Lissu ataja masharti kina Mdee kurejea Chadema

Dar es Salaam. Wakati baadhi ya wabunge 19 wa viti maalumu waliofukuzwa na Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema) wakiendelea na harakati za kisiasa kuelekea uchaguzi mkuu wa Oktoba 2025, Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu amebainisha kile kinachopaswa kufanywa iwapo wanataka kurejea.

Lissu amesema Halima Mdee na wenzake 18 ambao walivuliwa uanachama Novemba 27, 2020 na Kikao cha Kamati Kuu wanapaswa kufuata katiba ya chama hicho na si vinginevyo.

Wabunge hao walifukuzwa Chadema na kukata rufaa Baraza Kuu la chama hicho dhidi ya uamuzi huo wa Kamati Kuu. Baraza Kuu lililokutana Mei 11, 2022 katika ukumbi wa Mlimani City, jijini Dar es Salaam lilitupilia mbali rufaa yao.

Mdee na wenzke walivuliwa uanachama wakituhumiwa kwa usaliti, kughushi nyaraka za chama kisha kujipeleka bungeni jijini Dodoma kuapishwa na aliyekuwa Spika wa wakati huo, Job Ndugai.

Baada ya uamuzi wa Baraza Kuu, walikwenda mahakamani ambako walikuwa na ombi la kufungua shauri Mahakama Kuu. Kesi ilichukua hatua mbalimbali na ilibatilisha uamuzi wa Baraza Kuu lililobariki kuvuliwa uanachama na kuendelea na ubunge wao.

Mwenyekiti wa Chadema,Tundu Lissu akizungumza na waandishi wa habari wa Mwananchi,nyumbani kwake jijini Dar es Salaam.Picha na Michael Matemanga

Mbali na Mdee aliyekuwa mwenyekiti wa baraza la wanawake wa Chadema (Bawacha), wengine ni waliokuwa wajumbe wa Kamati Kuu, Ester Bulaya na Esther Matiko pamoja na aliyekuwa katibu mkuu wa Bawacha, Grace Tendega.

Katika orodha hiyo, wamo pia Hawa Subira Mwaifunga, aliyekuwa makamu mwenyekiti wa Bawacha (Bara); Agnesta Lambat, aliyekuwa katibu mwenezi, Asia Mwadin Mohamed, aliyekuwa naibu katibu mkuu wa Bawacha Zanzibar, na Katibu Mkuu wa Bawacha-Bara, Jesca Kishoa.

Pia wamo  aliyekuwa katibu mkuu wa Baraza la Vijana (Bavicha), Nusrat Hanje na aliyekuwa mwenyekiti wa Chadema mkoani Mtwara, Tunza Malapo, Cecilia Pareso, Naghenjwa Kaboyoka, Sophia Mwakagenda, Kunti Majala, Salome Makamba, Anatropia Theonest, Conchesta Lwamlaza, Felister Njau na Stella Siyao.

Kati ya kundi hilo, baadhi wamekwisha kuonyesha mwelekeo wa kusaka majukwaa mengine ya kisiasa ili kuwapa fursa ya kuwania ubunge katika uchaguzi ujao wa Oktoba 2025 ikiwemo Chama cha Mapinduzi (CCM).

Wapo ambao wanaelezwa watakwenda ACT-Wazalendo na huko nyuma Katibu Mkuu wa chama hicho, Ado Shaibu alikwisha kufungua milango kwa Mdee na wenzake 18 wanaotaka kujiunga nao wako tayari kuwakaribisha.

Hata hivyo, wapo ambao watatundika daruka za kisiasa na wengine wanakusudia kurejea Chadema kuendeleza harakati zao. Lakini hilo linawezekanaje kurejea Chadema? Lissu anabainisha hatua kwa hatua wanayopaswa kufanya.

Jana Jumapili, Februari 23, 2025, Lissu amefanya mahojiano maalumu na waandishi wa Kampuni ya Mwananchi Communications Limited (MCL) nyumbani kwake Tegeta, jijini Dar es Salaam pamoja na mambo mengine aliulizwa juu ya kipi wakifanye kina Mdee ili kurejea Chadema.

