Kilwa. Mtalii aliyepotea katika bahari ya Hindi Kisiwa cha Songosongo wakati akifanya utalii amepatikana akiwa hai katika eneo la Kilwa Kivinje wilayani Kilwa mkoani Lindi.
Raia wa kigeni kutoka nchini Ufaransa, Nakar Fszman (51), amepatikana akiwa hai baada ya kupotea katika Bahari ya Hindi, eneo la Kisiwa cha Songosongo, Wilaya ya Kilwa.
Taarifa ya Jeshi la Polisi Mkoa wa Lindi inasema Fszman alipotea Februari 23, 2025, wakati akifanya utalii kwa kutumia boti aina ya Kayati maarufu kama Kidau, inayotumia kasia. Mtalii huyo aliwasili nchini Februari 16, 2025, akiwa na mkewe na watoto wawili.
Fszman amepatikana Februari 24, 2025, saa tatu asubuhi, katika pwani ya Kilwa Kivinje, umbali wa maili nane za baharini (takriban kilomita 12.9) kutoka alikopotea. akiwa hai na mwenye afya njema baada ya juhudi za kikosi cha wanamaji cha Jeshi la Polisi (Marine), kilichofanya msako mkali baharini.
Taarifa hiyo imeeleza sababu ya mtalii huyo kupotea ni kutokana na upepo mkali na mawimbi yaliyosababisha boti kuelea.

Taarifa za awali zinaeleza kuwa mtalii huyo alipotea kutokana na upepo mkali na mawimbi yaliyosababisha boti yake kuelea mbali. Jeshi la Polisi limewataka wananchi kuchukua tahadhari wanapoona hali mbaya ya hewa kwa kuepuka safari za baharini hadi upepo utakapopungua.
Fszman amefanyiwa uchunguzi wa kitabibu na daktari wa Hoteli ya Fanjove Island, ambako alikuwa amefikia, na kuthibitishwa kuwa yuko katika hali nzuri. Tayari ameungana na familia yake na anaendelea vizuri.