Dar es Salaam. Hekaheka za uchaguzi mkuu zinaendelea kushika kasi huku vyama vya siasa vikiendelea na mchakato wa kuwapata wagombea wa nafasi ya urais.
Kwa upande wa Chama cha NCCR Mageuzi, maandalizi yanaendelea wakati Chama cha Mapinduzi (CCM) tayari kimemaliza mchakato wake kwa kumpitisha Rais, Samia Suluhu Hassan kuwa mgombea wake wa urais katika Mkutano Mkuu Maalum uliofanyika Januari 19, 2025, jijini Dodoma.
Katika upigaji kura, wajumbe 1,924 walimpitisha Samia kwa kura zote za ndiyo, sawa na asilimia 100.
Aidha, Katibu Mkuu wa CCM, Dk Emmanuel Nchimbi aliteuliwa kuwa mgombea mwenza, na iwapo chama hicho kitashinda, atakuwa Makamu wa Rais.
Na kwa upande wa Zanzibar, Dk Hussein Mwinyi alipitishwa kuwa mgombea wa urais.
Halikadhalika Kiongozi wa ACT Wazalendo, Dorothy Semu pia alishatangaza nia ya kuwania urais wa Tanzania katika uchaguzi mkuu ujao.
Semu alitangaza nia hiyo Januari 16, 2025 alipokuwa akizungumza na wahariri na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam akisisitiza yupo tayari kumkabili mgombea wa CCM, Samia.
“Ndugu zangu, Tanzania inahitaji uongozi mpya utakaolinda masilahi ya Taifa na uchumi imara, jamii yenye fursa sawa, na uongozi wa uwazi. Tunaweza kubadilisha hali hii kwa kushirikiana, kuondoa changamoto hizi, na kuimarisha mustakabali wa Taifa letu.
“Niko tayari kumkabili Samia Suluhu Hassan kwenye uchaguzi wa 2025 endapo chama changu cha ACT Wazalendo kitanipa ridhaa,” amesema Semu.
Mbali ya Semu, naye Mwenyekiti wa ACT Wazalendo na Makamu wa Kwanza wa Rais wa Zanzibar, Othman Masoud Othman, ameshatangaza rasmi nia yake ya kugombea nafasi ya Urais wa Zanzibar katika Uchaguzi Mkuu ujao.
Othman alitamgaza nia hiyo Januari Mosi, 2025 visiwani Zanzibar, huku akisema kwa heshima kubwa na kwa kufuata taratibu za chama chake cha ACT Wazalendo, atakiomba kumpatia dhamana ya kupeperusha bendera katika nafasi ya kuwania Urais wa Zanzibar.
“Napenda kwa heshima kubwa kutumia fursa hii kutangaza rasmi kwamba nimekusudia, inshaAllah, itapofika wakati wa kuanza mchakato wa kutafuta wagombea katika chama changu, kwa kufuata taratibu zilizopo, kukiomba chama changu cha ACT Wazalendo kinibebeshe dhamana ya kukiwakilisha kwenye nafasi ya kuwania uongozi wa juu wa nchi yetu, Zanzibar,” alisema Othman.
Kwa upande wa NCCR Mageuzi, Mkuu wa Idara ya Oganaizesheni na Utawala wa chama hicho, Florian Mbeo, akizungumza leo Jumatatu, Februari 24, 2025 na Mwananchi kwa simu, amesema baada ya kikao cha Kamati Kuu kilichofanyika Februari 18, 2025, iliamuliwa Aprili 30 ndiyo siku ambayo chama hicho kitamtangaza rasmi mgombea wake wa urais kwa Tanzania Bara na Zanzibar.
Tarehe hiyo pia imepangwa kwa ajili ya Mkutano Mkuu wa chama na miongoni mwa ajenda zitakazojadiliwa ni uteuzi wa wagombea wa nafasi ya urais Jamhuri na Zanzibar.
Mbeo ameongeza kuwa kikao hicho pia kiliridhia kuwa Aprili 30 itakuwa siku ya mkutano mkuu wa uchaguzi.