Profesa Kitila atambua mchango wa waokota taka

Dar es Salaam. Waziri wa Nchi, Ofisi ya Rais, Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo amesema waokota taka wana mchango mkubwa katika maendeleo ya Taifa na wana sehemu yao kwenye Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Profesa Kitila ambaye ni Mbunge wa Jimbo la Ubungo amesema kazi wanayoifanya waokota taka rejeleshi ni kuokoa kizazi cha sasa na baadaye ambacho kingeathirika na wingi wa taka ambao umekuwa kero Dar es Salaam.

Profesa Mkumbo ametoa kauli hiyo leo Februari 24, 2025 wakati akifungua mkutano wa mwaka wa waokota taka rejeleshi jijini Dar es Salaam ulioandaliwa na Mtandao wa Waokota Taka Rejeleshi Dar es Salaam (Mtawada).

“Kazi mnayoifanya mnatoa mchango mkubwa kulifanya Jiji la Dar es Salaam likae vizuri, mnaokoa sio vizazi vya leo, hata vya kesho. Tutakapozindua Dira ya Maendeleo ya 2050, mle ndani kuna mambo mengi lakini jambo kubwa ni ulinzi wa mazingira, kwa hiyo kazi mnayoifanya mnaisaidia Serikali kutekeleza majukumu yake,” amesema.

Mbali na hayo, amesema Tanzania ina changamoto ya ajira kwa vijana, hivyo jitihada zozote zinazofanywa na wananchi kujipatia kipato lazima ziungwe mkono na Serikali.

Katika kuwatafutia fursa waokota taka, Profesa Kitila amesema Serikali inaendelea na mazungumzo na uongozi wa kiwanda cha saruji Tanga kuangalia namna kitakavyoweza kutumia nishati itokanayo na taka.

Amesema kiwanda hicho tayari kinatumia gesi kama chanzo cha nishati na sasa kipo kwenye mpango wa kutumia taka na wanaangalia utaratibu mzuri wa kuanza kuzalisha nishati hiyo.

“Watakapoanza nyie mtakuwa wateja wakubwa wa moja kwa moja wa kiwanda kile, niwaahidi nitapambana sana tuwaunganishe moja kwa moja na mtapata haki yenu,” amesema.

Kuhusu changamoto ya vifaa kwa kundi hilo, Profesa Kitila amesema atazungumza na wadau kuwezesha vifaa vinavyohitajika kwa kundi hilo wafanye kazi yao kwa ufanisi, huku akidokeza kuwa suala la kundi hilo kutoheshimika litakwisha kwani tayari linatambulika.

Awali akisoma risala ya Mtawada kwa mgeni rasmi, Makamu Mwenyekiti wa umoja huo, Said Mohamed amesema changamoto wanayopitia ni kupunjwa malipo yao wanapookota taka rejeleshi.

Ameeleza kwamba wanapookota taka na kufikisha kilogramu 10 kwa siku nzima, mezani huchezewa na kuambiwa mzigo wao ni kilogramu nne na hulipwa Sh1,500, jambo alilosema kwao ni maumivu.

“Adha nyingine tunayopitia ni kudharauliwa na kutothaminika kwenye jamii, tunaitwa waokota makopo na wengine wanatuona wezi na hii imesababisha baadhi yetu kupigwa na wengine kupoteza maisha,” amesema.

Pia, Said amependekeza Serikali iwasaidie kuratibu suala la vipimo vya taka pamoja na kuwasaidia bima ya afya kwani wanafanya kazi kwenye mazingira hatarishi, ombi ambalo Profesa Kitila amesema kero ya vipimo itafanyiwa kazi na Wakala wa Vipimo (WMA) ambayo ina jukumu la kuzikagua.

Ombi lingine alilotoa Said ni Serikali kutoa maelekezo kwa viongozi wa serikali za mitaa kutambua na kuthamini kazi wanazofanya kwani wamekuwa wakiwadharau.

Related Posts