Na Farida Mangube,Morogoro
MAHAKAMA Kuu ya Tanzania Kanda ya Morogoro imetupilia mbali shauri la madai namba 5 la mwaka 2023, kesi iliyofunguliwa na Nkumbi Marashi Holela na wenzake 47 chini ya Wakili wao Yudathade Paul dhidi ya Mussa Ginawele na Anna Ballali walio kuwa wakiwakilishwa na Wakili Rabin Mafuru kuhusu umiliki wa shamba namba 512 lenye hati ya miliki wa aliyekuwa Gavana wa Benk kuu ya Tanzania Daud Balali.
Kesi hiyo iliyokuwa ikisikilizwa na Jaji Muruma ilitolewa hukumu na Naibu Msajili wa Mahakama Kuu Kanda ya Morogoro Suzan Kihawa Februari 21 mwaka huu baada ya Mahakama kukamilisha taratibu zote ikiwemo kusikiliza ushahidi uliowasilishwa na pande zote mbili.
Ambapo amesema upande wa walalamikaji wameshindwa kuithibitishia Mahakama madai saba waliyowasilisha mahakamani hapo.
Madai saba yaliyowasilishwa mahakamani hapo ni pamoja na eneo lenye mgogoro litamkwe kuwa linamilikiwa na walalamikaji, kitendo cha wadaiwa kuripoti polisi na kufanya alasemiti kitamkwe kwamba kimewanyima haki ya umiliki.
Madai namba mbili hamiliki ardhi katika eneo lenye mgogoro , malipo ya fidia kiasi cha Sh.million sita kutokana na usumbufu wa kisaikolojia na amri ya gharama ya uendeshaji wa kesi pamoja na riba ya asilimia 12 ya kiasi kilichombwa kutoka siku ya hukumu mpaka kitakapolipwa .
Baada ya kusikiliza pande zote mbili imeamuriwa upande wa walalamikaji umeshindwa kuithibitishia Mahakama hiyo , hivyo kutoa haki kwa Christopher Ginawele na Anna Ballali.
Wakati nje ya Mahakama ,Wakili wa upande wa wadaiwa Rabin Mafuru amesema wameridhishwa na hukumu hiyo ambayo ni udhihirisho kuwa Mahakama za Tanzania zinaendelea kusimamia haki,ingawa kuna wakati inachelewa lakini mwisho inapatikana
Ameongeza hata kabla ya kesi hiyo kulikuwa na kesi kadhaa tangu mwaka 2017 kutoka kwa watu hao hao lakini kesi hizo hazikufikia hatua za kusikilizwa kutokana na upungufu wa kisheria.
Pia amesema kuwa haki inapotendeka inaongeza heshima na funzo kwa wengine wenye tatia kama hizo huku akikiri kuwepo uhitaji mkubwa wa maboresho katika sheria hususani za umiliki ardhi na namna ya kushughulikia migogoro ya ardhi kwani bado kuna mianya mingi inawapa nguvu wavamizi wa ardhi dhidi ya wamiliki halali wenye nyaraka.
“Kulinganisha mtu mwenye hati na asiye na hati sioni kama tunamtendea haki mmiliki wa hati na serikali iliyotoa hiyo hati, naelewa msingi wa hatua za kisheria katika kutatua migogoro, hizi sheria inabidi tuzifanye ziendane na mazingira yetu…
“Kwani wavamamizi wanatumia hii mianya kupeleka madhara na hasara kwa wamiliki halali wenye nyaraka, kama wakili ni sehemu ya mahakama ,natoa maoni kama mdau wa haki,Bunge ndio lenye wajibu wa kufanya marekebisho ya sheria,kuona kama kuna haja ya kuendelea na taratibu za kisheria tulizorithi kwa Wakoloni,”amesema Wakili Rabin Rutabhu Mafuru.
Kwa upande wake Mwakilishi wa upande wa washitaki Nkumbi Holela akizungumza kwa njia ya simu amesema wamepokea hukumu hiyo na bado wapo katika majadiliano kama watakata rufaa kuendelea na shauri hilo katika ngazi nyingine ya Mahakama au laa.
“Tumepokea hukumu kwa vile Mahakama ndio yenye uamuzi wa mwisho wa kutoa haki, tumeipokea ila kwa upande wetu bado kidogo tunamjadala kuhusu kukata rufaa.”
Kesi hiyo Namba 5 ya mwaka 2023 ilifunguliwa na Wakulima 48 wakazi wa kiongozwa na Nkumbi Marashi Holela dhidi ya wadaiwa wawili Mussa Ginawele (Msimamizi wa Shamba) na Anna Muganda Ballalli ambaye ni mjane wa marehemu Daudi Ballali aliyekuwa Gavana ya BoT.
Kesi hiyo ilifunguliwa Mahakama Kuu ya Tanzania kanda ya Morogoro na kusikilizwa na mbele ya Jaji Mruma.