Arusha. Mkuu wa Mkoa wa Arusha, Paul Makonda amewaagiza viongozi wa Jiji la Arusha kwa kushirikiana na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya na Katibu Tawala, kufanya uchunguzi wa tuhuma za jaribio la wizi wa Sh252 milioni zinazodaiwa kutaka kuchotwa kwenye akaunti ya Serikali kwa kigezo cha kwenda kununua eneo la kujenga shule kata ya Muriet.
Agizo hilo la Makonda linakuja ikiwa imepita siku moja tangu Mbunge wa Arusha Mjini, Mrisho Gambo alipoibuka na taarifa za jaribio la wizi wa fedha hizo zilizobambikwa kwenye mahitaji ya ununuzi wa eneo lenye ukubwa wa ekari sita kwa ajili ya ujenzi wa shule, badala ya thamani halisi ya Sh300 milioni.
Akifungua kikao cha siku mbili cha baraza la madiwani kwa ajili ya kujadili mapendekezo ya mpango na bajeti ya Jiji la Arusha kwa mwaka wa fedha 2025/2026, kilichoanza leo Februari 24, 2025, Makonda amesema anataka uchunguzi ufanyike na wahusika wote wachukuliwe hatua za kisheria.
“Jana, nimekaa nasoma mahala, naona taarifa za ununuzi wa eneo la shule, halafu kuna Sh252 milioni zinataka kupigwa, nikajiuliza hii vipi tena? Sasa, Mstahiki Meya, baadaye nataka kupata taarifa ya jiji, hizo Sh252 milioni zinazosemwa, zimepigwa, ziko wapi na waliojaribu kuiba hizo hela nataka niwakute kituo cha polisi.
“Namaanisha kuwa nataka mkimaliza kikao tu hapa, meya, mkuu wa wilaya, mkurugenzi na DAS, kama ni taarifa sahihi ifanyiwe kazi haraka iwezekanavyo na tuwajue walioiba hizo hela na hatua zichukuliwe,” amesema.
Makonda ameongeza kuwa wananchi wanalipa kodi, kuna barabara haijajengwa lakini kuna Sh252 milioni zimepigwa mahala. Amehoji kama wanaweza kupewa tena fedha wakiomba kama hizo zimeibiwa.
“Naomba Takukuru (Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa) waanze kufanya yao na mtandao wote wa usalama na kama kuna mtumishi wa umma amehusika na taarifa zake zipo, wasimamishwe na uchunguzi uanze,” amesema Makonda.
Wakati huohuo, Makonda amewaonya wajumbe wa baraza hilo kuacha kuzungumza mambo ya ndani ya jiji kwenye mikutano ya hadhara na badala yake wawasilishe kwenye vikao, ili yafanyiwe kazi haraka na kutatuliwa.
“Najiuliza kwa nini mtu unaenda kuongelea kwenye mikutano ya hadhara, kwa nini msikae kwenye vikao mkasema? Sasa mkiwaambia wananchi hivyo, si wanawaona nyie wote wezi? Ndio maana nasema, jamani kaeni kwenye vikao ili taarifa kama hizi mnasulubiana hukuhuku wenyewe na mambo mazuri yanaenda kwa wananchi,” amesema.
Awali, kwenye mkutano wa hadhara wa kutambulisha eneo lililonunuliwa kwa ajili ya ujenzi wa shule ya kata ya Muriet, Gambo alifichua taarifa hizo za madai ya wizi wa Sh252 milioni zilizobambikwa kwenye mahitaji ya manunuzi ya eneo la ekari sita kwa ajili ya ujenzi wa shule katika kata ya Muriet, jijini Arusha.
Wizi huo unadaiwa kutaka kutekelezwa na baadhi ya watendaji wa halmashauri ya jiji la Arusha, baada ya kudai Sh552 milioni kwa ununuzi wa eneo hilo badala ya thamani halisi ambayo ni Sh300 milioni.
Akizungumza kwenye mkutano wa hadhara, Gambo alisema eneo hilo lilitakiwa kununuliwa kwa muda mrefu, lakini kutokana na mvutano wa kuokoa fedha za Serikali, ilisababisha lichelewe. Eneo hilo lililokuwa linunuliwe mwaka 2022, limenunuliwa Desemba mwaka 2024.
“Tunatambua changamoto mnayopitia lakini ununuzi ulichelewa kutokana na tatizo la fedha kutaka kupigwa ndio maana tukasimama kidete kutetea wizi wa zaidi ya Sh252 milioni ambazo zilitaka kupigwa na baadhi ya watendaji ambao sio waaminifu.”
“Tumefanya hivyo kwa sababu tunathamini namna ambavyo Rais wetu Samia Suluhu Hassan anavyohangaika dunia nzima kutafuta fedha kwa ajili ya kuwahudumia Watanzania, hivyo ni wajibu wetu kama wasaidizi wake kuzisimamia, kuzilinda ili zikatumike kwa mujibu wa malengo,” amesema.
Naye mwenyekiti wa maendeleo ya jamii jiji la Arusha, Issaya Doita, akielezea namna fedha hizo zilivyokuwa zinataka kupigwa, amesema mwaka 2022 walipokea kilio cha uhitaji wa shule katika eneo la Muriet mashariki na baraza la madiwani kupitisha ajenda hiyo na kupewa tathimini ya gharama za eneo kuwa ni Sh552 milioni.
“Wengi tulishtuka kutokana na asili ya eneo kuwa pembezoni na baadhi yetu akiwemo mbunge, tulifanya utafiti wa chinichini, ndiyo tukagundua mnyororo wa madalali walioshirikiana na baadhi ya watendaji na madiwani wa halmashauri yetu kupandisha gharama za eneo.
“Tulitoa taarifa kwa Takukuru na kusitisha ununuzi wa eneo hilo huku baadhi ya watu hao wakihojiwa na baadaye kwa ushirikiano na mkurugenzi aliyekuwepo wakati huo, Juma Hamsini, tulimpata mwenye eneo na kulinunua kwa gharama ya Sh300 milioni,” amesema.