Malkia Zahra aeleza kilichomsukuma Aga Khan kuanzisha vyuo vikuu

Dar es Salaam. Malkia Zahra Aga Khan amesema elimu ni nguzo muhimu ambayo Mtandao wa Maendeleo wa Aga Khan (AKDN), umekuwa ukiupa kipaumbele kwa kuwa ndio msingi wa kuboresha maisha ya wananchi.

Malkia huyo amesema baba yake alianzisha vyuo vikuu viwili ambavyo ni Chuo Kikuu cha Aga Khan (AKU) na Chuo kikuu cha Asia ya Kati (UCA),  kwa lengo la kuimarisha mfumo wa elimu.

Kauli hiyo ameitoa leo Februari 24,2025 Dar es Salaam katika mahafali ya 20 ya Chuo Kikuu Cha Aga Khan 2024,  ambapo zaidi ya wahitimu 71 wametunukiwa shahada  mbalimbali katika fani ya elimu, uuguzi, ukunga pamoja na uongozi wa sekta ya habari.

Katika mahafali hayo,  chuo hicho kilitoa heshima kwa mwanzilishi na mkuu wa  kwanza wa kwanza wa chuo,  hayati Aga Khan wa nne na kumkaribisha mrithi wake mfalme  Rahim Aga Khan wa tano.

Kufanyika kwa mahafali hayo,  Malkia Zahra amesema ilikuwa ni fahari kwa baba yake kuona kila mtu amehitimu elimu yake ndani ya chuo hicho,  huku akidokeza  wahitimu wa mwaka huu ndio wa mwisho kusoma chini ya busara ya baba yake.

“Naishukuru Serikali ya Tanzania kwa kutupa imani kwa muda mrefu hasa katika utekelezaji wa maono ya taasisi yetu ya  kufungua fursa sekta ya elimu na kuboresha sekta ya afya,”amesema.

Wahitimu wa Chuo kikuu cha Aga Khan wakiingia katika ukumbi wa Diamond Jubilee jijini Dar es Salaam leo Jumatatu Februari 24, 2025 wakati mahafali ya 20 ya chuo hicho. Picha na Sunday George

Malkia Zahra amesema baba yake aliamini zaidi katika ubunifu wa watu pamoja na kuunganisha nguvu pamoja kukabiliana na changamoto za dunia na kujenga jamii yenye nguvu zaidi.

“Baba yangu alianzisha na kusimamia taasisi na programu nyingi bora zilizolenga kuimarisha uwezo wa binadamu, ustawi, kujenga jamii imara na kulinda mazingira asili,”amesema.

Malkia Zahra amewashukuru wahitimu na wanafunzi wa Aga Khan ambao wamekuwa kioo duniani kote kwa kuyaishi kwa vitendo maono ya mwanzilishi wa chuo hicho,  kwa namna wanavyokabiliana na changamoto za maisha na kutoa huduma bora kwa wananchi wanaowahudumia.

Awali akimkaribisha Malkia Zahra, Rais wa Chuo Kikuu Cha Aga Khan Sulaiman Shahabuddin,  amesema mahafali ya chuo hicho yaliyofanyika hivi karibuni katika nchi za Kenya, Uganda,Pakistan, jumla ya wanafunzi  850 wamehitimu.

Amesema wahitimu hao ni katika fani mbalimbali za ualimu, uongozi katika vyombo vya habari, uuguzi pamoja na ukunga.

“Watatoa huduma za afya za hali ya juu na nidhamu ndani ya hospitali, shule, mashirika ya vyombo vya habari, na taasisi za kiraia na watapanua mipaka ya maarifa ya kimataifa na kuendeleza bunifu kutatua shida zilizopo kwenye jamii,”amesema.

Rais huyo amesema Chuo Kikuu cha Aga Khan kitaendelea kushirikiana na Hospitali ya Aga Khan,  ili kujenga mfumo wa afya shirikishi kwa nchi za Afrika Mashariki.

“Nchini Tanzania, mfumo wa afya wa AKDN unajumuisha hospitali mbili na vituo 22 vya afya vinavyohudumia takriban wagonjwa milioni moja kila mwaka,hii inatupa mazingira mazuri  kwa utoaji wa huduma za afya, elimu na utafiti.

Naye Mkuu wa Chuo Kikuu Aga Khan (AKU) Dk Eunice Pallangyo amesema idadi ya wahitimu katika chuo hicho ni 71, akisisitiza elimu inayotolewa chuoni hapo ni bora na sio bora elimu.

“Jambo ambalo tunahimiza kwa wanafunzi wetu ni ubora kwa kile wanachokifanya na wawe wa kwanza kuleta mabadiliko popote wanapokuwepo na kutumia akili zao kufanya vitu kwa ubora, “amesema.

Related Posts