Shirika la Habari la AP, usiku wa kuamkia leo, Jumatatu, Februari 24, limeripoti kuwa Papa Francis yupo mahututi huku vipimo vya damu vikionyesha dalili za awali za ugonjwa wa figo kushindwa kufanya kazi.
Hata hivyo, bado yuko macho na anatambua watu, na aliweza kuhudhuria misa ya Jumapili, Vatican imesema.
Kiongozi huyo wa Kanisa Katoliki mwenye umri wa miaka 88 anapambana na ugonjwa wa nimonia na maambukizi ya mapafu.
Katika taarifa ya mwisho ya usiku wa kuamkia leo, Jumatatu, Februari 24, Vatican ilisema kwamba Papa hajapata matatizo zaidi ya kupumua tangu Jumamosi usiku, lakini bado anapewa oksijeni kwa kiwango cha juu.
Vipimo vingine vya damu vimeonyesha dalili za awali na dhaifu za kushindwa kwa figo, lakini madaktari wamesema hali hiyo ipo chini ya uangalizi na inadhibitiwa.
Wakati huohuo, maombi kwa ajili ya Papa yameendelea kumiminika kutoka kila kona ya dunia, kuanzia nchi yake ya asili ya Argentina, makao makuu ya Uislamu wa Kisunni huko Cairo, hadi kwa watoto wa shule mjini Roma.
Madaktari wamesema hali ya Papa Francis ni ya wasiwasi kutokana na umri wake mkubwa, udhaifu wa mwili, na ugonjwa wa mapafu aliokuwa nao awali.
Hali yake imefufua mjadala juu ya nini kitatokea ikiwa atapoteza fahamu au kushindwa kutekeleza majukumu yake, na iwapo ataamua kujiuzulu.