Mbeya. Chama cha Mapinduzi (CCM) Mkoa wa Mbeya kimesema licha ya ujio wa kampeni ya msaada wa kisheria, bila kubadili mienendo na tabia za wananchi, migogoro haitaisha, huku kikiwataja baadhi ya wanasheria na mawakili kujihusisha na vitendo vya rushwa.
Akizungumza leo Februari 24, 2025 wakati wa uzinduzi wa kampeni hiyo mkoani humo, mwenyekiti wa chama hicho mkoa, Patrick Mwalunenge amesema migogoro haitaisha iwapo wananchi hawatabadili tabia.
Amesema baadhi ya mawakili na wanasheria wamekuwa wakijihusisha na vitendo vya rushwa akieleza kuwa kukithiri kwa migogoro mkoani humo ni kutokana na mienendo na tabia za wananchi.
“Baadhi ya mawakili na wanasheria siyo waadilifu, wanajihusisha na vitendo vya rushwa na ushahidi ninao, pale ofisi zetu za chama kuna mtu alidhulumiwa akaenda mahakamani akanyang’anywa haki yake, lakini CCM ilimrudishia haki yake,”
“Niwaombe wananchi tumieni hii fursa ya kampeni ya msaada wa kisheria kuwasilisha kero na changamoto zenu kwenye vyombo husika ikiwamo Takukuru (Taasisi ya Kupambana na Kuzuia Rushwa), lakini tuzungumze na familia zetu ili kuwa katika mstari ulionyooka,” amesema Mwalunenge.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa Chama cha Wanasheria cha Tanganyika (TLS), Nyanda za Juu za Kusini, Baraka Mbwilo amesema Mbeya imekumbwa na migogoro mingi inayotokana na mwingiliano wa shughuli za kiuchumi, mila potofu na tabia za wananchi.
Amesema migogoro mikubwa ni ya mirathi, ambapo wajane ndio hukumbwa na unyanyasaji pale mume wake anapofariki familia yao huingia kati kuchukua mali bila kujua utaratibu.
“Lakini pia kuna migogoro ya ndoa, hili ni nchi nzima, migogoro ya ardhi kutokana na uvamizi na mamlaka za serikali kugawa maeneo mara mbili na zaidi wanaonyanyasika ni wale wenye vipato vya chini,” amesema Mbwilo.
Akifungua kampeni hiyo, Mkuu wa Mkoa wa Mbeya, Juma Homera amesema huduma ya msaada wa kisheria itawafikia wananchi wote katika halmashauri za mkoa huo ili kila mmoja kuwasilisha kero na kusaidiwa.
Amesema huduma ya msaada wa kisheria inatarajia kuhitimishwa Machi 10 badala ya tarehe ya awali, Machi 5, 2025 akieleza kuwa mkoa huo utaenda kutoa vyeti vya kuzaliwa kwa wanafunzi wote wa shule za mkoani humo.
“Rais Samia amekuwa kinara katika utoaji haki nchini, amesisitiza utekelezaji wa 4R, kampeni hii ni muhimu katika kutoa haki na Mbeya itahitimishwa Machi 10 kuhakikisha wananchi wanapata huduma,” amesema Homera.
Mmoja wa wananchi katika stendi ya Kabwe, Mwajuma Mbeyale amesema wananchi wengi wanashindwa kwenda mahakamani kutokana na kukosa gharama za mawakili na wanasheria.
“Hii ni fursa kwetu wenye kipato cha chini, lakini Serikali iangalie namna ya kusaidia baada ya kampeni hii, uwepo utaratibu wa kupunguza gharama za mawakili kuwe na kiwango maalumu,” amesema Mwajuma.