwa kusaidiwa na mke aliyenaye kwa sasa (mama wa kambo) na kwamba tangu amemchukua binti yake huyo akiwa na miaka mitano, hajawahi kuona unyanyasaji wala ukatili wowote kutoka kwa mama huyo mlezi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa Mtaa wa Kambi Tano, Eliamini Kimaro amesema alipokea taarifa za kupatikana kwa mwili huo leo asubuhi baada ya kupigiwa simu na wananchi wa mtaa huo na alipofika eneo la tukio alikuta mwili wa binti kwenye dimbwi hilo.
“Kwa mimi nilivyoangalia lile dimbwi siamini kama yale maji ndio yameweza kumuua yule binti mkubwa vile, na hata mwili wake haukuwa umezama wala kuelea katikati ya maji, isipokuwa niliona sehemu ya tumbo na upande mmoja wa uso ndio ilikuwa kwenye maji, lakini miguu ilikuwa kwenye tope, Kwa mazingira haya polisi wanayo kazi ya kuchunguza kwa kina kujua nini kimemuua huyo binti,” amesema Kimaro.
Kimaro amesema taarifa alizopata mchana wa leo zinadai kuwa mchungaji aliyehusika kumuombea binti huyo kabla ya mwili wake kukutwa kwenye dimbwi hilo anashikiliwa na polisi kwa mahojiano zaidi.
Baadhi ya wanafunzi wanaosoma na binti huyo wamesema hawajawahi kumuona mwenzako huyo akianguka kifafa na hata wakiwa shule alikuwa akicheza kama kawaida.
Kamanda wa Polisi Mkoa wa Morogoro Alex Mkama leo Februari 24, 2025 amethibitisha kutokea kwa tukio hilo.
Katika taarifa hiyo ya kamanda Mkama imeeleza kuwa jana Februari 23 katika kituo cha Polisi Kihonda lilifunguliwa taarifa ya kupotea kwa binti huyo hata hivyo jitihada za kumtafuta zilifanyika hadi mwili ulipopatikana akiwa anaelea juu ya dimbwi hilo.