Kigoma. Hatima ya uhalali wa uchaguzi wa wenyekiti wa Serikali za Mitaa Saba katika Kata Saba za Manispaa ya Kigoma Ujiji, itajulikana ndani ya Juma hili wakati Mahakama ya Wilaya ya Kigoma itakapotoa hukumu ya mashauri ya kupinga uchahuzi huo kuanzia leo.
Mashauri hayo yamefunguliwa na wanachama wa Chama cha Alliance for Change and Transparency (ACT- Wazalendo), waliogombea nafasi hizo za uenyekiti katika mitaa hiyo, wakati wa Uchaguzi wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji wa mwaka 2024.
Wamefungua shauri hayo dhidi ya wenyeviti wa mitaa hiyo, wa Chama Cha Mapinduzi walitangazwa kuwa washindi katika mitaa hiyo walitangazwa kuwa washindi wa nafasi hiyo kupitia Chama cha Mapinduzi (CCM), wakiwa wajibu maombi (walalamikiwa) wa kwanza.
Walalamikiwa wengine katika mashauri hayo ni wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi ngazi ya mitaa katika mitaa hiyo inayolalamikiwa na Msimamizi wa Uchaguzi, Halmashauri ya Manispaa ya Kigoma Ujiji (ambaye ni Mkurugenzi wa Manispaa hiyo.
Mahakama hiyo baada ya kukamilisha usikilizwaji wa ushahidi wa pande zote inatarajiwa kuanza kutoa hukumu kuanzia leo Jumatatu, Februari 24, 2025 mpaka Alhamisi, Februari 27, 2025.
Usikilizwaji wa mashauri hayo yaliyosikilizwa na mahakimu tofautitofauti uliochukua takribani majuma mawili mfululizo, ulihitimishwa Ijumaa, Februari 21.
Kwa leo mahakama hiyo inatarajiwa kutoa hukumu za mashauri matatu ya mitaa mitatu tofauti.
Hukumu hizo ndizo zitakazotoa hatima ya uchaguzi wa mitaa hiyo iwapo ni halali au ni batili kutegemeana na uzito wa ushahidi wa walalamikaji na utetezi wa walalamikiwa.
Ikiwa Mahakama itashawishika na ushahidi wa walalamikaji kuwa ulikuwa mzito ulioweza kujenga kesi na kuridhika kuwa ulikuwa na kasoro kubwa zilioathiri uhalali wake kwa mujibu wa sheria na kanuni za uchaguzi huo zilizowekwa basi inaweza kuubatilisha na kutengua matokeo yaliyowapa ushindi walitangazwa washindi.
Katika mazingira hayo itatoa amri ya kurudiwa kwa uchaguzi huo, amri ambayo nafuu muhimu ambayo walalamikaji katika kila shauri wameiomba.
Lakini kama itaona kuwa ushahidi huo wa walalamikaji haukuweza kuthibitisha madai yake kwa kiwango kinachotakiwa itayatupilia mbali mashauri na kwa maana hiyo itakuwa imeuhalalisha.
Hata hivyo uamuzi wa mahakama hiyo hautakuwa wa mwisho kwani kwa upande ambao hautaridhika utakuwa na haki ya kukata rufaa Mahakama Kuu kuupinga na hata mpaka Mahakama ya Rufani, kama utaona kuna sababu za msingi.
Ni nini ambacho Mahakama itakiamua na amri gani itaiotoa katika uchaguzi wa mtaa gani, kitajulikana baada ya kusomwa kwa hukumu hizo.
Katika mashauri hayo, wanapinga mwenendo na matokeo ya uchaguzi huo wakidai kuwa ni batili kwa kuwa haukuwa huru na wa haki kutokana na kasoro mbalimbali wanazodai kuwa zilijitokeza kabla, wakati na baada ya upigaji kura.
Kasoro hizo wanadai kuwa ni pamoja na ukiukwaji wa kanuni za uchaguzi zilizowekwa katika upigaji kura kuhesabu na kutangaza matokeo na kuwepo kwa kura bandia zilizoingizwa katika masanduku ya kura isivyo halali.
Katika mitaa mingine wanadai kutokea vurugu zilizowalazimu wasimamizi kukimbia na masanduku ya kura bila kuhesabiwa lakini baadaye wagombea wa CCM wakatangazwa washindi.
Wanadai kuwa kuwepo kura hizo bandia kumesababisha tofauti ya idadi ya kura zilizopigwa kati ya nafasi ya uenyekiti wa mtaa na nafasi za wajumbe.
Hivyo wanaiomba mahakama hiyo itamke kuwa uchaguzi huo ni batili, iwaamuru wasimamizi wasaidizi wa uchaguzi wa mitaa hiyo watangaze uchaguzi ndani ya siku saba au 14 na kufanya uchaguzi mwingine ndani ya siku 60.
Katika kuthibitisha madai yao hayo pamoja na ushahidi wa mdomo walioutoa mahakamani chini ya kiapo pia wengi wamewasilisha ushahidi wa nyaraka hususan fomu za matokeo zilizopokewa mahakamani kuwa vielelezo vya ushahidi wao.
Fomu hizo zinaonesha idadi ya wapiga kura waliojiandikisha, waliopiga kura, kura halali, zilizoharibika na idadi ya kura alizopata kila mgombea wa nafasi hiyo ya uenyekiti.
Walalamikiwa katika utetezi wao walikana madai yote yaliyoibuliwa na walalamikaji, wakidai uchaguzi ulifanyika kwa uhuru na haki na kwamba hapakuwa na ukiukwaji wowote wa sheria na kanuni, wala kuwepo kura bandia huku wakikana kuzitambua fomu hizo hata za matokeo zikizowasilishwa na walalamikaji.
Hata hivyo hakuna hata mmoja aliyetoa ushahidi wa nyaraka hususan fomu za matokeo ya uchaguzi huo wanazozitambua ili kuthibitisha madai yao kuwa fomu hizo zilizowasilishwa na walalamikaji siyo halali.
Kutokana na uchaguzi huo wa Serikali za Mitaa, Vitongoji na Vijiji wa mwaka 2024, Chama Cha ACT- Wazalendo kilifungua jumla ya mashauri 51 katika Mahakama za Wilaya mbalimbali zikiwemo Temeke, Lindi, Ilala, Momba, Mkuranga, Mafia, Kigoma na Kibiti, kupinga matokeo na mwenendo wa uchaguzi huo.
Katika mkoa wa Kigoma chama hicho kilifungua jumla ya mashauri 13, huku Manispaa ya Kigoma Ujiji kikifungua mashauri tisa, lakini mashauri matatu, mawili kati yake yakiwa ya Manispaa ya Kigoma yaliyoondolewa mahakamani kwa njia ya mapingamizi.
Walalamikaji wote waliwakilishwa na jopo la mawakili watatu wa kujitegemea Emmanuel Msasa (kiongozi wa jopo) Eliutha Kivyiro na Prosper Maghaibuni.
Walalamikiwa waliwakilishwa na mawakili wa Serikali waliowawakili msimamizi msaidizi na msimamizi wa uchaguzi na mawakili wa kujitegemea watatu waliowawakilisha wenyeviti wanaopingwa, na kufanya idadi ya mawakili wa utetezi kuwa 20.