Lissu amesema kuna watu wanapigiana simu kuhusu hilo, lakini hakuna mazungumzo yoyote yamefanyika kuwahusu wabunge hao na au waliofika kumweleza yeye kama mwenyekiti wa chama.

“Najua yamezungumzwa mengi mitandaoni, lakini mimi kama mwenyekiti sijaletewa hoja yoyote ya aina hii. Nirudie tu ambacho nimekisema sana, wakitaka kurudi wala hawahitaji kuleta chochote kwangu,” amesema Lissu.

Akifafanua msingi wa hoja hiyo, Lissu amesema kuna dhana kwamba yeye Lissu ndiye amewawekea kigingi wabunge hao kurejea Chadema.

“Haya maneno yalikuwepo kabla hata sijawa mwenyekiti, yalisemwa kwamba kama isingekuwa Lissu wangekuwa wamesharudi. Maana yake hao watu wanataka kuaminisha watu kwamba hiki chama mwenye kauli ni mtu mmoja, inawezekanaje,” amehoji Lissu.

“Maana yake mheshimiwa (Freeman) Mbowe alivyokuwa mwenyekiti kwamba alikuwa hana kauli kwenye hili isipokuwa huyu jamaa (Lissu) peke yake? huko ni kunipa ukubwa ambao sijawahi kuwa nayo,” amesema.

Lissu akisisitiza kauli yake amesema, wabunge hao wakitaka kurudi Chadema hawahitaji kuhangaika na mwenyekiti wa chama: “Utaratibu unasema hivi, mwanachama aliyefukuzwa akitaka kurudi atakakwenda kuomba msamaha au kuomba kurudi kwenye kikao kilichomvua uanachama.”

“Hicho kikao kitamsikiliza, kikubaliana na maombi yake kitapekelea mapendekezo kwenye kikao cha juu, hawa walifukuzwa na baraza kuu, kabla walifukuzwa na kamati kuu ndipo baraza kuu likaridhia,” amesema.

Amesema mahali pa kuanzia wakitaka kurudi sio kwa mwenyekiti ni kwenye baraza kuu tena kwa kuandika barua ya kuomba kurudishiwa uanachama kwa katibu mkuu ambaye naye katika ajenda za baraza kuu ataweka na hiyo kama sehemu ya ajenda, baraza kuu litajadili.

“Mimi ni mwenyekiti wa Baraza Kuu, lakini wenye uamuzi kwenye hili ni wajumbe Baraza kuu. Hata nikisema siwataki kabisa, japo sijawahi kusema hivyo lakini hata nikisema bado nitawauliza wajumbe wa Baraza kuu wanaoafiki waseme ndiyo na wasioafiki waseme sio na kutoa majibu,” amesema.

Katika msisitizo kwenye hilo, Lissu amesema uamuzi wa kuwarudisha au kutowarudisha sio wake peke yake: “Watu wanaweza wakawa wanaliwa hela zao kama hawataangalia.”

Msingi wa hoja hiyo ni wale watu ambao watafika na kuwaeleza wawapatia fedha ili wakazungumze na mwenyekiti (yeye) kumlainisha akisema hilo halipo, bali kama wanahitaji kurudi utaratibu ni huo kikatiba.

“Wakifanya hivi wataliwa hela zao bure, njia ya kupita ni kumuandikia katibu mkuu na Baraza kuu ndilo litaamua. Mimi ni mtu mmoja tu, yes (ndiyo) kauli yangu inaweza ikaenda mbali lakini bado ni kauli ya mtu mmoja, wakitaka kurudi, waombe kwa katibu mkuu wakishaoamba sasa ndipo wanaweza kuja kwangu.

“Wakisema saaa mwenyekiti sisi tumekwishajisalimisha kwa Katibu mkuu, tunaomba kwenye kikao upotezee hii ajenda itakapokuja kwenye kikao, kama unaona ni vigumu kusema turudi, angalau usiseme tusirudishwe, hii ni lobbying inawezekana,” amesema huku akitabasamu.

Related Posts